Nazungumzia juu ya
tabia za baadhi ya watu walio katika uhusiano kupenda kuwapiga 'mizinga'
sana wenzi wao. Tabia hii ipo zaidi kwa upande wa wanawake, ingawa siku
hizi hata wanaume nao wameingia katika mkumbo huu.
Siyo ajabu kumsikia mwingine akisema; "Mimi nina kibuzi changu bwana
kila ninachotaka kinanipa, kinajua kisiponipa nitakitosa tu, yaani
nakichuna kama sina akili nzuri, maisha yanaendelea. Yaani ni full
kujiachia."
Si hivyo tu, wapo wanaume ambao ni kero kwa wapenzi wao, yaani wamegeuka
wanaume kama mabinti kwa tabia zao za kutegemea kupewa kila kitu na
wapenzi wao hata kama wanao uwezo wa kuvipata vitu hivyo kama
watajishughulisha.
Unaweza kumsikia mwanaume akisema; "Aaah! Yule demu kazimika ile mbaya
na mapigo yangu, kila ninachotaka ananinpa anajua akinizingua namtosa,
hadi mshahara wake akipata ananigawia. Yule ndiyo mwanamke wa kuwa naye
bwana!"
Ninachotaka kusema leo ni kwamba, mapenzi ya kweli hayana uhusiano
wowote na pesa, ukiona mpenzi wako anaweka pesa mbele na ukishindwa
kumpatilizia anachokitaka anakasirika, jua penzi lake lina walakini,
hakupendi bali anataka kukutumia kisha kukuacha.
Katika mapenzi hatukatai suala la kusaidiana, mpenzi wako akiwa na shida
fulani akaomba umsaidie, kama unao uwezo msaidie na kama huna mueleze
kwamba huna kisha muangalie jinsi gani mnaweza kusaidiana katika kutatua
tatizo linalomkabili.
Itakuwa sio busara kama utakuwa na tatizo lakini ukaona kwamba
ukimweleza mpenzi wako ataona kwamba unamchuna. Wapenzi wanaopendana kwa
dhati hawachunani bali wanasaidiana, na hili ni kwa pande zote mbili.
Kinachokera ni kutoishiwa na matatizo na wakati mwingine unakuta kuchuna
kwingine ni kwa mambo ya starehe. Yaani sasa hivi umemuomba mpenzi wako
vocha, hajakaa vizuri umemtaka akija akuletee chipsi mayai, baadaye
unataka akutoe ?out?, bila kujali kwamba wakati huo mpenzi wako ana
fedha au hana. Katika mazingira hayo unadhani mpenzi wako atashindwa
kukuchoka?
Akikuacha kwa sababu hiyo utamlaumu nani? Fanya mabadiliko tafadhali.
Kimsingi ukiwa na mpenzi mwenye tabia ya kutaka kukuomba pesa kila
wakati tena katika matumizi mengine ambayo sio ya msingi, vipengele
vifuatavyo vinafaa sana kwako...
MWELEZE UKWELI
Kama huna pesa wakati mpenzi wako anakuomba, mueleze wazi kuwa huna na
kamwe usijaribu kutoa ahadi ambazo huenda ukashindwa kuzitimiza. Usiwe
mtu wa kutoa ahadi za uongo, mara nitakununulia hiki na kile. Mwanaume
hatakiwi afahamike siku ana pesa au hana. Maana kuna wenzangu ambao siku
za mishahara wanabadilisha hadi kutembea! Mwanamke akijua hilo naye
ataongeza ?mizinga? ili afaidi.
Ishi kawaida, kuwa mkweli kwake siku zote, utakapokuwa mkweli kwake
atakuheshimu kwa uwazi wako. Siku zote zilingane, uwe una fedha au huna
asijue, hilo litakusaidia kwa kiwango kikubwa sana katika maisha yako ya
kimapenzi.
JENGA MAZINGIRA YA YEYE KUKUSAIDIA
Jambo la muhimu ambalo wanaume wengi wanalisahau ni kutokuwafundisha
wapenzi wao wajibu wa kutoa! Utakuta kila kitu ananunua yeye, hata nauli
ya daladala analipa, wakati mpenzi wake ana kazi yake. Ifike wakati kwa
makusudi, mwanaume ampe majukumu ya kufanya mpenzi wake, hiyo
itamsaidia mwanamke kujua namna pesa zinavyokuwa hazitoshi na akaweza
kubana matumizi.
BANA MATUMIZI
Kuna wanaume wengine tangu wanatongoza wanakuwa ni wafujaji wakubwa wa
pesa kwa kutoa ofa na zawadi kibao. Hii inaweza kumjengea imani mpenzi
wako kuwa wewe unazo! Wakati akiwa anaamini hivyo, ukweli ulionao moyoni
ni kwamba huna fedha za kutosha.
Unachotakiwa kufanya mapema ni kudhibiti matumizi yako hata kama pesa
zinakuwepo. Ifahamike kuwa kutoa hakusababishi uhitaji, kadiri unavyotoa
ndivyo unavyoongeza mahitaji. Weka maisha yako katikati usijidai tajiri
kumbe ni kapuku tu.
Kwa kumalizia niseme tu kwamba, mapenzi si kukomoana, mapenzi ni
kusaidiana. Jenga tabia ya kumsaidia mwenzako ili siku moja na wewe
ukiwa na tatizo akusaidie. Kitu unachotakiwa kukiepuka ni kuwa tegemezi
hadi unakuwa kero. Kumbuka kumpiga 'mizinga' mpenzi wako kila mara
kunapunguza mapenzi hivyo epukana na tabia hiyo.
NAWAPENDA SANA!!!