Dar es Salaam/Dodoma: Mapendekezo yaliyotolewa katika Rasimu ya
Katiba Mpya na Tume ya Marekebisho ya Katiba yamewavuruga wanasiasa
ambao tayari walikuwa wamejipanga kwa ajili ya kuwania urais katika
Uchaguzi Mkuu wa 2015, Mwananchi limebaini.
Tangu juzi Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph
Warioba alipotangaza rasimu hiyo, kumekuwa na wasiwasi mkubwa sasa
kwamba mipango ya urais wa 2015 itavurugika ikiwa mapendekezo hayo
yatapitishwa.
Tishio kubwa katika rasimu hiyo ni pendekezo la
kuwapo kwa Serikali ya tatu hali ambayo inatafsiriwa na baadhi ya
wanasiasa kwamba inaondoa nguvu ya Rais yeyote; awe wa Jamhuri ya
Muungano, Zanzibar au Tanzania Bara.
Habari za kuaminika zilizopatikana kutoka ndani ya
kambi za vyama vya CCM na Chadema zinaeleza kuwa wale waliokuwa
wakifikiria kuwania nafasi hiyo wameingiwa na wasiwasi.
Kadhalika, suala la umri wa kuwania urais kubakia
miaka 40 pia linaonekana kuwagusa waliowahi kutangaza kutaka nafasi hiyo
ya juu ya uongozi wa nchi kabla ya mapendekezo ya tume.
Katika suala la urais, wanasiasa wenye nia hiyo
wanauona uongozi wa Jamhuri ya Muungano kuwa ni kama hauna nguvu tena
kutokana na kushughulikia mambo machache, lakini wakati huohuo wanauona
urais wa Tanzania Bara kwamba hauna mamlaka kamili ya kuwawezesha
watambuliwe nje ya nchi.
Tume ya Marekebisho ya Katiba imependekeza mambo
saba tu yawemo chini ya Serikali ya Muungano kati ya 22 ya sasa.
Yanayopendekezwa ni Ulinzi na Usalama, Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya
Muungano, mambo ya nje, sarafu na Benki Kuu, uraia na uhamiaji, usajili
wa vyama vya siasa, ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo
na Muungano.
Ndani ya CCM
Makundi mbalimbali yanayowania urais ndani ya CCM inaaminika hayajafurahishwa na mapendekezo ya rasimu ya kutaka Serikali tatu.
Kwa maneno mengine, wanaona kama Rais wa Muungano
ameng’olewa baadhi ya meno na masuala mengi yatakuwa yanashughulikiwa na
Serikali ya Tanzania Bara na ile ya Zanzibar.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel
Sitta amesema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeliacha hewani suala la
Tanganyika hasa baada ya kutoa mapendekezo ya Serikali tatu kwenye
Rasimu ya Katiba.
Sitta ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM),
alisema hakuna mantiki ya kuunda Serikali tatu ikiwa Tume haikutoa
mwongozo wa hali itakavyokuwa kwa Tanzania Bara, Serikali ya Muungano na
ile ya Zanzibar.