Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika mikoa mbalimbali
nchini umegundua kuwa mbali ya kusambaratisha ndoa nyingi, simu pia
zimekuwa adui mkubwa kwa baadhi ya watumiaji badala ya kuwanufaisha kama
inavyotakiwa.
Uzuri na ubaya wa simu
Wananchi walieleza uzuri na ubaya wa simu ambapo
Peter Tesha mkazi wa Arusha aliitaja simu kuwa ndiyo chanzo cha
kumfikisha alipo sasa akikosa fedha za matumizi yake ya kawaida licha ya
awali kumiliki miradi mingi iliyokuwa ikimwingizia kipato.
Anaeleza kuwa baada ya kuoa mwaka 2009,
alibahatika kupata watoto wawili na mkewe na maisha yao yakaendelea
vizuri huku yeye akiendelea na biashara yake ya maduka matatu aliyokuwa
akilimiki jijini Arusha na mawili ya Moshi.
Anasema kuwa katika maisha yake na mkewe hakuwahi kushika simu ya mkewe huyo mbali mkewe kuwa hodari wa kuchunguza simu yake.
Hata hivyo siku moja bila kupanga alichukua simu
ya mkewe na kusoma ujumbe mfupi aliotumiwa, jambo analoapa kutolifanya
tena maishani mwake kwani alikutana na ujumbe aliouelezea kuwa ulikuwa
wa majibizano kati ya mkewe na mwanamume mwingine ambaye hata hivyo jina
lililotumika lilikuwa la kijiji badala ya mtu.
“Siwezi kusahau, hata huu umaskini unaoniandama ni
madhara ya simu. Ujumbe ule ulikuwa wa kulaumiana kati ya mke wangu na
huyo mwanamume kuwa hawa watoto wangu ni wake, mke wangu akiuliza; Kwa
nini umewatelekeza na kuniachia mzigo wa kulea mimi ambaye siyo watoto
wangu?”anasema Tesha.
Anafafanua kuwa ujumbe huo ulifafanua: “Kama
akiendelea kufanya hivyo ataiuzilia mbali nyumba aliyompa kwa ajili ya
watoto, ambao mimi siku zote nilikuwa nikiamini ni baba yao.”
Anaeleza kuwa tangu alipofungua simu ya mkewe na
kusoma ujumbe huo maisha yake yalibadilika kwani alikwenda kuwapima DNA
watoto hao na kumbana mama yao ambapo ilibainika kuwa ni kweli watoto
hao sio wake, jambo lililomchanganya na kumtia aibu kwenye familia na
jamii hivyo akaamua kuwa mlevi.
Tesha anasema kuwa kuanzia hapo aliacha kusimamia
biashara zake kutokana na kuchanganyikiwa na kukwepa aibu, huku akiishi
kwa kujificha kwa zaidi ya mwaka na alipotulia na kujifikiria kwa nini
amekuwa hivyo alikuwa tayari ameshachelewa, kwa kuwa baadhi ya maduka
yalikuwa yamefungwa na aliowaacha hakuwa na cha kuwafanya akibaki na
duka moja la Arusha ambalo pia lilikuwa limekufa kutokana na kuwa na
bidhaa chache.
“Naishi kwa ushauri na ndiyo maana mara nyingi
nimekuwa nakutumia ujumbe wa kutaka unishauri kwa kuwa siiamini tena
akili yangu wala mwili wangu. Kama mwanamke ambaye nilikuwa naishi naye
miaka yote aliweza kubeba mimba za mtu mwingine na nisijue, sina sababu
ya kujiamini tena, nimekuwa masikini kwa sababu ya simu, sitamani simu
ya mtu zaidi ya hii yangu, ambayo wakati mwingine huwa naamua
kuifunga,”anamaliza Tesha.
Wakati Tesha akieleza hayo, upande mwingine
Jennipher Lazaro wa Tanga anasema kuwa hawezi kuishi bila simu kwa kuwa
humsaidia mambo mengi ikiwamo kujifunza zaidi kupitia mtandao,
kumuunganisha na marafiki walio mbali naye.
Anafafanua
kuwa akiambiwa achague kati ya simu na kuzungumza na mtu anayempenda
kama mumewe atachagua simu kwa kuwa haimuuzi, lakini mumewe kuna siku
huwa anamkera.
Naye Zaituni Mapunda (siyo jina halisi) wa Mbeya
anasema kuwa simu kwake ni rafiki na adui, kwani imekuwa ikimpa mambo
mengi mazuri huku pia ikimsababishia matatizo.
“Nikiachwa basi, cha kwanza kukilaumu ni simu
kwani mara nyingi nakorofishana na mpenzi wangu, anakuta ujumbe
niliotumiwa na wanaume wengine nasahau kuufuta,”anasema Mapunda.
