UTATA MKUBWA BOMU LILILOLIPUKA ARUSHA

Dar/mikoani. Mlipuko wa bomu uliotokea Arusha na kusababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi 70 limezua utata kutokana na hisia tofauti za viongozi mbalimbali nchini waliozungumzia suala hilo, huku Rais Jakaya Kikwete akisema haamini kama Watanzania sasa wamefikia hatua ya kuanza kuhasimiana kwa misingi ya kisiasa.
Hii ni mara ya pili kwa Jiji la Arusha kushambuliwa kwa bomu baada  ya lile lililorushwa kwenye Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi kwenye Parokia ya Olasiti wakati wa sherehe ya uzinduzi wake Mei 5, mwaka huu na kuua watu watatu na kujeruhi 64. Wakati Rais Kikwete akisema hayo, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba wamesema tukio hilo ni la kisiasa na lilipangwa.
Kufuatia tukio hilo, uchaguzi wa  kata nne za Arusha mjini umeahirishwa hadi Juni 30.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana imeeleza kuwa Rais Kikwete ambaye yuko nchini Uingereza kuhudhuria mkutano wa nchi zilivyoendelea kiviwanda(G8), alisema haamini kama Watanzania ama wafuasi wa vyama vya siasa wanachukiana kiasi cha kudiriki kufanya matukio ambayo yanahatarisha usalama wa watu.
“Mimi   siamini   kuwa  Watanzania au wafuasi wa vyama vya siasa wanachukiana kiasi cha kufanyiana matendo ya unyama wa aina hii. Naamini kuwa hiki ni kitendo cha mtu ama watu wasioitakia mema nchi yetu, watu ambao wanatafuta kila sababu ya kupandikiza chuki miongoni mwa raia ama makundi ya raia, ili nchi yetu iingie kwenye machafuko makubwa.”
Mbowe
Akizungumzia suala hilo,  Mbowe alisema shambulio hilo la bomu ni la kisiasa na lililenga kumuua yeye na Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema.
“Haya ni mauaji ya kisiasa ya kupanga, tumeokota maganda ya risasi za bastola na SMG na tumepiga picha na kuwapa polisi katika eneo la tukio, gari letu lilipigwa mlango na vioo kwa risasi na kesho wabunge wote wa Chadema watakuwa hapa Arusha na wataondoka baada ya mazishi,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema pia wamebaini bomu lililorushwa ni la kiwandani na shambulizi hilo liliandaliwa na kikosi cha watu wengi wenye lengo la kufanya mauaji makubwa.
Alisema kilichomwokoa na kifo ni kushuka jukwaani saa 11:43 kabla ya muda wa kawaida wa saa 12:00 kwani ilipangwa washambuliwe wakiwa juu ya jukwaa.
“Tunasikitika sana, watu wamekufa wasio na hatia na msiba huu utakuwa wa kitaifa na tunatarajia kuaga miili katika uwanja huohuo wa Soweto,” alisema Mbowe.
Profesa Lipumba
Kwa upande wake, Profesa Lipumba alisema watu waliohusika kulipua bomu walipanga kuvuruga uchaguzi huo uliyokuwa ufanyike jana.
Alisema CUF walikuwa na nguvu katika baadhi ya maeneo ya uchaguzi Arusha ndiyo mana watu wameamua kuvuruga uchaguzi  ili usifanyike.
“Sisi tumewasimamisha wagombea udiwani ambao ni Abbas Mkindi, (Kaloleni), John Bayo (Elerai) na Labora Ndarvio (Themi) na maeneo haya tulitegemea leo (jana) tushinde ila baadhi ya watu wameamua kuvuruga kwa malengo yao binafsi,” alisema Lipumba.
Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba amevitaka vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina kuwabaini watu waliohusika na milipuko hiyo ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Nchimbi na Mwema
Wakati viongozi hao wakigawanyika Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi na Inspekta Jenerali wa Polisi(IGP), Said Mwema wamesema tayari jeshi lake limetuma timu inayoongozwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja na Kamishna wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Isaya Mngulu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana Dk Nchimbi alisema uchunguzi wa awali umebaini ya kwamba bomu hilo ni la kurusha kwa mkono (hand grenade).
Hata hivyo, Dk Nchimbi alisema hadi sasa hakuna mtuhumiwa  yeyote anayeshikiliwa kutokana na tukio hilo.
“Uchunguzi wa awali umebaini kwamba bomu hilo ni la kutupa kwa mkono. Tunachunguza kujua mlipuko ule ni wa aina gani,” aliwaambia waandishi wa habari jijini  Arusha.
Dk Nchimbi alitaja orodha ya vifo katika tukio hilo na kusema hadi sasa watu wawili wamethibitishwa kufa, huku 70 wakiwa wamejeruhiwa ambapo kati ya majeruhi hao, wawili wako katika hali mbaya. Alisema kwamba uchunguzi huo unalishirikisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili kubaini mlipuko uliojitokeza ni wa namna gani.
Naye IGP Mwema alisema jeshi litaendesha operesheni kali popote nchini ya kuwasaka na kuwatia mbaroni wote waliowezesha, kufadhili na waliotenda uhalifu huo. Alisema Jeshi la Polisi linalaani tukio hilo linaloashiria vitendo vya kigaidi ambalo limesababisha vifo na majeruhi pamoja na kujenga hofu kwa wananchi.
“Nawashukuru wananchi walioanza kutupa taarifa za mwonekano, wajihi wa mtu aliyetupa bomu hilo,” alisema.

Mwema aliweka hadharani simu yake ya mkononi yenye namba  0754 785557  akitaka wananchi wenye taarifa kuhusu uhalifu huo kumpa mwenyewe taarifa au kwenye vituo vya polisi vilivyo jirani yao.
Imeandikwa na Raymond Kaminyoge, Aidan Mhando (Dar), Mussa Juma na Moses Mashalla (Arusha).

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad