Sina budi kumshukuru
sana mwenyenzi Mungu kwa kunitendea mema na zaidi ya yote kunipa uhai na
afya hadi sasa. Wanasema “shukuruni katika yote” na mimi nalazimika
kushukuru kwa yale yote niliyofunuliwa na kuwa sehemu ya ushuhuda wangu
katika maisha niliyobakiza hapa duniani.
Namshukuru Mungu muweza wa yote kwa kunirejesha tena uraiani na kwa
kuniunganisha na familia yangu,mke na watoto,wazazi ,ndugu,majirani na
marafiki,viongozi wenzangu na wanachama wa chama kikubwa CHADEMA na
zaidi ya yote watanzania walio wazalendo wanaoipenda na kuipigania nchi
yao.
Ninapojikuta huru nje ya milango ya mninga uliowekewa makufuli
makubwa,madirisha yenye nondo,ukuta uliowekewa waya wenye miiba mikali
na ulinzi wa maaskari wanaonichunga saa 24,inanikumbusha wimbo mmoja wa
mchakamchaka uliokuwa ukiimbwa gerezani kila siku saa 11:00 alfajiri
tunapoamshwa uliokuwa na maneno;
“Kama raia!kama raia!kama raia!kama raia!
Iko siku moja nitarudi kwetu kwa baba na mama kama raia!
Iko siku moja nitarudi kwetu kwa ndugu na rafiki kama raia!
Kama raia…….”
Ni kweli kabisa na wala si hadithi kuwa ‘jela ni MBAYA, jela ni MATESO!’
Lakini zaidi ya hilo, kwangu mimi nimeyaona pia maisha ya gerezani ni
mahala pa mafunzo ya kuijua jamii, kuyajua maisha, kuyaelewa mambo,
kuifahamu nchi n.k.
Nimekubaliana mia kwa mia na maneno ya mwenyekiti wetu wa CHADEMA-Taifa
Freeman Mbowe(MB) aliponitembelea gerezani Segerea na kuniambia;
“hupaswi kulia na kujuta sana;now you are going to be a PRISON GRADUATE,
uhitimu ambao kila mwanasiasa na mpigania haki mahiri duniani
ameupitia.” Kipindi cha siku 92 nilichokaa ndani nikianzia polisi kituo
cha kati, gereza la Keko na kisha kumalizia Segerea kimenipa uzoefu na
ufahamu usio wa kawaida.
Ipo tofauti kubwa baina ya idara za polisi na magereza,jambo ambalo
lilikuwa nje ya ufahamu wangu kabla.Nina uhakika magereza wakipewa kazi
ya kuwasaka walipua mabomu ,watesaji,wapiga risasi mapadri watawakamata.
Nilipata bahati ya kuitwa na kufanya mazungumzo na wakuu wa magereza ya
Keko na Segerea .
Lakini pia, nilitembelewa na viongozi wakuu wengi wa jeshi la magereza
nchini akiwemo kamishena mkuu Minja.Wakuu hawa wana weledi mkubwa wa
kumpa mtu somo la ‘ushauri nasaha’(counselling). Wanakufutia fikra zote
za uraiani (nyumbani,mitaani na ofisini) na kukurejesha mahala pa maisha
yako mapya ya gerezani na kukujuza taratibu na kanuni unazopaswa
kuzifuata na kuzitii.
Madaktari na manesi waliweza kuangalia kwa karibu sana afya yangu kiasi
cha kulidhibiti kwa kiasi kikubwa tatizo langu la sukari ambalo limekuwa
likinisumbua kwa miaka 14 sasa.
2: KESI YA UGAIDI.
Ni kesi ambayo imenifikisha hatua au ngazi nyingine ya maisha yangu kama
mwanasiasa.Naamini wahusika walipoamua kuifungua bila shaka mwelekeo
ulikuwa uleule ambao niliusoma nikiwa chuo kikuu na ninaousoma katika
maandiko mbalimbali kuhusu historia za wanaharakati na wapigania
haki,uhuru na ukombozi waliopita na tulio nao au tunaowasikia hivi sasa
duniani;wakina Nelson Mandela, Martin Luther King Jr n.k. Wakiwa katika
harakati za kuitafuta haki walifunguliwa kesi na wengine kufungwa jela
kwa tuhuma za ugaidi,uhaini na kula njama.
Nilikubaliana na dhana ya kimtazamo iliyopo au waliyonayo viongozi
/watawala wote wadhalimu duniani kuwa watu wote wanaojitokeza kupambana
au kukabiliana na mfumo kandamizi bila woga, watu wote hao kwao ni
magaidi,mahaini,wala njama au wasaliti.
Ni kipindi kifupi kilikuwa kimepita tangu timu teule maalumu ilipokuwa
imemaliza kikao cha kujitathmini kama CHADEMA (RETREAT) kuona tumetoka
wapi, tuko wapi na kwa mfumo upi na mazingira yapi ilikuyafikia malengo
tuliyonayo.Nakumbuka miongoni mwa mambo niliyoyasema ni pamoja na nini
tutarajie baada ya CHADEMA kuonekana na kuthibitika kwa watawala kwamba
imekua,imeimarika na imejipanga vyema kiasi cha kuwatia hofu watawala
(CCM) kwamba karibu wanaondolewa madarakani.
Niliwaambia washiriki wenzangu kwamba wajiandae kukamatwa na polisi mara
kwa mara,kutiwa ndani,kufunguliwa kesi nyingi zisizo za
kweli,kubambikiziwa kesi,kuchafuliwa mbele ya jamii,kutishiwa maisha,
kupigwa, kuuwawa, kudhohofishwa kiuchumi n.k.
Nikasema, pindi tukiona hayo yamekamata kasi kila pembe ya nchi tujue
CCM tumeanza kuwashika pabaya na ushindi utakuwa umekaribia.
Nilishauri tujipange kisawasawa kimbinu na kimkakati kukabiliana na
mambo hayo kwa sababu ni lazima yatokee.Namshukuru Mungu yameanzia
kwangu na kama nilivyomwambia mwenyekiti Mbowe aliponitembelea gerezani
nilimwambia nimekipokea kikombe hiki na yaliyonitokea tusiyashangae bali
yawe changamoto na gia ya kutusukuma kwenda mbele kwa kasi kubwa
zaidi.Ni kukanyaga mafuta zaidi mpaka kieleweke na hiyo ndiyo itakuwa
faraja yangu mimi na wengine watakaofungwa magerezani.
Tuhuma za ugaidi nilizobambikiziwa zilinirejesha nyuma mwaka 2002
nilipokuwa bungeni kama mbunge wa jimbo la Bukoba mjini (CUF)
nikiiongoza kambi rasmi ya upinzani iliyokuwa ikijumuisha wabunge wote
wa vyama vya upinzani TLP,NCCR-Mageuzi,CHADEMA,UDP na CUF.Muswada wa
sheria hiyo ya ugaidi ukiwa ndio umeletwa bungeni kujadiliwa,niliongoza
kambi yangu ambayo miongoni mwao walikuwamo Mh. Mbowe wakati huo akiwa
waziri wangu kivuli wa biashara na viwanda na Dr. Willibroad Slaa akiwa
waziri kivuli wa katiba na sheria kuupinga na kuukataa muswada huo kwa
nguvu zote.
