Kuelekea ujio wa Rais Barack Obama nchini wiki ijayo, Jiji la
Dar es Salaam ambalo ndilo litakuwa mwenyeji wa mgeni huyo na ujumbe
wake hivi sasa limo katika hekaheka kubwa za kuandaa mazingira stahiki
kwa ugeni huo. Dar es Salaam ni moja ya majiji machafu sana duniani,
hivyo kila juhudi zinafanywa na mamlaka husika kuliweka jiji hilo katika
hali ya usafi kabla ya ugeni huo haujawasili.
Sasa sehemu nyingi za barabara zinatengenezwa
usiku na mchana kwa kujengwa upya au kuzibwa mashimo, ambayo baadhi yake
yalikuwa makubwa mithili ya mahandaki. Katika baadhi ya barabara,
mchanga na udongo uliokuwa umezimeza kutokana na kutotunzwa kwa muda
mrefu sasa vimeondolewa.
Taka zilizokuwa zimezagaa kila kona sasa
zinazolewa kwa kutumia magari ya Jiji na ya wamiliki binafsi. Katika
sehemu muhimu za Jiji, madawa ya kuua mbu na wadudu yamenyunyizwa, huku
baadhi ya wamiliki wa majengo katika sehemu atakazopita Rais Obama
wakilazimika kupaka rangi majengo hayo. Harufu mbaya iliyokuwa
imeligubika Jiji kutokana na uchafu sasa imepungua kwa kiasi kikubwa.
Ghafla vijana kutoka vijiweni wamepewa ajira ya
muda kufyeka nyasi, kuzibua na kusafisha barabara na mitaro iliyojaa
majitaka. Kumbe wanakaa vijiweni sio kwa kutaka, bali kwa kukosa ajira.
Polisi nao wameendesha kamatakamata ya vijana wengi inaodai ni vibaka,
wavuta bangi na vitendo vingine vya kihalifu, huku lengo kubwa likiwa ni
kusafisha mitaa kabla ya ujio wa Rais Obama. Wakati huohuo, Machinga
wameondolewa katika sehemu atakazopita mgeni huyo na ujumbe wake na
vibanda vyao vimefyekwa na tingatinga za Jiji, huku wananchi waishio
mikoani wakitahadharishwa kutokuja Dar es Salaam wakati Rais Obama
atakapokuwa jijini.
Jiji la Dar es Salaam zinazoendelea hivi sasa
jijini kuelekea ujio wa ugeni wa Rais huyo wa Marekani. Tumefanya hivyo
kwa sababu mbili kubwa. Kwanza ni kuonyesha kwamba Jiji la Dar es Salaam
na Serikali Kuu vinao uwezo mkubwa wa kulifanya jiji hilo kuwa safi
wakati wote. Pili ni kuonyesha jinsi tunavyojidhalilisha kama taifa kwa
kuishi katika mazingira machafu, lakini tunachukua hatua za zimamoto na
kukimbizana kufanya usafi tunapoona wageni wanatembelea nchi yetu.
Ni aibu iliyoje kwa Watanzania kuishi katika
mazingira machafu tukisubiri wageni waje ndio tufanye usafi. Ni dharau
na matusi ya viongozi wetu kwa wananchi, kwamba watu muhimu na ambao
wanastahili kuwekwa katika mazingira mazuri ni wageni. Wananchi
wanasakamwa walipe kodi na wanafanya hivyo. Pamoja na kulipa kodi hizo,
mamlaka husika hazioni umuhimu wa kuwatengenezea wananchi mazingira
mazuri kwa kuzoa taka, kutengeneza barabara, kufyeka nyasi, kunyunyizia
dawa katika mazalio ya mbu na kadhalika.
Usafi wa mazingira na wa kila mwananchi ni muhimu
mno katika ustawi na maendeleo ya binadamu. Wakati kila mwananchi analo
jukumu la kutunza usafi kwa nafsi yake na mazingira yaliyomzunguka,
mamlaka husika zinapaswa kuwawezesha wananchi kufanya hivyo.
Inawezekanaje halmashauri za miji na wilaya, kwa mfano, zishindwe kuweka
magari ya kuzoa taka kutoka barabarani na mitaani? Zipo wapi dampo za
kumwaga maelfu ya tani za taka zinazozalishwa katika makazi ya watu
mijini kila siku?
Source:Mwananchi
Source:Mwananchi