*Rasimu kutumika kuwaondolea sifa ya kugombea urais
*Yumo pia Membe, Magufuli, Sitta, Zitto na Wassira
MKAKATI
wa kuwaengua vigogo wanaotajwa kung’ang’ania kugombea nafasi ya Urais
katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 sasa umebainika, MTANZANIA Jumapili
linaripoti.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti
hili, mkakati huo ambao umelenga kuwang’oa viongozi hao, unadaiwa
kutekelezwa na baadhi ya wanasiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kupitia Rasimu ya Katiba Mpya, iliyotolewa hivi karibuni na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
Imeelezwa
kuwa kupitia Rasimu hiyo ya Katiba Mpya, kuna vipengele vilivyopenyezwa
kwa nia ya kuwabana watu fulani fulani ndani na nje ya CCM ambao
wanatajwa kuusaka ukuu wa dola mwaka 2015 na chama hicho hakitaki kuona
wanakuwa kikwazo dhidi yake.
Mtoa habari wetu ndani ya CCM alilidokeza gazeti hili kuwa vipengele
hivyo ambavyo vimewekwa kama mtego, ni vile vinavyotaja sifa za mgombea
Urais na mgombea Ubunge.
Kwa
mujibu wa taarifa zilizotufikia, kutokana na hilo, baadhi ya wanasiasa
ndani ya CCM kwa makusudi wameamua kuufanya mjadala kuhusu serikali tatu
kuwa mkali, ili kuzuia mjadala mpana katika masuala mengine.
Kipengele
ambacho kama kikiachwa bila kufanyiwa marekebisho kinaweza kuwabana
wanasiasa wengi ndani na nje ya CCM wanaotajwa kuwania Urais 2015 ni
pamoja na kile cha Sura ya Saba, ambacho kinazungumzia Serikali ya
Jamhuri ya Muungano kuhusu Serikali, Rais na Makamu wa Rais, katika
sehemu ya kwanza C kwenye kipengele cha 75 (E) kinachozungumzia sifa za
Rais kimeeleza kuwa mtu atakuwa na sifa ya kuchaguliwa kushika nafasi ya
madaraka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano ikiwa: anazo sifa za kumwezesha
kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Katiba hiyo.
Wakati ikiwa hivyo katika sifa za kuwania nafasi ya Rais, kwenye
Rasimu hiyohiyo kipengele cha sifa za kuwania nafasi ya Ubunge kilichopo
katika sura ya tisa, sehemu ya pili (A) inayozungumzia kuhusu uchaguzi
wa wabunge, katika kipengele cha (2a) kimeeleza kuwa mtu hatakuwa na
sifa za kugombea/ kuchaguliwa kuwa Mbunge ikiwa mtu huyo aliwahi kuwa
Mbunge kwa vipindi vitatu vya miaka mitano.
Kutokana na hilo, ni
wazi kuwa viongozi au vigogo waliowahi kuwa wabunge kwa vipindi zaidi ya
vitatu vya miaka mitano hawatakuwa na sifa za kugombea Urais kwa sababu
tayari kipengele cha sifa za kuwania Urais kimetaja kuzingatia sifa za
mgombea ubunge.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti
hili, umebaini kuwa vigogo karibu wote ndani na nje ya CCM wanaotajwa
kutaka kuwania nafasi ya Urais watakuwa wamepoteza sifa za kuwania
nafasi hiyo endapo kipengele hicho kitaachwa bila kufanyiwa mabadiliko.
Vigogo
hao wanaotajwa kutoka CCM ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta,
Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli,
Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine ni Waziri wa
Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi na Naibu Waziri wa Sayansi na
Teknolojia, Januari Makamba, wakati kutoka Chadema ni Mbunge wa Hai,
Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willbroad Slaa na Zitto
Kabwe.
Source:Mtanzania