Wachezaji hao ni Joe Fils, Fabian Tshiyaz, Fabrice
Baloko wanaotoka klabu ya Vita ya Lubumbashi ya DR Congo na Patrick
Milambo kutoka Nguena FC pia ya Lubumbashi.
Wengine, Mohamed Abdallah wa klabu ya Ferreviario
de Nampula ya Msumbiji, Adeyun Saleh (Miembeni) na Shaaban Kondo
(Mbagala Jack Sports Academy).
Wanasoka wengine waliojitokeza kuwania kusajiliwa
Msimbazi ni Rashid Salum (New Boko, Zanzibar), Ramadhan Kipiala (Buza),
Shaaban Saidi (Boom FC) na Samuel Ngassa, mchezaji wa zamani African
Lyon.
Wanandinga hao walijitokeza siku ya kwanza ya Kibadeni kuvaa mikoba ya Kocha Patrick Liewig kwenye Uwanja wa Kinesi.
Liewig alitimuliwa na uongozi muda mfupi baada ya kumalizika msimu wa Ligi Kuu Bara.
Akiongea kwenye Uwanja wa Kinesi jana, Kibadeni
aliyewahi kucheza klabu hiyo na baadaye kuwa kocha, alisema angependa
kufanya kazi kwa uhuru na bila kuingiliwa kwenye majukumu yake.
Kibadeni amesema, yeye kama kocha anafahamu wajibu
wake katika kufundisha na kwa sababu hiyo, angependa kupata ushirikiano
mzuri kutoka kwa viongozi wake.
“Hii ni mara yangu ya nne kufundisha Simba,
wanachama na wadau wa soka wanajua jinsi gani nilivyokuwa naacha kazi,
muda wote ilitokana na kukosa uhuru, kabla ya kujiunga na Kagera Sugar,”
alisema Kibadeni.
Kibadeni alisema sababu kubwa ya kujiunga na
Kagera ilitokana na hatua ya kocha wa Simba wakati huo, Moses Basena
kutaja msaidizi wake awe pia kutoka nje na hivyo kumleta Richard
Amantre.
“Kuna mambo ambayo kimsingi huwezi kuyakwepa hasa
viongozi wanapoamua kufanya uamuzi fulani. Hili lilitokea wakati
nafundisha Simba miaka ya nyuma,” alisema Kibadeni.
Kuhusu usajili, Kibadeni alisema: “Nimeikuta timu
tayari ina mipango ambayo baadhi imeshatekelezwa. Ninachohitaji ni
kufanya kazi na wachezaji wenye nidhamu nzuri.”