Ugaidi Waitesa CCM

Ugaidi waitesa CCM
• Ushahidi wa Mwigulu mbinguni waota mbawa

na George Maziku
Tanzania Daima

   
UAMUZI wa Mahakama Kuu ya Tanzania kumfutia mashtaka ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare, umekiweka katika mazingira magumu Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa.

Mazingira hayo magumu yanatokana na kuwepo kwa taarifa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba, ambaye baadhi ya wachambuzi wanasema ndiye mwasisi wa dhana ya ugaidi wa Lwakatare, alipanga kutumia kesi hii kama turufu ya kuiumiza CHADEMA inayoonekana kuwa tishio kwa chama tawala.

Vyanzo vyetu vya taarifa vinasema CCM ilitumia rasilimali nyingi kuchonga suala hili, ikitarajia kulitumia kuidhoofisha CHADEMA inayoonekana kuimarika hatua kwa hatua na kutishia mustakabali wao kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

CHADEMA sasa ndicho chama kinachoinyima usingizi CCM kiasi cha makada wake kupanga mbinu mbalimbali za kukiua ikiwemo kudai ni chama cha kikabila, kidini na kigaidi; mbinu ambazo huko nyuma walizitumia dhidi ya Chama cha Wananchi (CUF) kilichokuwa tishio.

Licha ya mbinu mbalimbali za kuiua CHADEMA, hali ya mambo bado inaonekana kuwa ngumu zaidi kwa CCM, kwani wananchi wanaonekana kuzipuuza, na hujuma hizi zimekuwa zikivuja kabla ya kutekelezwa.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wamelidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa kukwama kwa mbinu hizo za CCM ni dalili za wananchi kuchoshwa na utawala wa chama hicho na kuimarika kwa CHADEMA, ambayo imejipambanua kuwatafutia wananchi ukombozi wa pili.

Baadhi ya wanachama wa CCM wanaojipambanua kama makada makini, wamesema mbinu za kigaidi anazotumia Mwigulu na wenzake wakidhani wanaidhuru CHADEMA, zinaweza kukimaliza chama chao kwa kuwa wananchi wa sasa wana uelewa mpana kuliko miaka kadhaa iliyopita.

Majigambo ya Mwigulu
Katika hali ya kushangilia hujuma walizokuwa wamepandikiza dhidi ya CHADEMA, huku chama hicho kikisisitiza kuwa tuhuma za ugaidi zilikuwa za kupika, Mwigulu alijigamba bungeni Aprili 12 mwaka huu, kuwa ana ushahidi mzito wa ugaidi wa Lwakatare, na kwamba alikuwa tayari kuutoa popote, duniani au mbinguni.

Mwigulu amekuwa akihusishwa na mikakati ya kuimaliza CHADEMA, na inasemekana anaungwa mkono na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, ambaye amewahi kumsifia kwa jinsi “anavyoichachafya CHADEMA”. Wadadisi wa kisiasa wanasema sifa alizopewa na Rais Kikwete zilichangia kumpatia cheo cha unaibu Katibu Mkuu wa CCM, ambacho anakitumia zaidi kufanya propaganda dhidi ya CHADEMA kuliko kujenga chama chake.

Hata hivyo, tambo zake zimeota mbawa baada ya mahakama kumfutia Lwakatare mashtaka ya ugaidi.
Mei 8, mwaka huu, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam ilimfutia mashtaka ya ugaidi Lwakatare kwa hoja kuwa hapakuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba alikusudia kutenda jinai ya ugaidi kama ilivyodaiwa na jamhuri.

CHADEMA imekuwa ikisema kuwa tuhuma hizo za ugaidi ni za kupanga kwa malengo ya kisiasa, na kwamba Mwigulu ndiye amekuwa akishirikiana na baadhi ya maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa kutengeneza video ya uongo dhidi ya Lwakatare na chama chake.

Hoja ya vyombo vya dola kubambikizia kesi wananchi imeungwa mkono na Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Issa Ponda, ambaye mara baada ya kupewa adhabu ya kifungo cha nje cha mwaka mmoja, alisema ni tabia iliyoota mizizi ya polisi kuwabambikiza kesi wananchi wasio na hatia.

Wakati hoja ya kuwabambikia kesi watu ingali ikiendelea, juzi Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limewatia mbaroni askari wake watatu kwa tuhuma za kumbambikia fuvu la kichwa cha mtu mfanyabiashara mmoja wakimshinikiza awape sh milioni 25 ili wamuachie.

Wakati CCM ikionekana kuhaha kutafuta mbinu za kukabiliana na CHADEMA baada ya kushindikana kwa ugaidi, Katibu Mkuu wa chama hicho kikuu cha upinzani, Dk. Willibrod Slaa aliweka wazi kuwa chama tawala kisitarajie mbinu ilizotumia miaka ya nyuma kuudhoofisha upinzani zitafanya kazi sasa.

Dk. Slaa katika mahojiano yake na Tanzania Daima, katikati ya wiki alisema CHADEMA haitolipa kisasi kwa makada wa CCM wanaofanya mbinu chafu za kuudhoofisha upinzani.

