Dar es Salaam. Wakati magari 150 ya msafara wa ziara ya Rais Barack
Obama yamewasili nchini, majina ya mawaziri wa Tanzania yatakayoruhusiwa
kumpokea kiongozi huyo kuchujwa na makachero wa FBI.
Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, Moses Malaki
aliliambia gazeti hili jana kuwa matayarisho ya ujio wa Rais huyo ni
kabambe na hayajawahi kutokea katika historia ya Tanzania.
Pia alisema shughuli za kumpokea Rais Obama, anayetarajiwa kutua
Jumatatu saa 8:40 mchana, zitaanza asubuhi kwa maofisa wa Marekani
kushika majukumu yote katika uwanja huo, ikiwemo kuongoza ndege, ukaguzi
wa abiria na mizigo, kwa maana wafanyakazi wa uwanja huo kuwa likizo
kwa siku mbili.
“Wamesema kuwa wao watasimamia kila kitu kuanzia wageni watakaoingia na
kutoka na wataamua nani aingie na kutoka,” alisema Malaki. Imebainika
kuwa hata idadi ya maofisa wa Tanzania wakiwemo viongozi watakaompokea
pia itapangwa na Wamarekani wenyewe.
“Wenyewe wana orodha yao na wanajua nani atakuwepo au hatakiwi kuwepo
katika kundi la wageni watakaompokea Rais Obama,” alisema na kuongeza:
“Nilimuuliza Ofisa Usalama wa Marekani iwapo nitaweza kumwona Rais
Obama, akaniambia: Utamwona ukibahatika kuwepo kwenye orodha.”
Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe naye alikiri kuwa mawaziri
wanaotakiwa kuwepo katika msafara wa kumpokea Rais Obama ni wachache
watakaochaguliwa tu na Wamarekani, baada ya kuyapitia na kuyachunguza
majina hayo kwanza kabla ya kuyakubali.
“Hii sijawahi kuiona, hata sisi wenyewe tunateuliwa na wakishayapitia wataamua, nani aende au asiende,” alisema Chikawe.