Hivi karibuni uongozi wa klabu ya Simba ulitangaza
kuwatema wachezaji wao wanane akiwamo Moshi ‘Boban’ kwa madai ya utovu
wa nidhamu.
Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam
jana, Mfadhili Mkuu wa Coastal Union, Nassoro Binslum alisema klabu yake
imekamilisha usajili wa Boban, ambapo sasa ni mchezaji wake halali.
“Boban ni mchezaji halali wa Coastal Union na hii
ni baada ya mimi na yeye kumalizana leo yaani kwa kifupi nimemsajili kwa
mkataba wa mwaka mmoja,” alisema Binslum.
Kuhusu dau alilompa Boban hadi kusaini Union,
Binslum hakutaka kuweka wazi kwa madai kwamba uswahiba baina yao ndiyo
ulifanikisha zoezi hilo siyo fedha.
“Siwezi kutaja kiwango cha fedha nilichompa kwa
sababu urafiki wetu ndiyo uliomleta kwetu ingawa siyo kwamba amekuja
bure kabisa kuna kiasi nimempa,” alisema Binslum.
Alisema kuwa, klabu yake itakuwa tayari kumwongezea mkataba zaidi Boban endapo ataonyesha kiwango cha kuridhisha uwanjani.
“Tumeanza naye kwa mkataba wa mwaka mmoja ili
tuangalie mchango wake kama atatusaidia tutamwongeza mwingine, lakini
tusiporidhika basi tutakuwa tumemalizana,” alisema Binslum.
Wakati huohuo; Uongozi wa Simba umekanusha kutaka kumsajili mshambuliaji wa Yanga, Hamis Kiiza.
Awali kulikuwa na tetesi kuwa Kiiza atajiunga na
timu hiyo yenye maskani yake Msimbazi Kariakoo baada ya kumaliza mkataba
wake na mabingwa wa Tanzania, Yanga.
“Hatujafanya mazungumzo na Kiiza ili kutaka kumsajili acheze Simba msimu ujao,” alisema Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala.
Kwa mujibu wa kigogo huyo wa Simba hivi sasa klabu
yao inajipanga kusajili wachezaji watakaoisaidia timu hiyo kutwaa kombe
la ligi msimu ujao baada ya kuvuliwa ubingwa na Yanga msimu huu.