Dar es Salaam. Suala la baadhi ya Watanzania kuhifadhi mabilioni
ya fedha nchini Uswisi limechukua sura mpya, baada ya tume maalumu
kuwahoji vigogo 200 wakiwamo wabunge, wanasiasa na wafanyabiashara.
Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa tume hiyo
inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema
tayari imeshafanya kazi hiyo kwa miezi miwili sasa.
Tume hiyo maalumu iliyoundwa na Serikali kwa
Azimio la Bunge lililotolewa mwishoni mwa mwaka jana, inatarajiwa
kukamilisha uchunguzi huo wakati wowote kuanzia sasa na kuwasilisha
ripoti hiyo katika kikao kijacho cha Bunge. Jaji Werema alipoulizwa na
Mwananchi Jumpili maendeleo ya uchunguzi huo, alisema kuwa kazi hiyo
bado inaendelea.
“Uchunguzi huo unaendelea,” alisema Werema huku
akisita kueleza kwa undani juu ya kazi hiyo kwa kile alichosema kuwa
hana sababu ya kufanya hivyo kwa sasa.
“Subiri uchunguzi bado unafanywa,” alisema Werema na alipotakiwa kueleza utamalizika lini alisema: “Utamalizika tu.”
Mwanasheria huyo wa Serikali alikataa kutaja baadhi ya majina ya watu ambao tume yake imewahoji mpaka sasa.
Alisema anashangazwa na swali la namna hiyo, kwa
maelezo kwamba ni jambo ambalo liko wazi kuwa ni kinyume na maadili
kuwataja watuhumiwa wakati huu uchunguzi ukiwa bado unaendelea.
Uchunguzi huo unafanyika baada ya Benki ya Taifa
ya Uswiss (SNB) kutoa taarifa mwezi Juni, 2012 kuhusu raia wa kigeni
wanaomiliki akaunti za benki nchini humo.
Orodha hiyo iliorodhesha pia baadhi ya Watanzania wenye akaunti zinazofikia Dola196 milioni ambazo ni sawa na Sh323.4 bilioni.
Jarida la kimataifa la uchunguzi la The Indian
Ocean Newsletter toleo la hivi karibuni, lilimnukuu Werema akisema
uchunguzi huo kwa sasa unatia matumaini.
Werema anaripotiwa akiri kuwa uchunguzi huo
umefikia ‘hatua ya kutia matumaini’ na wanaendelea na kazi hiyo kwa
uangalifu ili kuwa na uhakika wa taarifa wanazozitafuta.
Alisema kwamba taarifa ya awali inatarajiwa
kutolewa hivi karibuni na tayari idadi kubwa ya wahusika wakiwamo
wabunge wameshahojiwa.
Werema alisema wanaendelea na uchunguzi kuwabaini zaidi ya Watanzania 200, waliotajwa kuficha mabilioni ya fedha nje ya nchi.
Mbali na Werema, tume hiyo inaundwa na viongozi
kadhaa wa taasisi nyeti kama vile Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea, Mkurugenzi wa Usalama
wa Taifa, Rashid Othman na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno
Ndulu.
Tume hiyo inawahusisha pia Mkuu wa Sheria wa BoT,
Mustapha Ismail na maofisa kutoka idara ya upelelezi na ofisi ya
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali.
Kwa mujibu wa jarida hilo la kimataifa, miongoni
mwa watuhumiwa hao ni wanasiasa na majenerali wastaafu wanaotuhumiwa
kutorosha zaidi ya Dola 133 milioni mwaka 2005, kupitia Mfuko wa Ulipaji
Madeni ya Nje (EPA)
Baadhi ya watu wanaodaiwa kuhusika wamehojiwa
kutokana na taaluma zao, familia zao, akaunti zao za benki zilizoko
nchini na nje ya nchi pamoja na nchi walizotembelea mara kwa mara kwa
miaka mitatu iliyopita.
Lengo la kuwahoji inaelezwa ni kutaka kujua iwapo
walifuata njia zinazotakiwa katika kufungua akaunti hizo nje ya nchi na
iwapo fedha zilizohifadhiwa huko zilipatikana kihalali.
Sakata la kashfa hiyo liliibuliwa Bungeni kwa hoja binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe mwishoni mwa mwaka 2012.
Zitto alisema kwamba kiasi cha fedha kilichofichwa nchini Uswisi ni kikubwa zaidi ya hicho kilichotajwa.
Bunge liliipa Serikali kipindi cha mwaka mmoja
ambacho kinaishia Oktoba mwaka huu, iwe imekamilisha uchunguzi na
kuwasilisha ripoti hiyo bungeni.