Ilivyokuwa
Watu
walioshuhudia tukio hilo wanasimulia kuwa bomu hilo lilirushwa yapata
saa nne asubuhi wakati mgeni rasmi akijiandaa kufungua jengo la kanisa
baada ya ujenzi wake kukamilika.
Kamanda Sabas alisema mtu aliyerusha bomu hilo alitokea nyuma ya kanisa
hilo la ghorofa na kurusha bomu hilo kwa mkono wa kulia... “Alifanya
jitihada za kupenya ili awafikie viongozi lakini alishindwa kutokana na
wingi wa waumini waliokuwapo kwenye eneo hilo.”
Msemaji wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha, Padri Festus Mangwangi
alisema aliyerusha bomu hilo alishuhudiwa na mtoto mdogo aliyekuwapo
kanisani hapo.
“Kwa mujibu wa maelezo ya mtoto huyo, mtu huyo alikuwa amevaa kanzu
nyeupe pamoja na koti la mvua lenye rangi ya kahawia na alikimbia mara
baada ya kulirusha katikati ya watu. Ametusimulia kuwa mtu huyo baada ya
kurusha bomu lile alikimbia na kuwahadaa watu kwa kuita ‘mwizi mwizi
mwizi…’ akionyesha mbele kama kuna mtu anayemfukuza jambo
lililowazubaisha watu lakini mtoto aliyemwona akirusha bomu aliwaeleza
kuwa ndiye mhusika.”
Akizungumzia tukio hilo, Ndowe ambaye amelazwa Mount Metu, alisema
aliona kitu kikidondoka kanisani na kutoa kishindo kikubwa na watu
kuanza kukimbia ovyo. Alipoteza fahamu kutokana na kutokwa na damu
nyingi.
Debora
ambaye ni Polisi alisema alipoona kitu kikidondoka alibaini mara moja
kuwa ni bomu. Alijeruhiwa mguu na mkono. Elizabeth alisema aliona kitu
kama kibuyu kikianguka chini na kupasuka na baada ya hapo hakujua
kilichoendelea.