HATIMAYE aliyekuwa kiungo wa Simba, Amri Kiemba, amekubali rasmi
kuachana na klabu hiyo na sasa atakuwa mchezaji wa Yanga msimu ujao.
Awali, Kiemba ambaye anatarajiwa kutua leo akitokea nchini Morocco
alipokuwa na kikosi cha Taifa Stars, alikuwa na kigugumizi kizito juu ya
kusaini mkataba mpya na Simba, kutokana na Wekundu hao kushindwa
kukubali dau alilotaka la Sh milioni 30 na mshahara wa dola 1,500 (sawa
na Sh milioni 2.4).
Ofa hiyo ilionekana ngumu kwa Wekundu hao ambao
walitaka kumpa Sh milioni 20 pekee nyota huyo ambaye aliifungia timu
hiyo mabao saba katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita.
Kwa mujibu wa
taarifa ambazo Championi Jumatatu limezipata kutoka kwa kaka wa kiungo
huyo, Ulimwengu Hamim, tayari Kiemba ameshakubaliana na Yanga juu ya
uhamisho wake, ambapo mara baada ya kutua leo, atasaini mkataba na klabu
hiyo wenye thamani ya Sh milioni 35.
Ulimwengu ambaye pia ndiye
Meneja wa Kiemba, alisema mbali na dau hilo, kiungo huyo atakuwa
akichukua mshahara mnono wa dola 2,000 (sawa na Sh milioni 3.2), ambapo
makubaliano hayo ameyafanya akiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya
Yanga, Abdallah Bin Kleb.
“Nilikwambia muda mrefu kwamba Yanga
walikuwa wanamhitaji sana Kiemba, lakini mimi kama meneja wake niliwapa
heshima sana Simba, niwe wazi, ofa ya Simba ilikuwa ndogo kulingana na
mahitaji na thamani ya Kiemba na ndiyo maana tulishindwa kukubaliana,”
alisema Ulimwengu na kuongeza:
“Tumekubaliana kila kitu, namsubiri
Kiemba arudi huko kesho (leo), nafikiri jioni yake tutakutana tayari kwa
tendo la kusaini mkataba mpya na Yanga utakaomfanya kuwa Yanga kwa
miaka miwili, nadhani hilo sasa limekwisha.”
Kiemba ndiye mchezaji
aliyekuwa akitumainiwa zaidi na Simba msimu uliopita. Kutua kwake
Jangwani kunaifanya Simba iwe imepigwa bao mara mbili na Yanga. Awali
Jangwani walimsajili beki Kelvin Yondani baada ya Wekundu kuonekana kuwa
na kigugumizi juu ya kumsajili.