Matokeo mabaya ya kidato cha nne ya mwaka 2012, yameendelea
kuitikisa sekta ya elimu nchini baada ya shule kufunguliwa jana bila
kutangazwa kwa waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano mwaka huu.
Kwa kawaida, wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na
kidato cha tano na vyuo vya ualimu, hutangazwa mapema ili kutoa fursa
kwa wanafunzi na shule husika kufanya maandalizi ya mahitaji.
Lakini tofauti na ilivyozoeleka, wanafunzi wa
kidato cha sita walianza masomo yao jana huku wale wanaotarajiwa
kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ualimu wakiwa hawajatangazwa.
Mkanganyiko huo pia unazigusa shule za sekondari
za binafsi kwani baadhi zilishachukua wanafunzi wa kidato cha tano na
nyingine ziliahirishwa kufunguliwa jana kutokana na kutokuwa na
wanafunzi hao.
Hali hiyo imewaacha njia panda baadhi ya wakuu wa
shule ambao waliwaambia waandishi wetu kwa nyakati tofauti kwamba
wanasubiri maelekezo ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhusu
suala hilo, huku wengine wakitishia kufunga shule hizo na kuzigeuza kuwa
vyuo vya taaluma nyingine.
Akitangaza matokeo mapya ya kidato cha nne Mei
mwaka huu, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa
aliahidi kwamba majina ya watakaojiunga na kidato cha tano yangetangazwa
mapema ili wapate muda wa kujiandaa na kuripoti kwenye shule husika
mapema kadri itakavyowezekana.
Jana, Dk Kawambwa hakupatikana kuzungumzia suala
hilo na msemaji wa Wizara hiyo, Bunyanzu Ntambi alisema suala la
kutangaza majina hayo lipo kwenye ngazi za uamuzi.
“Sababu hasa siwezi kujua, lakini kwa kuwa matokeo
yenyewe yalichelewa kutangazwa ni rahisi hata mchakato wa kutangaza
waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano uchelewe,” alisema Bunyanzu.
Wakuu wa shule
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Morogoro, Thomas Chihwalo alisema: “Ninachosubiri ni maelekezo ya wizara, nini kifanyike.”
Mkuu wa Sekondari ya Azania, Dar es Salaam, Benard
Ngoyaye alipoulizwa alisema: “Nenda kwa Ofisa Elimu wa Wilaya, yeye
anafahamu kwa nini majina yamechelewa kufika wakati
walikwishachaguliwa.” Mkuu wa Shule ya Sekondari Arusha, Christopher
Malamusha alisema walitarajia wizara ingetangaza majina hayo mapema
lakini hadi jana walikuwa hawajapokea taarifa zozote.
Mkuu wa Sekondari ya Tambaza aliyejitambulisha kwa
jina moja, Zuberi naye alisema wanasubiri maelekezo ya Ofisa Elimu
Wilaya ya Ilala.
Hata hivyo, Ofisa Elimu ya Sekondari wa Manispaa ya Ilala,
Germana Mng’aho alisema asingeweza kuzungumzia suala hilo na kwamba
mhusika mkuu ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Mkuu wa Shule ya
Sekondari ya Ilboru, Arusha, Julius Shula alisema hata majina ya
wanafunzi wanaojiunga na shule yao hawayafahamu.
Mmoja wa walimu wa Shule ya Sekondari ya Jangwani,
Dar es Salaam, alisema kwa kawaida wanafunzi wa kidato cha tano
huripoti shuleni wiki mbili kabla ya wale wa kidato cha sita kitu
ambacho mwaka huu kimekuwa tofauti. Msaidizi wa Mkuu wa Shule ya
Sekondari Bwiru Wavulana ya Mwanza, Malongo Charles alisema wanasubiri
wanafunzi watakaopelekwa na Serikali.
Hata hivyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Moshi, Fanuel Angalo alisema anaamini wizara husika itatangaza wiki hii.
“Ni jambo jipya kidogo limetokea lakini tunaamini
Waziri atatoa tangazo lake wiki hii halafu wanafunzi hao wa kidato cha
tano waripoti shuleni wiki ijayo,” alisema Angalo.
Mkoani Tanga, walimu katika Shule za Sekondari za
Tanga Ufundi, Gallanos na Usagara kwa nyakati tofauti, waliilalamikia
wizara kwa kuwachelewa kuwapelekea wanafunzi wa kidato cha tano na
kusema kuwa hiyo imevuruga utaratibu wa ufundishaji.
Hakuna athari
Baadhi ya wadau wa elimu walisema kilichotokea si
kigeni kwani kimepata kutokea miaka ya nyuma na mihula ilirekebishwa na
kwenda sawa na wenzao ambao walikuwa wameanza masomo.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Ushauri wa
HakiElimu, Nyanda Shuli alisema kubadilika kwa muhula wa kuanza masomo
si jambo kubwa ambalo linaweza kuathiri elimu na kwamba anaamini wizara
itakuwa imetoa mwongozo.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam
(UDSM), Dk Kitila Mkumbo alisema si mara ya kwanza kwa muhula wa masomo
kubadilika kwani imewahi kutokea siku za nyuma na marekebisho yakafanywa
ili kufidia muda ambao wanafunzi wanakuwa wamepishana na wenzao.
“Sidhani kama ni jambo kubwa sana ambalo linaweza
kuathiri chochote katika masuala ya elimu, la msingi ni kuhakikisha kuwa
waliochelewa kuanza masomo wanapata muda wa kumaliza mtaala (mtalaa) wa
masomo kama inavyotakiwa.”
Kwa siku tatu mfululizo, kuanzia Juni 29, mwaka
huu, wakuu wa shule za sekondari za Serikali walikutana katika Chuo cha
Ufundi, Arusha kupitia majina ya waliochaguliwa na kuiachia kamati ya
kukamilisha kazi hiyo.
Hata hivyo, habari kutoka ndani ya kikao hicho
zinasema tatizo kubwa lilikuwa ni idadi ya wanafunzi kuwa ndogo
ikilinganishwa na nafasi za kidato cha tano kutokana na kufeli kwa
wanafunzi wengi katika matokeo ya kidato cha nne, 2012.