Anafafanua kuwa mbali na hayo, bado anaithamini
zaidi simu kwa kuwa ni kiunganishi kikubwa kati yake na watu wake wa
karibu, huku akikiri kuwa mara nyingine hufanyia mambo yasiyo sahihi,
ikiwemo kuwasiliana na wanaume wengi kwa wakati mmoja, ambao huwapanga
kirahisi kwa kutumia simu.
“Nina uwezo wa kuwa na wanaume wengi kwa kutumia
simu, lakini pia maisha yangu yanakuwa na unafuu kupitia simu,”anasema
na kuongeza:
“Kama nitapewa adhabu kubwa basi ni kuambiwa
nisiwe na simu au mpenzi wangu akishinda na simu yangu hawezi kuishi
wala kunipenda tena maishani mwake, kwani atapigiwa simu na wenzake hadi
atashangaa.”
Mudi Mkotopaje wa Dar es Salaam anasema kuwa
ameshaacha wanawake wawili kutokana na kukuta maovu kwenye simu na
kwamba aliyenaye kwa miaka miwili tangu waoane hataki awe na simu.
Anafafanua kuwa simu ni kishawishi kikubwa na
kwamba wanawake wote aliwaacha huku bado anawapenda na wote walikuwa na
kesi zinazofanana za kuwa na matumizi mabaya ya simu kwa kufanya
uhusiano usio rasmi.
Anatoa ushauri kuwa hata kwa wazazi ili mabinti zao wasome kwa uhuru na kuelewa walichokusudia wasipewe simu.
Mwamvua Jumbe mama wa watoto wawili, anasema kuwa aliachana na mumewe kutokana na kumkuta na ujumbe wa mapenzi karibu kila siku.
“Wazazi wangu na wake walinikanya kuhusu
kuchunguza simu yake nilishindwa kwa kuwa nilikuwa nampenda na nilikuwa
naamini kuwa kuna kitu tofauti anafanya kunizunguka. Kila nilipojaribu
kumchunguza nilimkuta na hatia. Kama ikitokea nikaolewa tena sintotaka
kuwa karibu na simu ya mume wangu ili nisijue anachokifanya, kutokana na
kupata shida ya kumlea mtoto peke yangu ,”anasema.
Mwanasaikolojia azungumza
Mtaalamu wa masuala ya saikojia wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom)
Modesta Kimonga alisema kuwa matumizi mabaya ya simu ni kifo kwa kuwa
akili ya binadamu inabadilika kulingana na tukio lililotokea.
Alitoa mfano kuwa wakati msiba ukitokea mtu
analia, akiona kitu siyo cha kawaida anaweza kufurahi au akatabasamu,
akiongeza kuwa mtu ikiona kitu tofauti na inavyotarajiwa hubadilika na
ndiyo sababu kuna watu wanajiua kwa vitu vidogo.
“Miongoni mwa vitu ambavyo tunatakiwa kuwa na
tahadhari navyo ni simu kwani vinaweza kuleta athari kubwa kama
havikutumiwa vizuri kwa matumizi yaliyokusudiwa tofauti na hapo zinaweza
kuleta maafa,”anasema na kufafanua:
“Kwa mfano mume au mke anapekua simu ya mmojawao
bila idhini ya mwenzake na kukuta kitu tofauti kinachoweza kumpa hasira,
akapata matatizo ya kiafya au akaenda kumdhuru mkewe au mumewe kutokana
na akili yake kuvurugika kutokana na alichokiona. Kila mmoja aelewe
kuwa simu ya mkononi ni kwa ajili ya mwenye nayo.”
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
Mtaalamu wa takwimu ya Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania, Hango Juma, alitaja idadi ya watumiaji wa simu nchini hadi
Machi mwaka huu kuwa ni 27.6 milioni na kwamba mwenye haki ya kutumia
simu ni mhusika wa simu hiyo.
“Si ruhusa kwa asiyekuwa mmiliki halali wa laini
kuipeleleza kwa kwenda kwenye kampuni ya simu kujua amewasiliana na watu
wangapi au kwa namna yoyote ile. Wafanyakazi kwenye kampuni za simu
wanatakiwa kutunza siri za wateja kisheria na siyo kuzisambaza au
kuzitoa kwa wahusika hata kama ni laini zao,”anasema Juma.
Tafiti yagundua
Wakati hali ikiwa hivyo Tanzania, nchi 11 za Ulaya
zimefanyiwa utafiti na kubaini kuwa asilimia 94 ya watu wazima huona ni
heri waishi bila ngono kuliko kuishi bila simu za mkononi, huku
asilimia 65 ya watu waliofanyiwa mahojiano wakisema kuwa hawawezi kuishi
bila simu na asilimia 53 walikiri kuwa wameathirika na simu zao.
Zaidi ya 2,570 watu wazima nchini Uingereza, wenye
umri kati ya 18 na 30, walishiriki katika utafiti uliofanywa na
Mobileinsurance.co.uk ambapo iligundulika kuwa asilimia tisa ya watu
wazima wa Uingereza huona ni heri kuishi bila watoto wao kwa wiki kuliko
kukaa bila simu za mkononi.