Sababu mojawapo ya kuupinga ikiwa ni mahudhui na malengo ya muswada huo
kutoeleweka na kuwa wazi na kwamba ulilenga zaidi matakwa ya kijasusi ya
nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani na kwa hapa kwetu tulitamka
bayana kwamba serikali ya CCM ililenga kuitumia sheria hiyo kuvidhibiti
vyama vya upinzani. Hilo ndilo limetokea sasa na likaanzia kwangu.
Ukiachia mbali msongo mkali wa mawazo niliokuwa nao nikiwa gerezani juu
ya ugonjwa wa baba yangu mzazi mzee Elias Lwakatare aliyeletwa Dar Es
Salaam kwa ajili ya matibabu,athari za mke wangu kuathirika kimasomo
huko chuo kikuu Mzumbe aliko,mshtuko kwa watoto wangu shuleni na ugumu
wa karo zao za shule,kuwaweka roho juu kaka,dada na ndugu
zangu,kuvurugika kwa kazi za chama ofisini kwangu na mkoani kwangu
Kagera n.k,binafsi nililiona tukio hilo kama nafasi nyingine kwa chama
chetu kujitambua na kujipima udhaifu tulionao,nguvu tulizonazo na fursa
tulizonazo wakati tunapoelekea kuikamata dola.Niliisoma makala mojawapo
ya Mwanakijiji katika toleo mojawapo la Tanzania Daima,niliipenda sana
na niliguswa. Makala hiyo ilikuwa ikituasa CHADEMA kujitathmini. Ukweli
wenyewe ni kama makala hiyo ya Mwanakijiji sisi kama CHADEMA ilituvua
nguo na kutuacha uchi.
Kwanza tuhuma ya ugaidi niliiona kama kombora la mwisho la serikali ya
CCM kukamilisha mkakati wao wa kuichimbia CHADEMA kaburi ambayo siku
zote huwa ni ya pembe nne na katika kuichimba na kuifukia kawaida koleo
lenye umbo la ‘U’ mbele na mpini wake hutumika.
“U” ya kwanza yenye kutubamkikizia tuhuma za
ufamilia,Ukabila,Uchagga,Ukask azini alikuwa amebebeshwa mwenyekiti
Mbowe zikashindwa. “U” ya pili yenye kuzoa tuhuma za
Udini,Ukatoliki,Upadri alibebeshwa katibu mkuu Dr.Slaa nazo zikakwama
CHADEMA ikapenya. “U” ya tatu yenye kulenga
Uchonganishi,Umbea,Ufitinishaj i na Usongombingo, CCM wakalenga
kumbebesha Naibu katibu mkuu kijana Zitto Kabwe lakini naye akawashtukia
akawaumbua na kuwabwaga. Zitto ameendelea kuhimiza mshikamano mkubwa
ndani ya chama na kuwaacha wapambe nuksi hoi. “U” ya mwisho yenye kubeba
Ugaidi,Uuaji,Utekaji iliyolenga kukifuta kabisa chama vitabuni na
kuwasweka viongozi gerezani, kabambikiziwa Wilfred Lwakatare Mkurugenzi
wa Ulinzi na Usalama CHADEMA.Mungu mkubwa nayo hiyo mahakama kuu yenye
baadhi ya majaji weledi wa sheria na wasiokubali mizengwe wameifutilia
mbali.Hakika CHADEMA haizuiliki na kwa hakika lililobaki ni kulitumia
koleo hilohilo na “U” hizo kuwafukia CCM humohumo kwenye kaburi
walilojichimbia wenyewe. ‘Mchimba kaburi huingia yeye mwenyewe.’
Nashukuru CHADEMA hivi sasa imejipanga kama taasisi makini inayoongozwa
na kusimamiwa kitaasisi na wala si kwa utashi wa mtu binafsi au kundi
fulani la watu bali vikao vya kikatiba. Mshikamano wa pamoja na fikra
zinazotuelekeza kulenga paala pamoja tulikodhamiria, hivi sasa ndiyo
silaha kubwa na nusuru yetu kichama. Kama CHADEMA inavyoamini ;
“TUNAANZA NA MUNGU, TUNAENDELEA NA MUNGU NA TUNAMALIZA NA MUNGU.”
I AM REALLY PROUD OF BEING IN CHADEMA FAMILY!!!
3: HALI NA TASWIRA YA POLISI MAGEREZA NA VYOMBO VYA KUSIMAMIA HAKI NA USALAMA.
Wakati nikihojiwa na jopo la maofisa wa makao makuu ya polisi la akina
Mhigulu wakati huo akiwa Kaimu DCI na wenzake akina Obadia,Jonas,Simon
Pasua,Beneth Kipasuka,Nyombi na wengineo baadhi yao niliwapa ujumbe
wamfikishie ‘college mate’ wangu (IGP Said Mwema ) Chuo kikuu cha Dar es
Salaam kuwa naziona jitihada na mbio zao za kuwatafuta hao watu
wanaoitwa magaidi,wateka madaktari na waaandishi,wapiga risasi mapadri
n.k mbio zao haziwezi kufaulu kutokana na namna wanavyoliendesha zoezi.
Niliwaambia ;wakati wao wako ndani ya land rover 109 kilomita arobaini
nyuma yetu sisi tunaokimbizwa na kutuhumiwa kuhusu ugaidi na kupanga
njama za kudhuru watu, wahusika halisi wa mambo hayo wako na Range Rover
kilomita arobaini mbele yetu. Je,ni mwaka gani watawafikia na kuwaweka
mbaroni hao jamaa?Hivi, kikosi cha IGP Mwema ambacho tumeelezwa ni
maalum na kina makachero waliobobea kushindwa kurejesha mrejesho wa
maana hadi sasa kwa angalau hata tukio moja, hivi watanzania hatushtuki
tu? JK haushtuki ? Anyway,tuendelee kuwapa masurufu na kuwatengea
mafungu tutaona! Sijui kama walinielewa au kumfikishia IGP Mwema huo
ujumbe wangu.Na kwa kuwa asiyetaka kujua maana haambiwi maana basi
tuendelee mambo ni kanyaga twende!
Wakili wangu Kichehere niliyekuwa naye katika mahojiano wakati
nikihojiwa kituo cha kati alijaribu kuwapa changamoto japo chache za
kupanua akili zao kuhusu huo unaoitwa ugaidi dhidi yangu na ‘ka-cd’ kao
walikokachota kwenye mtandao wa “You Tube” (kama walivyotueleza) na
kutuonyesha pale kwenye mahojiano. Hawakutaka kumsikiliza wala kumuelewa
juu ya kasoro zilizojidhihirisha moja kwa moja . Hata pale
alipowashauri kuwaita na kuwahoji baadhi ya watu muhimu walioonekana
kuhitajika ili kuondoa walakini usio na sababu tangu mwanzo wa zoezi,
hawakutaka kuuchukua ushauri huo. Wakaona waendelee kukimbia na hako ‘ka
109’ kao. Mimi naamini upo wakati ambapo mshtukiwa wa tukio
linalochunguzwa aliye mzalendo na nchi yake anaweza kuwa msaada wa
kuinusuru nchi yake anayoipenda endapo anapewa nafasi ya kutoa
ushirikiano kwa njia za kuheshimiana kiutu .
