Dodoma. Siku moja baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba kuweka hadharani Rasimu ya Katiba, wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wamekuwa wakitumia muda mwingi kuijadili na kushindwa kufuatilia kikamilifu vikao vya Bajeti vinavyoendelea Mjini Dodoma.
Tangu kutangazwa kwa rasimu hiyo Jumatatu iliyopita wabunge wengi wameonekana kukaa katika vikundi na kuijadili.
Siku hiyo, wengi walishindwa kufuatilia hoja za Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ambayo ilikuwa ikihitimisha mjadala wake wa Makadirio kiasi cha kumlazimu Naibu Spika, Job Ndugai kuingilia kati kuwanyamazisha kutokana na kuendeleza mjadala kuhusu Katiba ndani ya Bunge.
“Waheshimiwa Wabunge, hili la rasimu lisiwachanganye, hebu tuache mijadala (kuhusu Rasimu ya Katiba), tumsikilize Mheshimiwa Naibu Waziri (Januari Makamba),” aliwaeleza wabunge.
Hata wakati Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alipokuwa akiwasilisha hotuba yake ya makadirio ya wizara yake juzi, baadhi ya wabunge walikuwa wakizungumzia Rasimu ya Katiba na kumlazimu Spika wa Bunge, Anne Makinda kukatisha hotuba ya Dk Kawambwa na kusema: “Tuacheni mazungumzo, naona wabunge wengine wamegeuza na viti na hawasikilizi.”
Maeneo yaliyotajwa kwenye rasimu na kuwagusa wabunge moja kwa moja ni kufutwa kwa viti maalumu badala yake, ukomo wa ubunge ambao ni mihula mitatu, mawaziri kutokuwa wabunge na wananchi kupewa uwezo wa kuwang’oa wabunge.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alisema wabunge kutokuwa mawaziri kutaleta mkanganyiko mkubwa... “Pendekezo hilo limetuvuruga wengi kwani tulishazoea kufuata mfumo wa Bunge la Uingereza, ambao unaelekeza kuwa waziri lazima awe mbunge ama wa kuteuliwa au wa kuchaguliwa.”
Simbachawene ambaye pia ni Mbunge wa Kibakwe (CCM), alisema muundo wa Serikali tatu utavuruga Muungano.
Mbunge wa Ole (CUF), Rajab Mbarouk Mohamed kwa upande wake alisema: “Naona Serikali tatu zitaongeza kero za Muungano kama mambo ya umiliki wa rasilimali, fedha, Wizara ya Mambo ya Nje na ukusanyaji wa kodi havitawekwa kuinufaisha Zanzibar.”
Mbunge wa Urambo Magharibi (CCM), Profesa Juma Kapuya alisema kwa Tanzania inayotawaliwa na vurugu na migogoro kila mahali, Rais hapaswi kupunguziwa nguvu na kwamba jambo hilo ni la hatari.
Profesa Kapuya ambaye aliwahi kwa waziri katika wizara mbalimbali alisema Rais anateua mtu kwa kuangalia hali ya mahali husika na uwezo wake katika utendaji kazi.