Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya tukio la
leo, Jumapili, Mei 5, 2013 la mlipuko kwenye Kanisa Katoliki la Mt.
Joseph Mfanyakazi la Olasiti Jijini Arusha. Tukio hilo la kigaidi
limesababisha mtu mmoja kupoteza maisha na wengine 40 kujeruhiwa. Rais
Kikwete analaani vikali shambulio hilo lililofanywa na mtu au watu
katili, waovu na wenye dhamira mbaya na nia mbaya kwa Tanzania na watu
wake.
Rais Kikwete ameagiza vyombo vya usalama nchini kumsaka mtu au watu
waliohusika na kitendo hicho kiovu na kuwafikisha kwenye vyombo vya
sheria. Vile vile Rais Kikwete amewataka wananchi wote kuwa watulivu
wakati Serikali na vyombo vyake inaendelea kufuatilia tukio hili.
Tutawasaka popote walipo na kupambana nao bila huruma. Aidha,
tutakabiliana na aina yoyote ya uhalifu nchini iwe ni ugaidi au aina
yoyote ya uhalifu wa namna hiyo au wa namna nyingine, uwe na chimbuko
lake ndani ya nchi ama nje ya nchi yetu. Kamwe hatutakubali kuwaacha
wavuruge amani na usalama wa Tanzania na watu wake. Rais anaamini kuwa
Serikali, kwa msaada na ushirikiano wa wananchi, watu hao watapatikana
na kuadabishwa ipasavyo.
Aidha, Rais Kikwete anatoa rambirambi za dhati ya moyo wake kwa wafiwa
na wale wote ambao wamejeruhiwa katika tukio hilo. Anaungana nao katika
machungu na msiba. Rais pia anawaombea wote walioumia katika tukio hili
wapate nafuu ya haraka na waendelee na shughuli zao za ujenzi wa taifa.
Rais Kikwete vilevile anatoa pole nyingi kwa viongozi na waumini wa
Kanisa Katoliki kwa tukio hili la kusikitisha na kuvurugika kwa ibada na
shughuli yao muhimu ya uzinduzi wa Kanisa lao.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM
5 Mei, 2013