Anyway,sijui mwisho wa mambo yote haya maana bado tuko safarini na bado
nina kesi moja ya kujibu ya njama ya kumdhuru Denis Msacky kwa sumu (kwa
mujibu wa maamuzi ya mahakama kuu ya jaji Kaduri).Sitaki kuingilia
mwenendo wa kesi hiyo na nikajiibulia mengine.Lakini kaka yangu IGP
Mwema endelea kutangaza bingo la mamilioni labda utafaulu,Inshallah!!
Ukiacha kesi yangu hiyo ya kutuhumiwa ugaidi, lakini kukaa kwangu pale
polisi central (kituo cha kati),gerezani,keko na Segerea
kumenithibitishia vituko na mambo chungu nzima niliyokuwa nikiyasikia
nikiwa uraiani na kufikiria ni ya uongo. Vitendo vya watu kubambikiwa
kesi viko njenje na wenyewe kwa lugha zao wanaita; “kumpa mtu kichwa!
kumpiga mtu armed robbery! kumpeleka mtu mapumziko!n.k” Nafikiri watu
wanaofanya vitendo hivi wanahitaji kufanyiwa ‘concelling…’ ( kupewa
ushauri nasaha) kwani sio vitendo vya kiutu.
Hivi huu ni utamaduni gani na taifa tunalipeleka wapi? Hivi kweli
inaingia akilini wakati mchezo kama huo ukiendelea na watu kibao
kubambikiziwa kesi kwa ‘kupewa vichwa’ wakati huohuo mh.JK yuko ‘busy’
kuwatunuku watu nishani za utumishi uliotukuka? ‘This is a typical
shame!!’ Sijui kama usalama wa Taifa wapo. Hivi wanafanya kazi gani kama
hawamsaidii mheshimiwa Rais kumjuza kinachoendelea? Au ni ugonjwa
uleule mchanganyiko wa ‘sisiemhosis’. Naanza kukubaliana na usemi wa mtu
mmoja niliyeongea naye gerezani Segerea aliyesema vyombo vya kulinda
usalama huenda ni vya kulinda usalama wa viongozi walaji,wahujumi wa
nchi,mafisadi na mfumo aliouita ; “chukua chako mapema.”
Na ni vyombo vyenye weledi mkubwa wa kuchora michoro ya
fitina,uongo,wizi,hujuma,kusam baratisha vyama vya upinzani kuiba kura
kutisha watu kutengeneza kesi bandia,kuandaa mashahidi feki n.k. Matokeo
yake watu ambao leo hii wamejaa na kurundikwa magerezani na mahabusu za
polisi,asilimia kubwa wanakuwa hawana hatia wahalifu wakubwa wako nje
wakiendelea kula nchi! Asilimia kubwa ya kesi zinazopelekwa mahakamani
ni feki na ni za kuwachosha mahakimu na majaji bila sababu kwani kesi
hizo huishia kufutwa.
Mrundikano mkubwa magerezani wa wafungwa na mahabusu unasababisha hata
huduma ziwe mbovu. Wapo wafungwa hawana sare za gereza wanavaa kitu
kinachoitwa ‘nusu mlingoti’, kauka nikuvae, sare zilizochanika kiasi cha
kutia aibu.Na kwa kuwa hata sera za uendeshaji magereza nyingi ni
zilezile za ‘vichwa vya ki-CCM’ (chama dhaifu,wabunge dhaifu na serikali
dhaifu) hakuna akili inayoweza kubuni namna ya kuitumia kiufanisi nguvu
kazi kubwa iliyojaa magerezani. Ndani ya gereza kuna kila aina ya fani
na vipaji lakini vimelala tu. Kama vile CCM, hawazai na hawana watoto
nyumbani, huwezi kuamini watoto lukuki waliorundikwa Segerea bila
utaratibu mzuri wa kimalezi na kimakuzi hata kama baadhi yao ni wakorofi
na wahalifu. Tutake, tusitake hawa ni taifa la leo na la kesho.Hawa ni
nguvu kazi yetu ya nchi ,hawa wanahitaji kukunjwa wangali wabichi.
Watoto hawa ambao wengine ni wa umri wa miaka kumi wenye kesi za kuiba
embe tano,kuiba simu, kudokoa pochi zenye elfu 30,000/=n.k,wamo gerezani
wakinyweshwa uji asubuhi,ugali wa dona na mchuzi mwingi wenye maharage
thelathini kwenye bakuli na muda unaobaki kuutumia kufundishana
ngumi,kupiga ‘vice’, na mengine mengi. Kuna kitu kipya ambacho
kimebuniwa na uongozi wa jiji la Dar es Salaam ‘kuusafisha mji’ kwa
kuwaondoa barabarani na mitaani watu wote mafukara na wasio na uwezo
mkubwa wa kipato. Hawa wote wanakusanywa kwa mamia kila siku na
kurundikwa Segerea kwa shtaka moja tu linaloitwa “kesi ya kubughudhi
abiria.”
Uwe umekamatwa unakojoa kichochoroni, unauza maji ya Uhai
barabarani,machinga wa bidhaa,mpiga debe,unayemsubiri jamaa yako pembeni
mwa barabara au kituo cha mabasi Ubungo, uwe ni mama lishe, ni ‘dada
poa’ n.k,ukishashindwa kuwakatia elfu kumi au elfu tano jamaa hao
wanaoitwa askari wa jiji au walinzi shirikishi, ujue wewe tayari
unakwenda Segerea kwa kesi ileile inayoitwa ya ‘kubugudhi abiria’.
Wakati huohuo bidhaa zako zote zinakwenda,masufuria na wali wa akina
mama lishe unapelekwa kunusuru familia za wasafisha jiji hao,simu na
pesa yoyote uliyonayo mfukoni inakwenda;yaani ni kiama! Jamani,
waheshimiwa wabunge na madiwani wa jiji la Dar es Salaam hususani wa
CHADEMA chukueni hatua za haraka.
Mzee kikwete upo hapo? Unakumbuka ahadi zako za hotuba yako ya kwanza
bungeni Dodoma na wakati ulipomaliza ziara yako ya magereza ya Keko na
Segerea mwaka 2007? Achana na hayo yote,sasa njoo gerezani upate picha
‘live’.
Nikiwa kwenye selo yangu,kwa bahati nzuri niliruhusiwa kuletewa magazeti
na kusikiliza redio . Siku moja wakati nasikiliza kipindi cha Bunge,
Naibu waziri wa mambo ya ndani akijibu hoja za wabunge kuhusiana na
hotuba ya bajeti yao iliyokuwa imewasilishwa na bosi wake Dr.Nchimbi,
nikamsikia akizungumzia swala hilo la upekuzi wa wafungwa na mahabusu
kwa utaratibu unaoonekana kumdhalilisha binadamu. Naibu waziri anasema
tatizo hilo lipo lakini kutokana na ufinyu wa bajeti hawawezi kununua
vifaa vya kisasa vya kufanyia upekuzi. Akasema kutokana na hali
hiyo,wataendelea kutumia njia hizohizo za ‘ubunifu’ mpaka hapo serikali
ya CCM itakapokusanya mapato yanayokidhi bajeti inayoweza kuvinunua
vifaa hivyo.