“CCM ilizoea kununua wananchi; zamu hii itakuwa na wakati mgumu, ilizoea kuiibia CHADEMA, sasa mambo ni magumu ijiandae kwa pigo kuu,” alisema.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wamesema kuwa hatua ya mahakama kufuta mashtaka ya ugaidi dhidi ya Lwakatare yameinusuru zaidi CCM kuliko CHADEMA, kwani kama kesi ingeendelea chama hicho cha upinzani kilikuwa kimeandaa ushahidi mkali ambao ungeiumbua CCM, serikali na Jeshi la Polisi.

Waziri afunguka
Tanzania Daima Jumapili, lilimtafuta Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe azungumzie kufutwa kwa kesi ya ugaidi na watu kubambikiziwa kesi, ambapo alisema vyombo vya dola vinatekeleza majukumu yake kulingana na taratibu walizojiwekea.
Alisema serikali haina tatizo na hukumu ya Mahakama Kuu, kwani imetekeleza kazi zake kwa mujibu wa sheria na yeyote anayehusisha na masuala ya siasa huu ni mtazamo wake.

“Mimi ndiye msimamizi wa mahakama, kwahiyo nakubaliana na hukumu ya Lwakatare, najua mahakama imetekeleza wajibu wake na kazi zake kwa mujibu wa sheria, sina tatizo na hukumu hiyo,” alisema Chikawe.

Wanasheria wanena
Akitoa maoni ya mtazamo wa kisheria kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu, wakili na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Helen Kijo-Bisimba alisema sura ya awali kabisa kuhusu mashtaka ya serikali dhidi ya Lwakatare haikuonesha ushahidi wa kutosha au mazingira ya kutendeka kwa kosa la ugaidi.

“Sijaisoma ile hukumu ya Mahakama Kuu ili kujua kwanini jaji alifikia uamuzi huo, lakini ninachoweza kusema kwa uhakika kabisa ni kwamba hapakuwa na ushahidi wowote wa maana wa kuthibitisha kosa la ugaidi, hapakuwa na kosa la ugaidi pale, na nadhani mahakama imezingatia ukweli huo,” alisema Bisimba.

Mmoja wa mawakili wa Lwakatare, Peter Kibatara alisema kuwa kwa sasa wanaandaa mipango ya kumtoa mahabusu kwa dhamana mteja wao, kwani shtaka lililobaki lina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Lwakatare sasa amebaki na shtaka moja tu la kula njama za kutaka kumdhuru kwa sumu Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications, Denis Msacky. Kesi hiyo itatajwa kesho katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Post a Comment

5 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Chadema ni wafa maji. Hawaachi kutapatapa. Honestly hawana tofauti ya Ponda

    ReplyDelete
    Replies
    1. Una virusi vya ugonjwa wa ccmmonia nadhani unahitaji tiba mara moja chademaqune ndio tiba sahihi !

      Delete
  2. CCM kimekuwa chama wahuni, mafisadi na magaidi. Waliokianzisha chama hicho huenda wanapinduka pinduka huko kuzimuni kwa jinsi hali inavyoendelea. Wangejua naona wangeweka vizingiti vya sifa na uwezo wa mtu kuchaguliwa kuiongoza CCM.

    ReplyDelete
  3. Umekulia kwenye mgongo wa ccm wewee imekupeleka USA tatizo watoto wa wakubwa mlifikiri baba zenu wakistafu mtaendelea kubebwa na ccm.kaa tulia siasa mchezo mchafu sio chadema,ccm wala cuf wote wanafanaa.john kagombee wewe tuone mambo yako.

    ReplyDelete
  4. Mfa maji asiyeishi kutapatapa hakika ni ccm..sio wnachma wote wa ccm wasiotimiza wajibu wao na wengine wanakwamishwa na wazito wengine kwa kuhofia mkate wao wa kila siku.hata katika maisha ya kawaida lazima kukubali changes,haiepukiki hat kidogo.the most important thing is how do u deal with those changes???wrong steps u r out!!ccm iliona hili toka mwanzo lkini wamelewa madaraka!
    Mimi hijlishi wewe ni chama gani as long s unatimiza wajibu wako.ccm mmekuwa madarakani miaka nenda rudi ila nchi inazidi kuwa worse n worse,we need changes ofkoz no one is perfect but tumetofautiana.we need new leaders,new party,lets give them a chance(chadema)and see are they going to do what they r preaching?to wat percentage?wataobki serikalini from ccm ni ambao wako makini tu na wannchi tunawajua sana tu.
    Ccm mnaogopa nini kuachia ngazi,mmeshindwa na liko wazi,mgeuzi yanakuja.njooni mtaani tuishi wote muone mzingira wanayoishi wannchi wa kawaida way from those unforgiven fvors u r giving urselves to the maximum!

    Chadema and all other parties dont give up on challenging the goverment for the betterment of the country.

    Mungu ibariki Tanzania,mungu ibariki Chadema.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad