Chadema: Kuna njama kumvua ubunge Lissu

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) Dk Wilbroad Slaa amesema kuwa CCM inafanya njama za kumuondoa bungeni, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lisu, kwa  kukata rufaa  ya kesi ya uchaguzi wa mwaka 2010,ambayo mbunge huyo alishinda, kinyume cha sheria. 
 Akizungumza na waandishi wa habari jana katika makao makuu ya ofisi za chama hicho Kinondoni, Dk Slaa alisema  Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana anawatumia mawakili binafsi kukata rufaa dhidi ya Lisu, licha ya walalamikaji wakuu wa kesi hiyo kutofahamu lolote kuhusu rufaa hiyo.
Dk Slaa alisema baada ya hotuba ya Lissu, ndipo Kinana alipoanza mchakato wa kuzungumza na Wakili wa Kujitegemea, Godfrey Wasonga wa kampuni ya uwakili ya Wassonga, Dodoma na kumtaka afungue rufaa dhidi ya Lissu. Dk Slaa alionyesha nakala ya barua ya wakili wa Wasonga kwa Kinana iliyohusu madai ya malipo ya awali ya shauri la rufaa ya kesi ya uchaguzi Jimbo la Singida Mashariki, yenye kumbukumbu namba: KM/CCM/01/2013.
Hata hivyo, uchunguzi wa Chadema umebaini kuwa walalamikaji wakuu wa kesi ya Lissu, ambao ni Shabani Itambu Selema na Paschal Masele hawajui lolote wala hawahusiki na rufaa hiyo.
Dk Slaa alifafanua kuwa Shabani Itambu amekula kiapo mahakamani Dodoma kwamba yeye na mwenzake ambaye bado ni Katibu Kata wa CCM, hawakuambiwa chochote juu ya rufaa hiyo.
Pia Dk Slaa alidai kuna njama zinazofanywa na kigogo wa CCM za kuwahonga kiasi kikubwa cha fedha majaji ili Lissu ashindwe katika kesi hiyo ya rufaa.
Shabani Itambu, mlalamikaji wa kesi hiyo ya Lissu aliyekuwepo katika mkutano huo, alikiri kuwa hakuwahi kufungua kesi ya rufaa dhidi ya Lissu. Itambu anasema alihama CCM na kuhamia Chadema tangu Januari 7, mwaka huu, baada ya kuona sheria zinapindishwa katika chama hicho.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi alipotakiwa kuzungumzia hilo alijibu kuwa hataki kujihusisha na masuala ya mahakama. “Sitaki umbea… naogopa masuala ya mahakama, ingawa sijazisikia tetesi hizo na mimi nipo hapahapa Dar es Salaam,” alisema Lukuvi.
Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema Chama Cha Mapinduzi hakiwezi kufanya mchezo mchafu na wa kitoto kama huo.
“Ninajua chama changu, kina nguvu bara na visiwani na hakina hofu ya mtu yeyote tena wa chama chochote kile,” alisema Vuai.
Kiongozi huyu wa CCM, alisema chama chake kinaamini katika msingi wa demokrasia na haki hivyo hakuna ushahidi wa madai ya Chadema.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Hv kila mshindi wa chadema anawekewa vipingamizi ktk ushindi wake? Jamani hiyo ndo demokrasia,na hao ccm eti mna nguvu bara na visiwani na mnajiamini,so kama mnajiamini mbona embarassment haziishi kwa chadema? What r u guys afraid of,tell us,nonsense,shame on you,God will punish you for your evil actions,stupid

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad