Dar. Siku moja baada ya Simba kumwongezea mkataba Amri Kiemba,
klabu hiyo ya Msimbazi inatarajia kumpiga bei kiungo huyo mwenye kiwango
kilichosimama kwenye mstari kwa timu ya Wydad Ac Casablanca ya Morocco.
Mpango wa kumuuza Kiemba umekuja baada ya
mashushushu wa timu hiyo ya Morocco kuridhishwa na kiwango alichoonyesha
wakati akiichezea Taifa Stars dhidi ya Morocco katika mchezo wa kufuzu
Kombe la Dunia mwakani.
Katika mchezo huo, Stars ilifungwa mabao 2-1, huku
Kiemba akifunga bao nzuri la kufutia machozi kwa kiki ya mwendo mrefu
nje ya boksi la hatari.
Zakaria Hanspope, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili
Simba, aliithibitishia Mwananchi jana kuwa, mazungumzo ya awali ya
kuuzwa kwa kiungo huyo aliyewahi kucheza Yanga yako hatua za mwisho
kukamilika.
“Ni kweli, mazungumzo ya awali yameshafanyika kati
ya Simba na uongozi wa Wydad Ac Casablanca, leo tunamalizia
tulipofikia,” alisema Hanspope.
“Niko Morocco kufanya mazungumzo ya mwisho na
uongozi wa Wydad Casablanca, natumaini tutafikia mahala pazuri Mungu
akijalia,” alisema Hanspope.
Mmoja wa vigogo wa Kundi la Friends of Simba ndiyo
aliyeushtua uongozi juu ya mpango huo, ambao nao waliharakisha
kumsainisha mkataba mpya kabla ya kumuuza. Juzi, Simba ilimsainisha
Kiemba mkataba wa miaka miwili wenye thamani ya Sh35 mil.