Wakati wa kupitisha mafungu,jamaa wakapitisha pesa ya kununua
chai,vitumbua,maji ya kunywa,ziara za viongozi,ununuzi wa
magari,semina,warsha,mafunzo ,motisha n.k. Nikajiuliza,hayo mambo ndiyo
kipaumbele kweli hata kuliko kuyanunulia magereza mashine mojamoja za
kufanyia upekuzi? Taasisi mbalimbali za haki za binaadamu ni kweli
zinafanya kazi nzuri kwenye mitandao ,uitishaji semina,uandikaji ripoti
nyingi nzuri zinazotumwa kwa wafadhili ili michuzi izidi kutoka n.k.
lakini nasema haitoshi. Tembeleeni magerezani msiishie kwa bwana Jela ,
ombeni kutembelea maeneo yote na kuongea na wafungwa . Kwa njia hiyo
mtaboresha kazi yenu kwa uzuri zaidi.
4: SALAAM TOKA MAHABUSU, POLISI NA GEREZANI.
Mwenyekiti Mbowe alipokuja gerezani Segerea kunitembelea akiwa na
Mkurugenzi wa mambo ya Bunge na Halmashauri Bwana John Mrema alinipa
kazi ya kukijenga chama humo humo ndani gerezani . Nitakua namkosea
adabu nisipo fanya mrejesho wa kazi yake. Na kwa kuwa mengi ya yale
niliyoyafanya na kuelezwa na wadau wangu yanatuhusu sisi wote kama
viongozi wa CHADEMA, wanachama na hata wanachama watarajiwa, sio vibaya
nikiyaweka hadharani. Ya Mbowe kama Mbowe nitamuwasilishia yeye mwenyewe
kwa muda muafaka.
Wafungwa, mahabusu, baadhi ya watumishi wa gerezani, mapolisi na
wengineo wanatoa salamu nyingi sana. Wengi wanaipongeza kazi inayofanywa
na CHADEMA ndani na nje ya bunge. Wanasema karibu wote ni CHADEMA japo
wengi hawana kadi. Ili upokelewe vyema gerezani lazima uwe ‘vidole
viwili’ ukijitia ‘ukada’ utalijua gereza. Wanasema kamwe wabunge wa
CHADEMA msitiwe woga na tambo za wabunge wa CCM ndani ya bunge kwa
kujiona wako wengi wakifikiria huo wingi upo hata nje ya mjengo.
Wanasema katika hilo ‘wamebugi meen!!’. Nje ya Bunge CHADEMA mna
mashabiki na wafuasi nyomi!! Yaonekana kwa hivi sasa Bunge ni uwanja wa
nyumbani anaoutumia CCM kimchezo na ninyi CHADEMA uwanja wenu uko huku
uraiani kwa umma.
Wanasema vitendo vya dada Makinda na mwenzie Job Ndugai wameshavipigia
hesabu. Mwisho wao hauko mbali , ninyi kazi yenu ni kukaza buti bila
kulegeza. Wamenituma niwaambie, maana mjumbe huwa hauwawi!, eti CHADEMA
nje ya Bunge tusiendelee kupoteza muda kuwahubiria watu ufisadi, wizi,
manyanyaso ya vyombo vya dola vya serikali ya CCM, kushindwa uongozi kwa
serikali nzima ya CCM, umaskini mizengwe ya CCM katika kuandikwa kwa
katiba mpya n.k. Wanasema yote hayo wameshayaweka kichwani na wanajionea
wao wenyewe kama waathirika namba moja wanatambua fika kwamba wamo
ndani ya gereza kwa sababu ya mfumo uliosababishwa na kutengenezwa na
CCM.
Wanasema katiba halisi ya watanzania itaandikwa baada ya CHADEMA kuingia
ikulu kwani CCM ni mizengwe mitupu.CCM hawajaanza leo, kumbukeni
yaliyompata Jaji Kisanga na Tume yake walipoambiwa na Mkapa kwamba
wamewasilisha taarifa ya mambo ambayo hakuwatuma. Wanasegerea wanasema
elekezeni nguvu zote kwa kipindi hiki kilichobaki kabla ya chaguzi za
2014 za serikali za mitaa na ule mkuu wa 2015 kuwapanga wapiga kura
kiuchaguzi .
Lipigwe jaramba na kuwekwa mpango mahususi utakaowezesha kila aitwaye
mtanzania mwenye umri wa kupiga kura apate uhalali wa kupiga kura.
Uwekwe mfumo wa kubanana kuhakikisha watu wanajipatia vitambulisho vya
uraia wanatunza shahada zao au vitambulisho na wanakwenda kupiga kura.
Wanaamini kwa hali ilivyo hivi sasa, ni binadamu ‘asiye majaliwa’ au
wale wachache wasiojaa kiganjani waitwao ‘CCM maslahi’ watakaothubutu
kuelekeza kura zao kwenye rangi ya kijani- mchicha, kisamvu!
Wamo baadhi ya wafungwa na mahabusu walionieleza kwamba walikua CCM kufa
mtu na walishiriki kwenye hujuma mbalimbali na hata kuiba kura, lakini
hivi sasa wamekoma kwani wametumika kama karai na kisha kutelekezwa nje
ya jumba walilosaidia kulijenga na ndio maaana wanaozea jela. Baadhi ya
mbinu walizokua wakizitumia kutuibia kura wamenieleza na nimetoka nazo
kibindoni.
Wamenituma niwaeleze, kwa kipindi kilichobaki, ‘chonde! Chonde! acheni
kugombana, kurumbana na kufukuzana. Tumieni kipindi hiki kujenga
mshikamano utakaowezesha kukisuka kikosi cha ‘Real Madrid’ au
‘Manchester United’ ya siasa za Tanzania ili uchaguzi ujao CCM walazwe
chali-mwanguko wa kifo cha mende! Wanasema CCM ni wepesi kama nyama ya
maini, wakibanwa kwenye kumi na nane hawana ujanja wataachia tu , tatu
bila!!!
Wameniambia hivi sasa CHADEMA ni chama kikubwa chenye uwezo wa kubuni
njia mbalimbali mbadala zinazoweza kutumika kuwadhibiti viongozi wowote
au wanachama wanaodiriki kukivuruga chama makusudi au kukihujumu badala
ya kuchukua hatua za kuwafukuza.
Wanampongeza na kumpa heko Mwenyekiti wa chama kwa umahiri na ubunifu
wake uliokifanya chama kikue na kupanuka kwa haraka. Kwa lugha zao
wanasema Mbowe ni jembe na ni kichwa,anafanya kazi nzuri ya kutengeneza
timu kwa lengo la kushinda mechi. Wanamshauri ajitahidi kuona namna ya
kuumudu mchezo ulioko mbele yetu 2014 na 2015. Iangaliwe karata
zitachangwaje? Wanasema ni vyema tukajifunze namna mchezo wa siasa za
Kenya ulivyochezwa dakika za lala salama za uchaguzi wao. Wanatambua na
kupongeza namna CHADEMA ilivyomuunga mkono Kamarade Odinga na muungano
wake wa ACCORD, lakini kwa msingi wa kujifunza mbinu za kuusaka ushindi ,
tuangalie na kujifunza namna Kenyatta alivyoubadili mchezo. Kwanza kwa
kumudu kuunda chama kipya na kukijengea mtandao ndani ya muda mfupi.
Pili alivyoweza kuwavuta na kuwashawishi waliokuwa mahasimu wake walio
muhimu (kama vile Ruto) ambao bila ya kuwa nao asingeweza kufua dafu kwa
Odinga. Tatu , namna Kenyatta alivyocheza mchezo wa kisiasa kwa
kuzingatia na kutumia kanuni isemayo ‘siasa hazina rafiki wala adui wa
kudumu’ bali ni kuangalia nani anawezesha kupenya vikwazo ili kuwezesha
kufika salama ninakokwenda (kwa maana ya kuingia Ikulu). Ukishaingia
ndani ya mjengo mambo mengine ni akili kichwani, utajua unachemsha vipi
kichwa lakini muhimu kuliko yote si tayari umo ndani na unachezea ndani?
