KIUNGO bora wa Afrika aliyecheza mechi zaidi ya 100 Barcelona
tangu mwaka 2007 kabla ya kwenda Manchester City ameona mchezaji mmoja
tu wa Taifa Stars.
Mechi baina ya Taifa Stars na Ivory Coast
imeingiza Sh 502 milioni huku mashabiki 57,203 wakiwa wamelipa tiketi
kuona mechi hiyo.
Yaya Toure, ambaye mwaka 2009 alikuwamo katika
kikosi cha Barcelona kilichoweka rekodi ya kutwaa makombe sita tofauti,
amemtaja Kelvin Yondani kama mtu aliyekuwa akimnyima raha uwanjani na
kwamba anachelewa kwenda Ulaya.
Lakini, Gervinho na Solomon Kalou nao kila mmoja wamewataja wachezaji wao waliowasumbua na wanaodhani wanastahili kucheza Ulaya.
Mastaa hao ambao walikuwa na ulinzi mkali wa
mabaunsa wa Ivory Coast walizungumza na Mwanaspoti kwa kina baada ya
mechi ya kuwania nafasi ya kucheza Kombe la Dunia dhidi ya Taifa Stars
jijini Dar es Salaam huku kila mmoja akitikisa kichwa mwisho wa siku kwa
kutoamini kama kweli wametoka salama tena na pointi tatu mbele ya ya
vijana wa Kim Poulsen.
Yaya alisema; “Yule aliyevaa jezi namba tano
(Kelvin Yondan), ni beki mwenye uwezo mkubwa na nimeambiwa kwamba
anacheza soka Tanzania. Kwa uwezo wake anaweza kupambana na mshambuliaji
wa aina yoyote hapaswi kuendelea kucheza soka Tanzania.”
“Yule beki alinipa tabu sana kila niliposhika
mpira nilifikiri jinsi ya kumpita kwani ana uwezo wa kumkaba
mshambuliaji bila ya kusababisha rafu ya aina yoyote, inakulazimu
kutumia akili sana kumuingia,”alisema Yaya ambaye amecheza mechi 74
kwenye kikosi cha Ivory Coast.
“Alinifanya nibadili mbinu za uchezaji, nikawa
natumia muda mwingi kutoa pasi nyingi kila ninaposhika mpira, labda mimi
ningemshauri atafute timu nje ya Tanzania ili apate uzoefu na ataweza
kuisaidia timu ya Taifa katika mashindano makubwa kama haya,”alisema
mchezaji huyo ambaye aliamua kutumia jezi namba 42 Manchester City baada
ya kukuta Patrick Viera akitumia jezi namba 24.
Gervinho ambaye ni straika wa Arsenal aliyeichezea
nchi yake mechi 45 akifunga mabao 13 alisema: “Kama tusingekuwa makini
na kutumia uzoefu wetu wote Tanzania wangetufunga kwa sababu baada ya
yule mchezaji aliyevaa jezi namba 10 (Thomas Ulimwengu) kufunga bao la
pili tulichanganyikiwa na kuamini kwamba tusipotumia uzoefu na juhudi
binafsi hatuwezi kushinda mechi,”alisema.
“Binafsi nilifarijika sana kucheza na timu yenye
wachezaji wenye vipaji vikubwa vya soka, cha msingi wachezaji wajitahidi
kutafuta timu nje ya Tanzania hasa katika nchi zilizopiga hatua katika
soka, nimesikia mchezaji namba 11 na 10 wanacheza TP Mazembe ni mwanzo
mzuri sana lakini wasiishie hapo, pia wengine waige mfano wao na
kutafuta timu nje, ingawa kupata timu si kazi rahisi lakini juhudi za
mchezaji binafsi zinapaswa kuonekana anapopata timu ya kuchezea.”
Straika aliyepigwa chini na Chelsea na kutimkia
Lille ya Ufaransa Julai mwaka jana, Solomon Kalou alisema; “Mchezaji
aliyevaa jezi 10 (Mbwana Samata) anajua. Kwanza anaweza kukaa na mpira,
mshambuliaji anayekaa na mpira huwezi kumkaba kwa sababu anajua ni wapi
apite ama ni wapi atoe pasi na ili umzuie ni lazima uwe makini kutazama
atakapopeleka pasi yake vinginevyo anakuwa na madhara makubwa,”alisema
Kalou.
Akitaja namba za wachezaji wa Stars waliokuwa
tishio katika mechi hiyo alisema kwamba ni pamoja na mchezaji anayevaa
jezi namba 2 (Sure Boy),10 (Samata), 11(Ulimwengu) na 20 (Shomari
Kapombe).