MENGI yameibuka kufuatia kuuawa mfanyakazi wa ndani wa Jaji Engera
Kileo na kutupwa jirani na nyumba ya Kamishna wa Polisi, Suleiman Kova,
Mikocheni kwa Kova, jijini Dar.
Habari za uchunguzi wa gazeti hili zimebaini kuwa
msichana huyo, Pepetua Nyambura Maina (pichani), inadaiwa aliuawa na
mfanyakazi mwenzake Philemon Laizer (27) ambaye pia alikuwa akimtumikia
Jaji Kileo.
MAPENZI YATAJWA
Habari zaidi zilidai kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa
ni mtunza bustani katika nyumba ya Jaji Kileo na ilidaiwa kuwa wawili
hao walikuwa na uhusiano wa siri wa kimapenzi lakini siku za hivi
karibuni wakawa hawaelewani.
“Walikuwa marafiki wakubwa na
inawezekana kijana alipoona msichana hamtaki tena, akaamua kumchinja. Ni
uamuzi wa kikatili lakini ameufanya na kutuacha tumeduwaa,” kilidai
chanzo.
Kijana Laizer anayedaiwa kufanya unyama huo ni Mmasai na
alitiwa mbaroni na alipokaguliwa chumbani kwake, polisi walikuta nguo
zilizolowa damu inayosadikiwa kuwa ni ya marehemu na wanaamini zililowa
wakati anamchinja.
Licha ya nguo zenye damu, pia polisi walikuta
kiatu kimoja ndani ya chumba chake ambacho kilikuwa kimevaliwa na
marehemu kabla ya kuchinjwa.
Katika uchunguzi zaidi, habari zilidai
kijana huyo alikutwa pia na nguo alizokuwa amevaa mrembo huyo wakati
anakwenda kulala siku ya tukio zikiwa na damu.
“Polisi wanaamini kuwa Laizer alikuwa na wenzake, hivyo watuhumiwa wa mauaji haya ni lazima waongezeke,” kilidai chanzo chetu.
Habari
za kina zinasema kuwa wawili hao walikuwa wanaelewana sana kiasi kwamba
kwa yule ambaye alikuwa hajui angeweza kudhani kuwa walikuwa ni mtu na
mdogo wake.
KINACHOSHANGAZA
Hata hivyo, kinachowashangaza watu ni kutosikia
sauti yoyote ya kulalamika ya Pepetua kwani nyumba ya jaji ambayo wawili
hao walikuwa wakiishi ipo karibu na nyumba za viongozi wa ngazi za juu
serikalini na wengi wao wana walinzi kwenye mageti yao.
KOVA ANASEMAJE?
Akizungumzia tukio hilo, Kamishna Kova alikiri
kukamatwa kwa Laizer akiwa na kiatu na nguo za marehemu pamoja na zake
zilizokuwa na damu, huko maeneo ya Mikocheni B kulipotokea mauaji hayo.
“Tukio
hilo lilitokea karibu na dampo la kutupa takataka Mikocheni ‘B’, katika
eneo linalomilikiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
“Mfanyakazi
huyo wa ndani alikutwa ameshakufa baada ya mwili wake kuchinjwa sehemu
ya shingo, jeraha sehemu ya mkono wa kushoto karibu na kiganja, jeraha
kwenye paji la uso na mwili wake ukiwa umetapakaa damu sehemu za
kichwani,” alisema Kova.
Alieleza kuwa mtuhumiwa huyo aliyekuwa
akifanya kazi pamoja na marehemu, alikiri kuwa na marehemu siku hiyo ya
Ijumaa ya Juni 8, mwaka huu.
“Baada ya mahojiano ya muda mrefu,
alidai kuwa marehemu alitoweka nyumbani tangu Ijumaa na baada ya kubanwa
na polisi mtuhumiwa alikiri kuhusika na tukio hilo na atafikishwa
mahakamani wakati wowote, ” alisema Kamishna Kova.
MWILI WAAGWA, WASAFIRISHWA
Mwajiri wa Pepetua, Jaji Kileo alimwaga
machozi wakati wa kuuaga mwili nyumbani kwake Mikocheni B na baadaye
ulisafirishwa kupelekwa kwao Naivasha, nchini Kenya kwa mazishi.
Habari hii imeandikwa na Makongoro Oging, Haruni Sanchawa na Issa Mnally.
MENGI YAIBUKA MREMBO ALIYECHINJWA JIRANI NA KWA KOVA MKOCHENI
0
June 18, 2013
Tags