Katika jamii yoyote mtu mwenye tabia ya umbea
huchukiwa, hutengwa na hata wakati mwingine hupigwa kwa kuonekana kuwa
ni chanzo cha migogoro na huku viongozi wa dini wakimwona mtu wa aina
hiyo kuwa ni mtenda dhambi.
Watu wanaopenda tabia ya umbea huenda wakawa
wamepata mtetezi. Ripoti iliyotolewa hivi karibuni kuhusu tabia ya watu
kupenda kutumia muda mwingi kusema mambo ya watu wengine, inasema tabia
ya umbea ina manufaa kiafya.
Ripoti hiyo iliyotolewa na watafiti kutoka chuo
kikuu cha Rhode Island cha Marekani, inasema kuwa watu wanaonufaika
zaidi za tabia hiyo ni wale wanaopenda kuongea mambo mabaya wa watu
wengine kuliko wenzao wanaopenda kuzungumza kuhusu mambo mazuri.
Wataalamu hao wamebaini kuwa iwapo mtu atatumia
dakika 20 kuzungumzia mambo mabaya ya watu wengine, anaweza kuimarisha
afya yake kwa kupunguza msongo wa mawazo, woga na mashaka kwa asilimia
96 kwa muda wa masaa manne mfululizo.
Hata hivyo, wamebainisha kuwa mtu akitumia muda
huo huo kuzungumza mambo mazuri ya watu wengine, atapunguza msongo wa
mawazo kwa asilimia 72 ikimaanisha kuwa watu wenye kuzungumza mambo
mabaya ndio wenye kunufaika zaidi.
Watafiti hao, wakifafanua hali hiyo wameelezwa
kuwa mtu anapoongea habari nzuri zinazowahusu watu wengine huuchochea
ubongo kutaka kujiunganisha na mtu anayezungumzwa, wakati yule
anayezungumza habari mbaya huwa kinyume chake.
Mtu anayezungumza habari mbaya anatabia ya
kutokuhifadhi alichokisema, bali huendelea na mambo yake kama kawaida,
wakati anayezungumza habari nzuri hukaa nazo moyoni kwa kipindi cha muda
fulani.
Mtaalamu wa Saikolojia kutoka Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH), Lusajo Kajula anasema binadamu wote huongea kuhusu watu
wengine, lakini umbea ni zaidi ya maongezi.
Lusajo anasema asili ya mwanadamu ni kuzungumza
japokuwa wakati mwingine hujikuta akiishia kutoa mifano halisi ya maisha
ya watu wengine na hivyo kuingia katika mgogoro wakati mtu aliyesemwa
anaposikia.
“Umbea ni kawaida na hauzuiliki, tatizo ni
yaliyomo ndani ya umbea ambayo mara nyingi hutegemea na mawazo mtu
aliyonayo. Kama ana mawazo hasi, ataongea mambo mabaya,” anasema Kajula.
Hata hivyo, Kajula anapingana na dhana iliyopo
miongoni mwa watu kuwa mwanamke ndiyo anayependa zaidi tabia ya
kuzungumza mambo ya watu wengine kuliko mwanaume.
“Kuna tafiti nyingi zinazoonyesha kuwa wanaume ni wambea zaidi
kuliko wanawake, ila wao hawasutani na pia hawawezi kujieleza vizuri
kama wanawake,” anasema Kajula na kuongeza kuwa kwa kawaida tabia ya
kuongea mambo mazuri yanayowahusu watu wengine hukusudia kukuza heshima
ya mtu anaezungumziwa.
Mwanasaikolojia na mwandishi wa kitabu kiitwacho
‘Nguvu ya Umbea’, Maria Konnikova anasema hakuna mtu anaeweza kuukwepa
umbea na kushauri kuwa mtu asihangaike kutaka kuwazuia wambea kusema
wayatakayo.
Anasema wataalamu mbalimbali wa masuala ya
saikolojia wamebaini kuwa umbea ni njia muhimu katika kuleta umoja na
mshikamano katika jamii kwani kwa kufanya hivyo husaidia kueneza taarifa
ambazo wanajamii wasingeweza kuzifahamu. “Pia imebainika kuwa umbea ni
zana nzuri ya kuifundisha jamii mtu gani anafaa kuwa rafiki na yupi
anastahili kuepukwa,” anasema Konnikova.
Mwanasaikolojia Homer Simpson wakati fulani
aliwahi kusema: “Kama hatutakiwi kula nyama kwanini wanyama waliumbwa
kwa nyama? Kama kila mtu anafahamu kuwa umbea ni mbaya kwa nini anasema?
Jibu ni rahisi; katika ubongo wetu kuna sehemu inayopenda umbea.”
Anasema kila mtu ananufaika na mambo mazuri
yanayosemwa juu yake anapoyasikia. “Wapi ungependa kufanya kazi, sehemu
ambayo watu wanakusema vibaya au vizuri?”anahoji Simpson.
Mchungaji wa Kanisa la Free Pentekosti Tanzania
(FPCT) Njia Panda ya Himo, Kilimanjaro, Elisante Ngailo, akizungumzia
utafiti huo anasema watu wanaotumia muda mwingi kuzungumza mambo mabaya
yanayowahusu watu wengine husema tu bila kufiria.
“Watu wa aina hii hawaumizi kichwa kufiri sana,
wao husema mambo walioyasikia au kuyaona, kisha kuendelea na maisha
yao,” anasema Ngailo.
Anaongeza: “Lakini hawa watafiti wanataka
kutuambia kwamba sasa tuwaseme sana watu kusudi tupunguze msongo wa
mawazo? Hili haliwezekani” anasema Ngailo.
Kwa maoni yake si sahihi kwa watu kuwasema watu
wengine vibaya na kwamba tafiti kama hizi hazijengi jamii kwa kuwa tabia
ya umbea inapingwa na makundi mbalimbali ya watu.
Maoni ya watu mbalimbali
Roda Mgimwa mkazi wa Vingunguti anasema matokeo ya
utafiti uliofanywa kuhusu tabia ya umbea anakubaliana nao kwasababu
watu wa aina hiyo hawana hofu ya jambo wanalolizungumza.
“Wakati mwingine unaweza kumsikia mtu anasema
umbea kuhusu mtu fulani ndani ya daladala bila kujua iwapo yule
anayesemwa ana ndugu yake hapo au la. Kwa namna hii watu hawa hawawezi
kusumbuliwa na msongo wa mawazo,” anasema Roda.