Wanamuomba Mbowe azidi kuzamisha akilli na kuupanga mchezo kwa
“formation” ileile ya Kenyatta, lakini kwa kuongezea na mbinu nyingine
zinazozingatia mazingira yanayotunzunguka KICHADEMA.
5: NIMEKUTANA NA SHEIKH PONDA
Milima huwa haikutani lakini binadamu wanakutana. Ndivyo sakata la
ugaidi lilivyonifikisha gereza la Segerea na huko nikajikuta nawekwa
selo moja na ‘mjukuu wangu’ Issa Ponda mtoto kutoka Kigoma. Issa Ponda
ni kiumbe wa mwenyezi Mungu wa aina ya pekee. Kwa nchi za wenzetu
zilizoendelea mtu mithiri ya Ponda si mtu wa kuchukulia mzaa kama
ninaouona ukichezwa hapa kwetu. Ni mtu ambaye fikra zake, ubunifu
alionao kichwani na katika vitendo, hulka zake, nasaha zake, ushawishi
wake, ujengaji hoja zake, uchaji wa Mungu wake, uswalihina wake na
vingine vingi ni watu wachache sana unaoweza kukutana nao wakiwa navyo
vyote kwa mpigo.
Ponda tofauti na namna mfumo unavyomchukulia, ni mtu ambaye angetumika
vyema kwa kusikilizwa sehemu kubwa ya mawazo yake na yakafanyiwa kazi
ipasavyo, nina uhakika mambo mengi tunayoyaona yana mitafaruku ya kidini
yasingelikuwepo.
Tatizo wakubwa wanamuangalia kwa taswira ya upande mmoja ya kumuona
‘mkorofi, mchochezi’. Sijui na ndio maana nauliza, hivi ni mamlaka gani
ya juu na yenye kauli ndani ya nchi hii imewahi kukaa na Ponda kwa
karibu katika misingi ya kuheshimiana kwa dhati na kusikilizana ili
kujua ana mawazo na mitizamo gani kwa masuala mbalimbali
yaliyolalamikiwa na baadhi ya waislamu walio wengi?
Nimeishi naye zaidi ya siku 60 selo moja kwa masaa 24 karibu kila siku
na masaa mengi tukiwa wawili tu, mimi na yeye. Ni mdadisi wa kupenda
kujua, na ukisha mwelewesha ni mwepesi wa kuelewa na kujenga fikra mpya.
Hivyohivyo siyo mchoyo wa kuyabania maarifa aliyonayo na elimu kubwa ya
kidini aliyobahatika kuipata.
Alinielewesha kuwa kwenye dini ya kiislamu mtu anapokuwa amefikia
kiwango cha kuitwa U-Ustadhi kwa lugha ya haraka inayoeleweka na wengi
ni sawa na U-profesa.Hakika Sheikh Ponda ni ‘profesa’.
Nilipata fursa ya kujadiliana naye pia mambo ya msingi yanayolikabili
hivi sasa Taifa letu. Moja wapo ni nguvu nyingi zisizo na sababu
zinazotumiwa na polisi kushughulika na watu kama sisi ambao hata rungu
hatuna. Nguvu kubwa inayotumika ya kumpeleka Ponda au Lwakatare
mahakamani ili kesi itajwe tu na kurudi Segerea kulala ni sawa na
kumlipa daktari wa muhimbili mishahara mizuri ya miezi miwili. Magari
nane na mapikipiki kujazwa mafuta,ving’ora barabarani,askari polisi
zaidi ya hamsini kuvunja shughuli nyinginezo kwa siku nzima, barabara
kufungwa na mengine kuzuiwa wakati wa kupita n.k Mikwara yote hiyo ya
nini?
Mfungwa mmoja aliyesoma kwa kiwango fulani alipoletwa kulala kwenye selo
yetu na kuikuta mada hiyo, alichangia hivi, “kawaida ya mtu yeyote
anayelazimisha aonekane mbele ya wakubwa zake kwamba anafanya kazi ni
lazima atengeneze mazingira yanayomfanya aonekane kweli anafanya kazi”.
Kisha kasema hivi “nyie waheshimiwa ili wale waliowafungulia tuhuma za
ugaidi na uchochezi lazima watoe taswira ya nje kwa umma kuonesha kuwa
ninyi ni watu hatari sana na mkipewa upenyo wowote mnaweza kusababisha
maafa makubwa sana wakati wowote kwa taifa. Kwa ufupi wanataka umma
uwahukumu kinadharia kwamba mnahusika na tuhuma mlizoshtakiwa nazo hata
kama mahakama haijazipitia tuhuma zenyewe kuona zina uzito gani.”
Nilimuelewa vizuri sana na kukubaliana na huyo mfungwa maana vyombo
vyetu hivi vya dola wakati mwingine vinapenda kutumia nguvu nyingi sana
katika jambo dogo sana kwa sababu tu za kuridhishana na makundi fulani
au kulinda nafasi zao za kazi ambazo hawazimudu.
Jambo jingine lililoangukia katika mijadala yetu ni hii migogoro ya
makundi ya kijamii na hata mauaji na maumizano yanayojitokeza mara kwa
mara. Sheikh Ponda alitoa changamoto moja muhimu ambayo naona ina
mashiko sana. Alisema hivi; huko uswazi (mitaani wanakoishi watu wengi
kwa kubanana) ambako nyumba moja wanapanga na kuishi zaidi ya watu
hamsini, mchanganyiko wa waislamu kwa wakristo, mbona hakuna ugomvi?
Mbona akina mama humo ndani waislamu kwa wakristo wanaachiana watoto
kwenda sokoni? Mbona wanaazimana vijiko na masufuria? Mbona wanapeana
mboga bila kuulizana? Ponda akatumbukiza na utani pia kuwa “mbona humu
selo ukileta chakula alichopika mama Frank siulizi na wala wewe chakula
anachoniletea mama Mariam naona unabugia tu bila maswali yoyote?
Na mimi nikamwambia mbona ukiamka saa tisa usiku ukaanza swala zako za
sunna mpaka alfajiri wakati wa ‘Azanna’ na kisha swala zote tano za
‘faradhi’ za siku nzima na lakhai zake mbilimbili humu humu ndani ya
selo havijaingiliana na ibada zangu za ‘Tumwabudu Mungu wetu?’ Selo yetu
ndio msikiti wetu na ndilo kanisa letu. Haya mambo chanzo na chimbuko
lake ni nini? Hayawezi kuwa yanatengenezwa na kundi maalum la watu kwa
malengo maalum?
Swali hili la mwisho likanikumbusha somo moja tulilowahi kufundishwa
kipindi fulani nilipokwenda Ujerumani kwa mafunzo ya ‘Strategic
Planning’. Katika kipengele kimojawapo cha mafunzo hayo nakumbuka kuna
kitu mwalimu alikiita ‘Power Winning and Maintaining Strategy’, kwa
tafsiri nyepesi ‘mkakati wa kuupata utawala na kuulinda’.
