Chama Cha
Mapinduzi (CCM), kimepinga muundo wa Muungano wa Serikali tatu
unaopendekezwa katika rasimu ya Katiba Mpya iliyotolewa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba mwanzoni mwa wiki iliyopita.
Chama hicho tawala kimesema bado kinaamini katika muundo wa Serikali mbili.
Katibu wa Itikadi
na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye aliwaambia waandishi wa habari mjini
Dodoma jana kwamba mapendekezo yaliyowasilishwa mbele ya Tume hiyo
yanabaki kama yalivyo, hivyo msimamo wao ni kuwapo kwa muungano wenye
muundo wa Serikali mbili.
“Mapendekezo
ambayo ndiyo msimamo wa chama tulishayawasilisha kwenye Tume kuwa sisi
tunapendekeza mfumo wa Serikali mbili na siyo tatu wala moja,” alisema
Nape alipokuwa akitoa taarifa ya uamuzi wa Kamati Kuu (CC) ya CCM
iliyokutana usiku wa kuamkia jana kujadili suala hilo.
Kauli ya Nape
inafanana na matamshi ambayo yamewahi kutolewa na baadhi ya wanasiasa
wakongwe ambao ni makada wa CCM wakiwamo, mawaziri wakuu wastaafu,
Frederick Sumaye na John Malecela, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Samuel Sitta na baadhi ya wabunge ambao mara kadhaa
wamekaririwa wakipinga pendekezo la Serikali tatu.
Hata hivyo, Nape
alisema matamshi ya viongozi hao yalikuwa ni maoni yao binafsi na kauli
yake ndiyo rasmi ya chama hicho... “Mimi ndiye msemaji wa chama hiki.
Ndiye ninayeeleza msimamo wa chama chetu, yanayozungumzwa na watu
wengine hata kama ni viongozi siyo msimamo wa chama ni maoni yao
binafsi.”
Habari ambazo
gazeti hili ilizipata zinasema katika kikao hicho cha CC kulijitokeza
hofu ya suala la wananchi kuwa na mamlaka ya kuwang’oa wabunge ikiwa
hawatatekeleza masilahi yao na kwamba pendekezo hilo lina upungufu kwani
halitafsiri masilahi hayo ni yapi.
Waunda kamati
Nape alisema
rasimu iliyotolewa na Tume siyo waraka wa mwisho kwani bado unatoa fursa
kwa Watanzania kuijadili na kutoa maoni yao na kwamba CCM kitatumia
nafasi hiyo kuwasilisha maoni yake kuhusu jambo hilo.
Alisema chama hicho kitawasiliana na wanachama wake zaidi ya 6,000 nchini ili waendelee kutoa maoni yao kuhusu suala hilo.
“Wengi wanadhani
rasimu hii ndiyo ya mwisho… hii ni ya mwanzo tu, itajadiliwa italetwa ya
pili na ya tatu, kwa hiyo hatuwezi kusema kilichoelezwa kwenye tume
ndiyo msimamo. Ndiyo maana tumeamua kurejesha suala hili kwa wanachama
wetu liendelee kujadiliwa,” alisema na kuongeza:
“Kama wanachama
wetu wakiamua kuwepo kwa Serikali tatu, hatutachakachua, tutayachukua na
kuyapeleka kama msimamo wetu, lakini tutakubaliana ikiwa uamuzi utakuwa
umewahusisha wanachama wetu katika ngazi zote.
“Hatuangalii
kipengele kimoja tu. Tutapitia vipengele vyote hadi kuzimaliza kurasa
zote zaidi ya 70 zinazoainisha mapendekezo ya Tume ya Jaji (Joseph)
Warioba.”
Alisema wanachama
wake wanapaswa kuipitia na kuijadili rasimu hiyo kwa kuzingatia
mapendekezo kilichoyatoa awali wakati wa mchakato wa kukusanya maoni ya
Katiba Mpya.
“Tulitoa maoni
yetu na sasa tunaijadili Rasimu ya Katiba Mpya kwa kuzingatia maoni yetu
yale, CCM tunakwenda kwa mujibu wa sheria,” alisema. Habari kutoka
ndani ya CC ya CCM zinasema chama hicho kimeipa kazi kamati ambayo
ilitumika kuandaa mapendekezo yake awali, kupitia rasimu hiyo na kufanya
ulinganisho wa yale ambayo chama hicho kilipendekeza dhidi ya yale
yaliyozingatiwa katika Rasimu ya Katiba hiyo.
“Kamati itafanya
ulinganisho na baada ya hapo tutakwenda kwa wanachama kuwaeleza ni yapi
tulipendekeza kama chama na ni yapi ambayo Tume imeyazingatia na hapo
tutapata mawazo yao ambayo tutayatumia katika ngazi ya mabaraza ya
Katiba,” kilisema chanzo chetu.
Kwa hisani ya gazeti la Mwananchi