Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya
kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam,
Kibanda alisema asingependa kuona jambo hilo linamtokea mwandishi
mwingine wa habari.
Kibanda, ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni
ya New Habari (2006) Ltd, alikuwa akitibiwa huko baada ya kushambuliwa
na kuumizwa vibaya na watu wasiofahamika usiku wa Machi 5, mwaka huu.
Alisema kutokana na hali hiyo, waandishi wanapaswa kuwa na mshikamano ili kuhakikisha matukio ya aina hiyo hayajirudii.
“Waandishi wana nafasi kubwa ya kuliondoa taifa
katika hali hii. Waendelee kuandika na kuelimisha wananchi ili nao
wasaidie kuzuia ukatili wa aina hii. Hatuwezi kuishi katika nchi ambayo
watu wanafanyiwa ukatili mkubwa kiasi hiki halafu wanaachwa hivihivi,”
alisema Kibanda.
Kibanda alisema jambo lililomtokea lilikuwa baya kwani alikuwa akipoteza fahamu kila wakati kutokana na maumivu makali.
“Lakini sasa namshukuru Mungu, nimepona, sina
maumuvu tena kama yale,” alisema Kibanda na kuelezea kufurahishwa kwake
na ushirikiano mkubwa alioupata kutoka kwa wadau wa habari na wananchi
kwa jumla.
Ameiomba Serikali kuharakisha ripoti ya uchunguzi
wa tukio lake kwa sababu ni muda mrefu umepita na kwamba mpaka sasa
hakuna taarifa zozote zilizotolewa.
“Nilipolazwa Muhimbili Kitengo cha Moi, alikuja
kuniangalia Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova na
Mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema waliniahidi kushughulikia suala
langu ili waliohusika na tukio hili wafikishwe mahakamani,” alisema.
Alisema si hao tu, bali pia Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, ambaye alikwenda Afrika Kusini
kumjulia hali, alimwahidi kuwashughulikia watu waliohusika.
“Sisi sote ni mashahidi wa ukimya ambao upo kwani
mpaka sasa watu hao hawajakamatwa, wala hakuna taarifa zozote zinazohusu
kufikishwa mahakamani,” alisema.
Kibanda alisema katika miaka ya karibuni, kumekuwa
na matukio mbalimbali yanayohusisha kupigwa, kuuawa au kutishiwa maisha
kwa waandishi, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa matukio hayo hayaji
bure, kuna chanzo chake.