Dodoma. Ikulu imetajwa kuwa ni moja kati ya taasisi zinazonuka rushwa Tanzania kutokana na utendaji wake.
Hayo yamo katika mada iliyowasilishwa na Mbunge wa
Magu, Dk Festus Limbu kwenye semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo,
wajumbe wa Kamati za Bunge za Kudumu za Bajeti, Hesabu za Serikali (PAC)
na Hesabu za Serikali za Mitaa, (LAAC) kuhusu rushwa, iliyofanyika
mjini Dodoma juzi.
Katika semina hiyo iliyoandaliwa na Ofisi ya Bunge
kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Dk
Limbu alisema: “Rushwa imeenea kila mahali, katika sekta na nyanja zote
(horizontal) na kwa ngazi zote, kuanzia Ikulu hadi ofisi ya kitongoji,
balozi, kaya na mtu binafsi.”
Alisema kuwa rushwa hiyo inajidhihirisha kwa namna
mbalimbali ikiwamo mipango mibovu ya Serikali, mashirika ya umma,
mikataba mibovu, taratibu mbovu za ununuzi, ujangili, uhalifu, upendeleo
na hongo.
Huku akisikilizwa kwa makini na wabunge, Dk Limbu
alisema kwa mujibu wa Taasisi ya 2012 Corruption Perception Index
iliyopima nchi 176 kwa rushwa, Tanzania inashika nafasi ya 102 ikiwa na
alama asilimia 35, huku Rwanda ikitajwa kuwa na rushwa ndogo ya asilimia
53 duniani.
Naye Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Dodoma,
Sosthenes Kibwengo akiwasilisha mada yake, aliitupia lawama Ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuwa ndiyo inayochelewesha kesi za rushwa
wahusika wanaponaswa.
Alisema Takukuru hukamilisha upelelezi wa kesi
kubwa tano kila mwaka, lakini hucheleweshwa na Ofisi ya DPP kutoa uamuzi
wake kuwafikisha wahusika hao mahakamani, huku akiwaasa maofisa wa
Serikali kutoingilia kazi za taasisi yake.
Akichangia mada hizo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Utawala Bora, George Mkuchika alisema bado Takukuru haina meno
katika utendaji wake na kwamba mfumo wa utawala uliopo , hauipi nguvu.
“Nimezunguka nchi mbalimbali duniani, hadi China
huko kote taasisi zao ziko huru, zinamkamata mtu, zinamfungulia mashtaka
na kumfikisha mahakamani bila kupitia kwa DPP, lakini mfumo wetu hauipi
uhuru Takukuru,” alisema akiongeza: “Takukuru inamkamata mtu kwa
rushwa, inamfungulia mashtaka na baada ya hapo yanapelekwa kwa DPP, naye
anaamua mtuhumiwa hana makosa, Takukuru ijitegemee, ipeleke watu moja
kwa moja mahakamani.”
Alisema pia kwamba rushwa imekuwa kitu cha kawaida Tanzania na kwamba watu wanaomba rushwa bila woga.
“Utakuta mtu anashughulikiwa jambo lake na watu
wakimaliza wanamuuliza, sasa unatuacha-achaje?...,” alisema na kuamsha
kicheko kwa wabunge.
Baadhi ya waliochangia ni pamoja na Mbunge wa
Ukonga, Eugene Mwaiposa aliyesema adhabu kwa wapokea na watoa rushwa ni
ndogo wakati Maria Hewa alisema maofisa wa Takukuru hutoa siri za watu
wanaokwenda kutoa taarifa za wanaodai rushwa kwani hata yeye yalimkuta.