Katika mkakati huo nakumbuka alitwambia, kuna wakati watawala fulani
wanapoelemewa na mambo au jambo wakakosa majibu mbele ya watawaliwa
wanaotaka kujua kulikoni ili kuzima mambo hayo aidha ni kutumia nguvu na
fursa zilizopo kumshughulikia kinara mmoja anayeonekana kimbelembele
kuhoji.
Mkisha mziba mdomo kwa njia zozote zinazowezekana walio nyuma yake
wataufyata tu! Njia nyingine ni kuibua au kufanya jambo fulani kubwa
bila kujulikana linaloweza kusaidia kuwahamisha watu kifikra toka jambo
jingine lililopo ambalo ni hatarishi zaidi kiutawala.
Njia nyingine ni ile iliyotumika tangu ukoloni ya ‘watawanye uwatawale’ (Divide and rule policy).
Ukiwapa nafasi au fursa watawaliwa wakakaa, wakapanga wakaelewana na
nyie mpompo tu mkiwaangalia, jua siku watakapozua ajenda ya kushughulika
na wewe, ujue umekwenda. Dawa ni kuwafanya siku zote wasielewane kwa
kuwagonganisha vichwa wenyewe kwa wenyewe tena kwa mambo madogo yasiyo
hitaji gharama kubwa na nguvu nyingi. Tulijadiliana sana na kwa urefu na
Sheikh Ponda juu ya mambo haya lakini hatukupata jibu la mwisho na kwa
bahati mbaya au nzuri Mungu akawa amezisikia dua zake na sala zake za
masaa zaidi ya 18 kila siku akawa amechomolewa Segerea na kuniachia
Sello No. 3. Najua Mungu atatukutanisha tena Inshallah! Ila, isiwe tena
Segerea au Keko ili tuhitimishe mada hiyo.
Siku moja kabla ya kusomewa hukumu yake na Hakimu Nongwa (9/5/2013)
tulijadili sana hukumu yake kwamba inaweza kuwa ya mwelekeo gani na
maamuzi yapi. Panga pangua ilishindikana kueleweka mambo yatakuwaje
kutokana na mazingira yaliyokuwa yakiizunguka kesi yenyewe. Mawakili
wake walikuwa wameifanya kazi yao vyema bila kubakiza punje ya shaka.
Lililokuwa likimpa faraja zaidi na kesi yake ni kusikia kwamba huyo
hakimu ni mama mlokole, ameokoka. Hiyo ilikua ikimpa moyo sana kwamba
atahukumiwa na kupewa haki yake sawa na lile lililozungumzwa na
kuwasilishwa mbele ya hakimu Nongwa.
Nilimuuliza endapo hukumu itamuweka katika mazingira ya kumkata makali
yake ya kazi ya utetezi anayoifanya na wakati huohuo upande wa pili wa
‘system’ ukamtaka aanze kutoa ‘Ushirikiano’ atafanyaje? Sheikh Ponda
aliniambia kuwa haki huwa hainunuliwi wala kuombwa bali hudaiwa. Alisema
atakuwa tayari kutoa ushirikiano kwa yeyote yule anayezungumzia utoaji
na upatakanaji haki.Na akasema mdomo na nafsi vilivyodhamiria
kuzungumzia na kuitafuta haki huwa havifungiki kwani vikifungika hata
hiyo amani haiwezi kuwepo.
Nikiwa ndani ya selo nilimsikia Sheikh Ponda akimwaga mistari yake
redioni baada ya kuhukumiwa. Kwa mara nyingine nikazidi kumuaminia
Sheikh Ponda kwamba ni mmojawapo ya watu wachache tulio nao hivi sasa
nchini wanaoweza kutembea na kuishi ndani ya maneno yao.
Lipo jambo moja muhimu ambalo tulikubaliana na Sheikh Ponda tulijadili
na kulifanyia kazi kwa nia ya kuwanusuru watu wanaosota jela bila sababu
endapo tungeliachiwa na kuwa huru uraiani. Namtafuta kwenye simu hayuko
‘reachable’. Nikishampata tukashauriana na likaonekana linatekelezeka,
nitalitoa hadharani.
6: USHAURI WANGU MDOGO KWA VIONGOZI WETU WA DINI.
Mimi ni mtu mdogo sana na muumini wa kawaida ndani ya dhehebu la KKKT.
Lakini natambua kanisa ni waumini na wajibu mkubwa wa kila muumini ni
kuhakikisha anatimiza wajibu wake kama kanisa la Mungu linavyoelekezwa
kupitia maandiko matakatifu ya Biblia. Wajibu mmojawapo sisi kama
waumini ni kuonyana ( Ebr. 10:24 – 25).
Nawaombeni viongozi wetu wa dini zote wakristo kwa waislamu mtimize
wajibu wenu mliokabidhiwa na Mungu, Imeandikwa kwa dini zote kwamba kila
mmoja bila kujali wadhifa wake atahukumiwa sawa na matendo yake.
Nawaomba simamieni na kuuzungumza ukweli(hata kama ni mchungu) mbele ya
watawala na hata watawala watarajiwa.Ninyi mmepewa mamlaka na Mungu ya
kuonya, kukemea, kuelekeza na kubariki na ndio maana watawala wote
wanawaogopa na kuwaheshimu. Wengine huenda ninyi bila ya kuwatambua
hutafuta njia za kujikomba kwenu ili wakipate wanachokitafuta.Yasemeni
wazi na kuyahoji hata yale machache yanayoonekana au kusikika pasipo
kificho.
Muulizeni Mheshimiwa Rais huyo waziri wake anayezungumzwa kila siku
kwamba mchana kweupe alisema anao maadui zake wawili ambao ni waandishi
wa habari na angewashughulikia, Rais analisemaje hilo? Maadam ni ninyi,
nina uhakika Mheshimiwa Rais atajibu na atachukua hatua stahiki.
Binafsi nawaombeni kwa heshima na taadhima muache kuwa vuguvugu (si moto
si baridi-Ufunuo wa Yohana 3:15-16) Baadhi yenu acheni kuogopa vivuli
vyenu kwa maana ya kuhofia kunyimwa upendeleo au misaada ya serikali
(i.e misamaha ya kodi) na baadhi kuutumia mwanya huo vibaya. Kama
maandiko yanavyosema JIKANENI WENYEWE.
Lazima mtambue hawa jamaa wakati mwingine huenda wanaitumia fursa hiyo
kama chambo cha kuwanasia pindi wanapokua wana taarifa zenu zote za
fursa ya misamaha iliyotumika vibaya. “Mnapaswa kushuhudiwa mema na watu
walio nje…” (1 Tim 3:2-9)
Binafsi nawaomba msiwalee wala kuwabeba wale wote wenye dhamira chafu na
nia mbaya ya kutaka kuyatumia madhehebu yenu kukidhi matakwa binafsi
kwani wanachafua taswira zenu nzuri za madhehebu yenu mbele ya waumini
wenu na umma kwa ujumla.
Lakini zaidi ya yote ni imani yangu mimi binafsi kwamba madhehebu yenu
ni makubwa na yana mtandao mkubwa na wenye nguvu ndani na hata nje ya
nchi.Kama inawezekana tumieni mtandao wenu kuisaidia serikali ambayo
vyombo vyake vinaelekea kushindwa kuwabaini wahalifu wachache
wanaoelekea kuchafua na kuivuruga amani tuliyoizoea ndani ya nchi yetu.
