DEREVA wa pikipiki maarufu kama bodaboda, Victor Ambrose, anatuhumiwa
kurusha bomu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi,
Parokia ya Olasiti jijini Arusha, lililosababisha vifo vya watu wawili
na wengine karibu 70 kujeruhiwa.
-
Ambrose mwenye umri wa miaka 20 na mkazi wa Kwa Mrombo, Arusha,
anashikiliwa pamoja na watuhumiwa wengine tisa, wakiwemo raia wanne wa
Saudi Arabia kwa mahojiano zaidi ya kuhusika na tukio hilo.
Taarifa zilizopatikana jana jioni, zilieleza kuwa raia hao wa Saudi
Arabia, waliingia nchini Jumamosi usiku kwa ndege kupitia Uwanja wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), na baada ya tukio Jumapili, waliondoka
nchini kupitia mpaka wa Tanzania na Kenya, Namanga.
Serikali kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel
Nchimbi, ilitoa taarifa hiyo jana bungeni na kueleza namna uhalifu huo
ulivyotendeka kanisani hapo juzi, muda mfupi baada ya ibada kuanza.
Kwa mujibu wa Waziri Nchimbi, uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mlipuko
huo ni bomu. Hata hivyo uchunguzi wa kubaini aina ya bomu lililotumika,
unaendelea kufanywa na Polisi na wataalamu wa Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
“Hadi sasa watuhumiwa sita wanashikiliwa na Jeshi la Polisi. Miongoni
mwao ni Victor Ambrose mwenye umri wa miaka 20 dereva wa
bodaboda...ambaye anatuhumiwa kurusha bomu hilo. “Watuhumiwa wengine
watano waliokamatwa ni raia wa kigeni na Mtanzania mmoja ambao
wanashikiliwa kwa mahojiano,” alisema Dk Nchimbi.
Waziri alitaja waliokufa katika tukio hilo kuwa ni mtoto mwenye umri wa
miaka 16, James Gabriel, aliyefariki usiku wa jana na Regina Kurusei
(45), mkazi wa Olasiti aliyefariki siku ya tukio wakati akipatiwa
matibabu katika Hospitali ya Mount Meru.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alisema waliokamatwa wamefikia 10, na raia hao wa nje ni wa Saudi Arabia.
Alisema pia mtu wa tatu alifariki lakini hakumtaja jina. Kaimu Mganga
Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru, Dk Mariam Murktadha, alifafanua kuwa
kijana Gabriel, alifia Uwanja wa Ndege wa Arusha, akiwa njiani kupelekwa
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Aliongeza kuwa majeruhi walikuwa 66 na hivi sasa wamebaki 34 na wengine wameruhusiwa.
Kwa mujibu wa Dk Nchimbi, majeruhi walikimbizwa Hospitali ya Mount Meru,
wengine Hospitali ya St Elizabeth kwa Father Babu, Hospitali ya Selian
na mwingine alipelekwa katika Hospitali ya Dk Wanjara, Mianzini.
Bomu lilivyorushwa
Akielezea tukio hilo, Waziri Nchimbi alisema lilirushwa wakati mgeni
rasmi, Balozi wa Vatican nchini na Mjumbe wa Baba Mtakatifu, Askofu
Fransisco Padilla, akiwa ametoka nje ya kanisa akijiandaa kukata utepe
kama ishara ya uzinduzi.
Alisema mtu huyo alirusha kitu chenye ukubwa wa ngumi, kwenda eneo
kulipokuwa na mkusanyiko wa watu na baada ya kutua, kulitokea kishindo
na mlipuko mkubwa. Inakadiriwa uzinduzi huo wa Kanisa, ulihudhuriwa na
watu zaidi ya 2,000.
Alisema viongozi wa dini na Serikali waliohudhuria ibada hiyo,
hawakupata madhara yoyote kutokana mlipuko huo. Udini Amewasihi
Watanzania kuwa watulivu wakati vyombo vya dola vikiwasaka walihusika na
shambulio hilo.
Aidha ametaka kila mwenye taarifa za kuwezesha kukamatwa wahalifu hao
azitoe Polisi. Kwa mujibu wa Waziri Nchimbi, siku za hivi karibuni
kumekuwepo jitihada kubwa za watu wachache wasioitakia mema nchi, kutaka
kupandikiza chuki za kidini miongoni mwa Watanzania na kuleta mapigano
na mauaji.
“Sina shaka kuwa shambulio la Arusha ni sehemu ya mikakati hiyo miovu,”
alisema bungeni na kusisitiza kwamba Serikali itachukua hatua kali kwa
mtu yeyote bila kujali hadhi na nafasi yake katika jamii.
Wanasiasa waonywa
Wakati huo huo, Waziri Nchimbi amekemea wanasiasa wanaotafuta umaarufu
wa kisiasa kupitia tukio hilo, akisisitiza kwamba Serikali isilaumiwe
kwa hatua kali za kisheria itakazochukua dhidi ya viongozi wa aina hiyo.
“Kokote duniani tukio la kushitukiza linalosikitisha na kuhuzunisha kama
hili linapotokea, wananchi wote huungana na kuwa wamoja kama taifa na
kulaani wahusika na kuwafariji waathirika wa tukio hilo,” alisema Dk
Nchimbi.
Akikemea wanasiasa wanaotumia matukio kujinufaisha, huku akitoa mfano wa
Marekani na kusema mgombea mmoja wa urais wakati wa uchaguzi mkuu wa
mwaka 2012, aliishutumu Serikali kutokana na kulipuliwa kwa ubalozi wa
Marekani nchini Libya.
“Ni wazi kuwa mgombea huyo alichukua tatizo lile kama ajenda ya kisiasa.
Hata hivyo alishutumiwa vikali na Wamarekani wenzake kwa kuelezwa kuwa
ni mtu mwenye kukosa kabisa misingi ya uaminifu na uzalendo kwa taifa
lake.”
“Serikali inasikitishwa sana na wanasiasa wa aina hii, ambao
wanajitokeza nchini na kutafuta umaarufu wa kisiasa kwa gharama za
maisha ya Watanzania…Serikali isilaumiwe kwa hatua kali za kisheria
itakazochukua dhidi ya viongozi wa aina hii, ambao maslahi yao ni muhimu
kuliko maisha ya Watanzania,” alisema.
Dk Nchimbi alilaani waliohusika kufanya uhalifu huo na kusema Serikali
kwa nguvu zote itahakikisha watuhumiwa wote waliohusika na kushiriki kwa
namna yoyote katika tukio hilo, wanasakwa popote walipo na kufikishwa
katika vyombo vya sheria.
“Tunawataka viongozi wa kisiasa, kidini na wananchi wote kwa ujumla kila
mmoja kwa nafasi yake kuwajibika, ili kuhakikisha kuwa nchi yetu
inaendelea kuwa kisiwa cha amani na utulivu,” alisema.
Imeandikwa na Stella Nyemenohi, Dodoma na Veronica Mheta, Arusha.
Source: Habari leo
Victor Ambrose ndie aliyerusha bomu kanisani !
0
May 08, 2013
Tags