Timu hizo zinakutana kufunga msimu, huku Yanga
ikiwa tayari imeshatawazwa ubingwa kabla hata ya mechi kumalizika na
Simba ikijihakikishia nafasi ya tatu kutegemea matokeo ya mchezo huo.
Juzi jioni Naibu Spika Job Ndugai, alitangaza
bungeni wakati akisoma ujumbe wa maandishi wa Mbunge wa Korogwe
Vijijini, Stephen Ngonyani, aliouandika akitaka Ndugai kuwatangazia
wabunge wanaoishabikia timu hiyo kukutana.
“Kuna mambo muhimu sana lazima niyatangaze sasa
hivi, Mheshimiwa Ngonyani anawatangazia wabunge wote mashabiki wa Simba
kesho (jana) wakutane kule wanakokutana Msalato kwa ajili ya kupanga
mikakati,” alisema Ndugai.
“Hapa nimekaa na mwenyekiti wa Simba, Aden Rage na
yeye kaniambia wale wote (Waziri wa Ujenzi John Magufuli) na Naibu wake
(Gerson Lwenge) ni Simba pia,” alisema Mbunge wa Mbinga Magharibi, John
Komba (CCM) wakati akichangia hotuba ya Wizara ya Ujenzi.
Juzi, Mbunge wa Urambo Magharibi, Juma Kapuya,
alimshauri Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage kuwataka yosso
wa Simba kuwafunga ‘babu’ zao wa Yanga.
Wabunge mashabiki wa Simba ni Rage (Mwenyekiti wa
Simba), Ndugai (Kongwa), Ngonyani, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta (Urambo Mashariki), Kapuya, Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema).
Idd Azzan (Kinondoni), Naibu Waziri wa Habari,
Utamaduni na Michezo, Amos Makala (Mvomero), Murtaza Mangungu (Kilwa
Kaskazini) Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge, ( Njombe Magharibi),
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima, (Mkuranga) na
Waziri wa Ujenzi, John Magufuli.
Wakati huohuo, mashabiki wa Simba wametakiwa
wasiwe na hofu na wajazane uwanjani kuona timu yao ikiwaadhiri watani
wao wa jadi, Yanga.
Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Liewig na msaidizi
wake, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ walitamba jana mjini Zanziba kuwa Simba
iko imara na itaibwaga Yanga.