KIKONGWE Somoe Issa, anayekadiriwa kuwa na umri zaidi ya miaka 90,
ambaye aliwahi kutishia kuigeuza gesi kuwa maji iwapo serikali
itaendelea kulazimisha kusafirisha kwenda Dar es Salaam, sasa hajulikani
alipo.
Taarifa zilizoifikia MTANZANIA Jumapili ambayo ipo mkoani Mtwara,
zilidai kuwa bibi huyo baada ya kutoa tishio hilo sasa amefichwa, ili
asiweze kutekeleza lengo lake hilo.
Bibi Somoe, anayeaminika kama
Mkuu wa Kaya ya Msimbati, kijiji ambacho gesi asilia iligundulika, sasa
hajulikani alipo, huku ndani ya kijiji hicho ulinzi mkali ukiwa
umeendelea kutawala.
Ulinzi umeimarishwa katika kijiji hicho,
lengo likiwa ni kuhakikisha hakuna mtu anayefika karibu na nyumba
aliyokuwa akiishi bibi huyo.
MTANZANIA Jumapili, lilifika katika
kijiji hicho juzi, ambako liliweza kuzungumza na Mwenyekiti wa Kijiji
cha Msimbati, Salum Athuman Tostao, ambaye alikiri kuwa bibi huyo hayupo
na wala haifahamiki alikopelekwa.
“Ni kweli bibi huyu
hajaonekana tangu palipotokea vurugu na watu wa usalama waliokuwa
wakitaka kumuiba, kama unavyofahamu kulikuwa na mtu aliyejifanya
mwandishi wa habari alitaka kumuiba bibi huyu, lakini wanakijiji
wakamshtukia na kuchoma gari lake moto.
“Kutokana na hali hiyo,
mpaka sasa hatufahamu alipo na hatujui kama ni serikali au wanafamilia
wamemficha, kwa sababu kwanza hawaturuhusu hata sisi ambao ni viongozi
kufika maeneo ya nyumba aliyokuwa akiishi kwa sababu wanadhani tutaleta
watu wengine wasiokuwa waaminifu kwa familia hiyo,” alisema Tostao.
Gazeti
hili lilipomtafuta mtoto wa bibi huyo, Manzi Faki, alikataa kuzungumza
chochote kuhusu mama yake, lakini aliitaka serikali kutekeleza ahadi
zake kwa Wanamtwara.
“Hilo suala la mama sitaki kulizungumzia
kabisa… jambo la muhimu serikali inapaswa kufahamu kuwa sisi wana Mtwara
tunataka itekeleze ahadi ilizotuahidi ndipo waje kuchukua hicho kidogo
wanachokitaka, zaidi ya hapo kijumla gesi haitoki,” alisema Faki.
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Mtandi, Salum Waziri, alieleza kuwa bibi huyo anaaminiwa
na wanakijiji wenzake kutokana na uwezo wake wa kuzuia mambo
yasiyotakiwa ndani ya jamii, sambamba na kuleta riziki pale wanapokwenda
kumuomba.
“Kwa kweli sasa ulinzi mkali umeimarishwa na
wanakijiji, hakuna mtu anayefika nyumbani kwake, hata sisi wenyewe
hatuthubutu, ndiyo maana hatufahamu alikopelekwa.
“Nakumbuka bibi
aliwahi kutumiwa na kampuni ya Artumas kukwamua mashine iliyokuwa
imenasa katika mchakato wa uchimbaji wa gesi hiyo baharini, ambapo
wazungu hao walihangaika kuita wahandishi nje ya nchi, lakini wote
wakashindwa, ndipo waliponong’onezwa kuhusu bibi huyo wakamwendea na
akaja kunasua.
“Wakampa zawadi ya kumjengea nyumba, haya ni mambo
ambayo yalitokea mwaka 1994, kiujumla yapo mengi ambayo yametufanya
tumwamini sana,” alisema Waziri.
Januari mwaka huu, Afisa usalama
mmoja anayedaiwa kufahamika kwa jina la babu alijikuta katika wakati
mgumu kiasi cha gari lake kuchomwa moto huku yeye mwenyewe akikimbilia
kusikojulikana baada ya kuzuka vurugu kubwa wakati akimshawishi bibi
huyo asizuie gesi kwenda Dar es salaam.
Inadaiwa kuwa
mwanausalama huyo alitumwa na viongozi wa juu wa serikali baada ya bibi
huyo kutamka wazi kuwa gesi haitoki Mtwara kauli ambayo iliwafanya
viongozi kupata wasiwasi na hivyo kumtuma mtu huyo ili amshawishi bibi
huyo.
Wakati bibi huyo akizungumza na mwanausalama huyo inadaiwa
kuwa aliwaita wajukuu zake wamsikilize ndipo vurugu kubwa zilipoibuka na
kusababisha mwanausalama huyo atimue mbio huku akilitelekeza gari lake.
Juzi
na jana baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wakizungumza na gazeti hili
walisema wao hawazuii gesi kutumiwa na Watanzania, ila wanataka gesi
hiyo ichakatwe hapohapo mkoani Mtwara na ndipo isafirishwe kuelekea
sehemu nyingine.
Vurugu kuhusu gesi hii ya Mtwara zilianza
kuibuka Novemba mwaka jana, wananchi wa mkoa huo walikuwa wakipinga
ujenzi wa bomba la gesi kwenda Dar es Salaam.
Pamoja na vurugu
hizo kuzimwa mara kadhaa na Jeshi la Polisi, ambao sasa wanashirikiana
na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), lakini bado MTANZANIA Jumapili
imeshuhudia hali ya amani haijaweza kurejea mkoani humo.
Baadhi
ya watu mkoani hapa, bado wanaendeleza visasi kwa kuchoma nyumba za
wenzao, huku JWTZ wakidaiwa kuwapiga raia kila mara hata inapotokea kuwa
wamezomewa.
MTWARA-BIBI KIZEE ALIYESEMA ATAGEUZA GESI KUWA MAJI ATOWEKA
0
June 16, 2013
Tags