*Mandla amtuhumu Mbuso kuzaa na mkewe
CHIFU
Zwelivelile Mandlesizwe Dilubhunga ‘Mandla’ Mandela (39), ambaye ni
mjukuu mkubwa wa kiume wa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela,
amemtuhumu mdogo wake, Mbuso Mandela (22) kuwa alikuwa na uhusiano wa
kimapenzi na mkewe.
Tuhuma hizo nzito ndani ya familia ya Mandela, zimeibuliwa na Mandla
kwa kumtaja jina moja kwa moja Mbuso kuwa alikuwa na uhusiano wa
kimapenzi na mke wake wa pili, Anais Grimaud, ambaye alimpa ujauzito.
Mandla na Mbuso ni watoto wa Marehemu Makgatho Mandela ambaye ni mtoto
wa kiume wa Mandela kwa mkewe wa kwanza, Marehemu Evelyne Maso.
Watu
walio karibu na familia ya Mandela, wamepata kukaririwa na vyombo vya
habari vya nchini hapa wakieleza kuwa, Mandla amekuwa akilalamika mara
nyingi kuwa mke wake ambaye wameshatalikiana, alikuwa na uhusiano wa
kimapenzi na mmoja wa ndugu zake, lakini hakuwahi kumtaja kwa jina.
Katika malalamiko yake hayo, Mandla alikaririwa akieleza kuwa, ndugu
yake alimpa mimba mke wake na kuzaa naye mtoto mmoja jambo ambalo
wanafamilia wamelifumbia macho wakati wanajua alitendewa vibaya.
Alhamisi
wiki iliyopita, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari huko
Mvezo, Eastern Cape, baada ya kushindwa kesi aliyokuwa amefunguliwa na
shangazi yake, Makaziwe Mandela ya kuvamia eneo la makaburi usiku na
kuiba mabaki ya miili ya watoto watatu wa Mandela, Mandla alisema
anashangazwa na watu wanaojiita wanafamilia ya Mandela kudai wanataka
amani ndani ya ukoo wakati malalamiko yake hawajawahi kuyashughulikia.
Katika
mkutano wake huo, Mandla alisema mke wake aliyemuita ni mzuri, Anais,
ambaye ni raia wa Ufaransa, alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mdogo
wake wa damu aliyemtaja jina kwa mara ya kwanza, kuwa ni Mbuso.
Alisema
kwamba, alipopata taarifa hizo, alishtuka na kuumia na alimtaja mtoto
ambaye mke wake alizaa na mdogo wake Mbuso kuwa anaitwa Nkosi Qheya II
Zanethemba Mandela.
Mandla alisema alilazimika kuachana na mkewe
huyo aliyemuoa mwaka 2010 na kwamba aliamua kumbadili jina mtoto
aliyezaa na Mbuso na kumuita Nkosikazi Nobubule, kabla hajaondoka kwenye
makazi ya Mandla na kurejea kwao Ufaransa.
Tuhuma hizi
zilizotolewa na Mandla juzi kwa mara ya kwanza, ziliripotiwa na Gazeti
la Sunday Sun la Afrika Kusini mwaka jana na kuibuka tena wiki
iliyopita.
Taarifa hizo, zimezidi kuipa nguvu hofu ya baadhi ya
watu wanaofuatilia mtafaruku wa ndani ya familia ya Mandela ambaye kwa
sasa anapigania uhai akiwa hospitalini.
Kwa zaidi ya wiki mbili
sasa, familia ya Mandela imekuwa katika mnyukano wa kugombea uhalali wa
eneo linalostahili kuwa maalumu kwa ajili ya kuzika marehemu wa familia
hiyo baada ya Mandla kuhamisha mabaki ya miili ya watoto watatu wa
Mandela, waliokuwa wamezikwa katika nyumba yake iliyoko kijijini Qunu na
kwenda kuwazika kwenye makazi yake ya kichifu ya Mzove.
Mahakama
Kuu ya Mthatha ya Jimbo la Eastern Cape ilimtia hatiani Mandla
aliyekuwa akishitakiwa na wanafamilia 16, ambapo ilimuamuru arejeshe
mabaki ya miili hiyo Qunu.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa familia
yake, Mandela bado yuko mahututi hospitali mjini Pretoria na hakuna
taariza zozote za mabadiliko ya afya yake.