Kwa bahati nzuri nimesoma na kusikia kwenye vyombo vya habari kwamba IGP
Mwema amezishauri taasisi za kidini kuanzisha ‘ulinzi shirikishi ndani
ya misikiti na makanisa’. Kama mambo serikali ya CCM imeyafikisha hapo,
tumieni fursa hiyo kuziomba taasisi makini mnazozifikia nje na ndani ya
nchi.
7: MTIZAMO WANGU WA MBELE BAADA YA SAKATA LA UGAIDI.
Mimi kama mimi na wakati huohuo Mkurugenzi wa ulinzi na Usalama wa
CHADEMA, kanuni yangu ya maisha ya kila siku huwa ni kutoangalia yale
yaliyokwisha kuniumiza bali ni kuangalia yanayoweza kuniumiza kuanzia
leo na kwenda mbele.
Ushauri wangu wa namna gani twende katika kukilinda chama kwa ujumla
wake nitawasilisha mbele ya mamlaka na vyombo husika vya Chama.Lakini
rahi kwa wanachama wa CHADEMA na wapenda mabadiliko ya kweli wote
nchini, ni kulichukua jukumu la kuzilinda harakati hizi zinazoendelea
kama jukumu letu wote na kila mmoja kujiona anahusika na anaguswa.
Chukua hatua kuyadhibiti yale unayoweza palepale ulipo na yanayokushinda
toa taarifa au tafuta msaada kwa mtandao wa chama chetu ambao hivi sasa
unaendelea kujikita maeneo yote nchini.Asiye na Uongozi wowote ndani ya
chama wala kadi lakini anajisikia kwenye nafsi kuipenda na kutaka
kuitumikia CHADEMA, naomba achukue cheo cha u-volunteer na aingie kazini
kuanzia dakika hii na sisi tutaitambua na kuienzi kazi yake.
Kwa viongozi wangu wakuu na wale wote waliopewa dhamana ya kukisimamia
na kukiongoza chama katika ngazi na nyadhifa zozote, Sioni njia ya
kutuvusha na kutufikisha haraka tunakokwenda zaidi ya kuziendesha kazi
zetu kwa falsafa ya USIMAMIZI LAZIMISHI (Lwakatare Theory). Ni kheri ya
fedheha kuliko lawama. Tujitahidi kuyafanyia tafsiri ya kutekelezeka
mambo yote tunayoazimia au kuyapanga kufanyika. Kwa njia hiyo nina
uhakika rasilimali zetu tulizonazo (fedha kidogo watu wengi) zitaweza
kutuvusha na kuyashinda mapambano yaliyo mbele yetu.
Kukaa kwangu mahabusu siku 92 kumenipa fursa ya kuyatafakari mambo mengi
kwa kina yanayonizunguka.Nimeamua NIFUNGUKE. Kufunguka kwangu ni pamoja
na kujitokeza hadharani kwenye mitandao ya kijamii kama hivi sasa
nilivyoamua kufanya jambo ambalo nilikuwa nalikwepa kutokana na watu
wengi kutumia vibaya fursa hii ambayo binadamu ameigundua.
Nilipojiunga CHADEMA, nilimuuliza mwenyekiti angependa niifanyie nini
CHADEMA kama sehemu ya mchango wangu katika harakati za kutafuta
ukombozi zinazoendelea.Aliniambia kama naweza nitumie uzoefu mdogo
niliokuwa nao kuanzia CUF wa kutengeneza mfumo wa ulinzi na usalama wa
chama. Mimi sijawahi kusomea upolisi, ushushushu wala uanajeshi labda
jeshi la kujenga Taifa mwaka 1982 Makutopora JKT Operesheni wajibu kwa
mwaka mmoja. Lakini pia japo kidogo ujumbe wangu wa muda mrefu ndani ya
kamati ya ulinzi na usalama ya CUF-Taifa, nao unaweza kuwa ulinisaidia
kunitoa tongotongo kwa kiasi Fulani.
Nikiwa gerezani Segerea nilimshangaa sana ‘bwana mdogo’ Julius
Mtatiro-Naibu Katibu mkuu wa CUF alipozungumza kwenye vyombo vya habari
kuwa ;”Lwakatare akiwa CUF hatukumfundisha ugaidi.” Sikumuelewa hayo
maneno alikuwa na maana gani na alitumwa na nani. Kwanza sijui kipindi
hicho nikiwa CUF yeye alikuwa wapi na sidhani kama kwa wakati huo
alifikiria hata kujiunga na hiyo CUF.Awaulize CUF ‘Original’ kama wapo,
Lwakatare alikuwa ni nani ndani ya CUF.
Hata siku moja haitatokea nibeze uzoefu na msingi wa kisiasa nilioujenga
ndani ya akili zangu na nafsi yangu kutoka CUF. CUF iliniweka katika
ramani ya kisiasa ninayoitumia kutamba hadi leo hii. CUF ilinijengea
nguzo moja kubwa iliyonipaisha kisiasa na inayoendelea kunisaidia katika
kazi niliyokabidhiwa CHADEMA ya ulinzi wa chama hadi leo ambayo ni
UJASIRI WA KUJITOA KWA NAFSI YANGU NA KWA AKILI ZANGU ZOTE KUIPIGANIA NA
KUITAFUTA HAKI BILA KUCHOKA NA KUTOKUBALI DHULUMA NA UONEVU. ‘HAKI HUWA
HULETEWI KWENYE KISAHANI CHA KIKOMBE CHA CHAI, HAKI HUDAIWA NA
KUTAFUTWA.’
Ukisha kuwa na nguzo hiyo, ni silaha tosha inayoweza kumsaidia mtu
yeyote Yule kuyaongoza au kushiriki ipasavyo katika harakati za
kimapambano. Ndio maana leo hii, wapo wanajeshi, mapolisi, usalama wa
Taifa wengi mno ambao serikali ya CCM imewadhulumu na kuwanyanyasa
isivyo kawaida lakini kwa sababu ya kukosa nguzo hiyo niliyoisema
hawathubutu kujitokeza hadharani. Ganzi la CCM la kuwafanya wawe waoga
au wasijitambue limewakolea kwelikweli, hawathubutu kufurukuta.
Wachache wanaojaribu na kuthubutu kujitokeza wanapenda wafanye hivyo kwa
kutokea mafichoni. Binafsi nawapongeza angalau hata kwa hilo maana
najua ipo siku ambayo haiko mbali, ngoma itakapokolea watajitokeza
hadharani kucheza. Kitendo hiki cha kuvishwa tuhuma za ugaidi na kikosi
cha Mwigulu na CCM wenzake kilitukatisha sana ‘stimu’ ya kazi nyingi
tulizokuwa bado tukizipanga. Kwa wahaya wanasema, “Bampeya
ntakamazile…”kwa maana ya kukatishiwa safari kabla ya kufika mwisho wa
safari. Makamanda tukaze buti, tushirikiane kwa dhati tusonge mbele
mpaka kieleweke, neema inakuja.
Afya yangu nikiwa gerezani imeathirika kidogo na kunilazimisha kufanya
vipimo ambavyo wataalam wamenieleza vinampunguzia mtu maisha yake ya
kuishi. Siliogopi hilo najua tunaye Mungu, hata nikiondoka mimi kesho
makamanda wengine wanaendelea na kazi na kusonga mbele.
