Dar es Salaam. Makachero wa Marekani
wameendelea na matayarisho ya mwisho ya ziara ya Rais Barack Obama,
ambapo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere walikuwa na
kazi ya kuunganisha helikopta za doria.
Makachero hao walikuwa wakiunganisha helikopta
sita zilizosafirishwa vipande vipande kutoka Marekani, ambapo meli mbili
za kivita na ndege moja pia zimewasili.
Rais Obama tayari yuko katika ardhi ya Afrika,
ambapo leo anatarajiwa kwenda Afrika Kusini baada ya kumaliza ziara yake
ya kwanza Senegal na anatarajiwa kuwasili nchini Jumatatu.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa jana na
Mwananchi unaonyesha Marekani imeleta helikopta hizo kwa ajili ya ulinzi
wa Rais Obama, zikiwemo meli zilizobeba helikopta nyingine mbili na
ndege.
Habari zilizopatikana kutoka kwa wafanyakazi wa
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,zinasema kuwa helikopta
sita zinaunganishwa katika sehemu ya karakana ya Kikosi cha Anga cha
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Mpashaji mmoja aliliambia gazeti hili kuwa
helikopta hizo zililetwa kama vipande vipande vilivyosafirishwa kama
mzigo kwenye meli za kivita zilizotia nanga jijini Dar es Salaam.
“Nilikaribia kwenye eneo la karakana na
nikashangaa kuona jinsi jamaa walivyokuwa ‘bize’ wakiunganisha vyuma
mbalimbali na kutengeneza helikopta hizo,” aliongeza mpashaji wetu,
ambaye alibahatika kusogelea eneo hilo licha ya kuwepo kwa ulinzi mkali.
Inaaminika kuwa helikopta hizo zitakuwa zinasaidia
kusafirisha watu na mizigo kutoka kwenye meli za kivita ambazo
zimeegeshwa kwenye Kikosi cha Maji cha JWTZ.
Pia helikopta mbili zinaaminika ziko katika meli ambazo zimeegeshwa huko Kigamboni.
Meli za kivita na ndege ya kijeshi
Katika hatua nyingine, meli mbili za kivita ambazo zimetengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu zimeegeshwa Kigamboni.
“Jamaa wana meli kali kwa kweli, mimi nimekuwa
askari wa Kikosi cha Maji kwa muda mrefu na kufanya mazoezi na mataifa
kadhaa, lakini sijaona meli kama zile.
“Wamarekani wanatisha sana. Meli zao zina zana muhimu za kivita.
Pia wanafuatilia kila kitu kinachoweza kuhatarisha usalama wao.
Hawaamini mtu kabisa wala kudharau chochote,” aliongeza mtoa habari
mmoja.
Ndege ya kijeshi
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kuna ndege ya Jeshi la Marekani lakini imeegeshwa kwenye karakana ya Kikosi cha Anga cha JWTZ.
Ndege hiyo inadaiwa iko nchini tangu mwanzoni mwa
wiki hii, ingawa kuna taarifa kuwa zipo ndege nyingine ambazo zimekuwa
zikitua na kuruka.
“Ndege nyingi za Wamarekani zinatua nchini kwa
kipindi cha wiki mbili sasa, zaidi zinaleta watu, ambao nahisi ni wale
wanaohusika na usalama na mizigo.
“Kimsingi kuna mambo mengi yanaendelea hapa uwanja
wa ndege. Ila msisahau pia kuna ujio wa marais kutoka sehemu mbalimbali
duniani kwa ajili ya mkutano wa Smart Partnership ndiyo maana kuna
mengi yanaendelea hapa,” kiliongeza chanzo chetu.
Matapeli waibuka
Kuna habari pia, kuna kundi la watu limeibuka
jijini Dar es Salaam ambalo linataka kutapeli wakazi wa jiji kwa kutumia
mgongo wa ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama.
Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalumu, Suleiman Kova
aliliambia gazeti hili kuwa wamepelekewa kesi tatu za majaribio ya watu
kupora wengine kwa kutumia mgongo wa Obama.
Ziara ya Rais Obama imesababisha kuongezeka kwa
mahitaji ya usafiri na malazi, hali iliyosababisha kuibuka kwa matapeli
wanaowalenga watu wenye magari yenye hadhi kwa wageni wa nje.
Pia hali hiyo imechangiwa zaidi kutokana na ugeni
wa viongozi wapatao 11 kutoka mataifa mbalimbali duniani, wanaohudhuria
mkutano wa Smart Partnership unaoanza leo jijini Dar es Salaam.
Kova alisema kundi hilo limekuwa likiwasiliana na watu wanaomiliki magari ya kifahari ili wakodishe magari yao.
Source:Mwananchi
Source:Mwananchi