Nikiwa gerezani nimezitumia siku zangu 92 kutengeneza andiko la toleo langu la kwanza la kitabu nilichokipa jina;
“USHINDANI NDANI YA MFUMO KANDAMIZI (SAFARI YANGU KISIASA HADI KUTUHUMIWA KUWA GAIDI ASIYE GAIDI).
Nimeona ni wakati muafaka kwa baadhi ya watu wenye nia nzuri na hata
mbaya wasionijua Wilfred Lwakatare ni nani wanijue maana nikiwa gerezani
yuko mwandishi mmoja wa gazeti la TAZAMA aliandika makala yenye mtazamo
wa kubeza akiuliza, “kwani Lwakatare ni nani?” Maneno yaleyale
aliyoyatumia Waziri Steven Wassira kwa mwandishi Absalom Kibanda.
Naamini kazi na uzoefu nilioupitia wa uanafunzi hadi chuo kikuu, uafisa
utawala na utumishi serikalini, ujasiliamali, ukulima, ufugaji,
uenyekiti wa mtaa Omukituli Kibeta, uenyekiti wa CUF na CHADEMA mkoa,
ubunge wa jimbo, ukuu wa upinzani Bungeni,uratibu mkuu wa ushirikiano wa
vyama vya CHADEMA, NCCR-Mageuzi, TLP na CUF, unaibu katibu mkuu wa CUF,
ukurugenzi wa ulinzi na usalama CHADEMA, ukuu wa familia ya mke na
watoto wanne na HATIMAYE kujikuta mahabusu nikituhumiwa kuwa GAIDI ASIYE
GAIDI – sio kazi za mchezo. YATAKA MOYO.
Lakini pia nimeona si vibaya nikaonyesha uzoefu niliopitia kisiasa kwa
wengine ili pale nilipokosea basi wengine wasitumbukie katika makosa
yaleyale niliyoingia. Na kama yapo mazuri ya kujifunza, basi wayachukue
na pengine kuyaboresha zaidi ili yawe chachu ya kuwatengenezea njia
katika kufanikisha malengo yao na hasa ya harakati za kisiasa.Kwa wale
watakaohitaji toleo la kitabu hicho wasisite kuwasiliana nami kwa
kunipigia simu au kutuma ujumbe wa maandishi 0713 237869, 0758 417169,
0786 774697 au barua pepe lwaks62@hotmail.com.
Kwa wale wanaotaka kunisaidia kwa namna moja au nyingine kuhakikisha
toleo hilo linatoka kwa haraka na kwa viwango, nitawashukuru kwa mikono
miwili.
8: USHAURI WANGU WA BURE KWA CCM NA WATANZANIA KWA UJUMLA.
Waswahili husema ukishikwa, shikamana. Maana tunakoelekea sio siri CCM
wameshashikwa pabaya . CCM hawana namna ya kuyakwepa mabadiliko ya
nyakati. Kukunjwa ni kuzuri kuliko kuvunjwa. “If they can’t change,
changes will change them.”
Watanzania ambao bado wamesinzia tokeni usingizini. Acheni kugeuzwa
mazezeta na CCM kiasi cha kushindwa kujitambua utu wenu kama watu na
ubinadamu wenu kama binadamu wanaoishi katika Taifa huru. Waache ushamba
wa kuendelea kufikiria kwamba bila kuilamba miguu CCM hawawezi
kufanikiwa katika shughuli zao. Ukombozi wa kifikra ni mkubwa zaidi
kuliko ukombozi wa kutoka utumwani.
Wajiulize wataendelea kuishi maisha ya kila kitu ‘deal’ na uchakachuaji
mpaka lini? Hawaoni kuwa ni utumwa wa kujitakia wenyewe? Naona hata
baadhi ya hizi kesi zinazofunguliwa ni zenye msukumo wa ‘DEAL’.
Wafanyakazi na watendaji ndani ya serikali na taasisi zake nawashauri
anzeni kubadilika na kujipanga kifikra tayari kutumika chini ya utawala
wa chama chochote. Anzeni kujiunga na chama chenu cha AGIP (Any
Government In Power) ambacho sio lazima kisajiliwe wala kutoa kadi.
9: SHUKRANI.
Kipindi cha kukaa kwangu gerezani kililikua cha mtihani mkubwa kwangu
ambacho kimenipa mafunzo tosha katika maisha. Gerezani sio mahala pa
kumuombea au kuombea mtu kupelekwa . Ni mahala ambapo kwa wengine
panakua chanzo cha familia kugombana, kufarakana, kusambaratika, ndoa
kuvunjika na uadui kujengeka baina ya mtu na mtu, na mengine mengi.
Baadhi nimeyashuhudia mimi mwenyewe kwa macho yangu.
Binafsi nashukuru kwa ukaribu niliopewa na familia, ndugu, jamaa,
marafiki, viongozi wa chama, wanachama na wanajela wenzangu. Ukaribu wao
wa muda wote uliifanya siku iwe fupi.Sio siri ndugu zangu,
unapotembelea ndugu yako aliyeko gerezani furaha unayomuachia mule ndani
haipimiki.
Namshukuru sana mke wangu Angel Mercy kwa kukikabili kipindi chote hicho
kigumu kwa kunipa huduma, kufuatilia afya yangu, kuiangalia na kuitunza
familia iliyopo nyumbani na watoto walioko mashuleni licha ya yeye
mwenyewe kukabiliwa na masomo chuoni,Mzumbe-Mbeya.
Nawashukuru sana ndugu zangu kaka, dada zangu, ndugu, marafiki, majirani
na watoto wetu wote kwa misaada waliyonipa kupitia kwa mke wangu lakini
kubwa kuliko yote kitendo chao cha kuja kuniona gerezani. Nikishukuru
chama, (CHADEMA) kwa kunipigania na kunitolea misaada isiyohesabika.
Kipekee nimshukuru sana Katibu Mkuu Dr. Slaa kwa ufuatiliaji mkubwa
alioufanya.
Pongezi na shukrani nyingi kwa jopo zima la mawakili mahiri. Peter
Kibatala, Tindu Lissu, Mabere Marando, Prof. Abdallah Safari na Nyoronyo
kichehere, ambao najua bado tuko pamoja katika ngwe ya pili ya kesi ya
shitaka moja ambalo bado linanikabili na huenda na mazagazaga mengine
yanayoweza kujitokeza.
Nivishukuru kwa namna ya pekee vyombo vya habari vilivyofuatilia na
vinavyoendelea kufuatilia sakata zima la kesi yangu na kuifahamisha
jamii kujua kinachoendelea. Niwape pole na shukrani nyingi wale wote
waliofika gerezani na kushindwa kuniona kutokana na idadi kuwa kubwa
kuliko idadi ya watu walioruhusiwa kuniona.
Kipekee nimshukuru sana Baba Mchungaji wa usharika wetu wa King’ong’o
Kimara na mke wake. Mr & Mrs Rev Joseph Kyaka walionitembelea na
kunijengea moyo wa imani, matumaini na faraja. Niwashukuru wote
waliokuwa pamoja nami kifikra na kimaombi na ninasema kwa maombi yenu,
yote yamewezekana. Mungu anasikiliza maombi na haachi kujibu.
Nimuombe Mungu azidi kututangulia na kutupa ujasiri wa kukabiliana na adui na kumshinda shetani huku tukidumu katika imani.
IN GOD I TRUST.
IMEANDALIWA NA:
WILFRED MUGANYIZI LWAKATARE
MKURUGENZI WA ULINZI NA USALAMA CHADEMA.