*Mandla Mandela aendelea kulikoroga
WAKATI mgogoro kati ya watoto wa Mandela na wajukuu ukizidi kutokota kuhusu uhalali wa uchifu wa Mandla Mandela, yeye amejibu mapigo akisema Mfalme Buyelekhaya Dalindyebo wa kabila la abaThembu ”hana akili timamu”.
Hiyo inatokana na madai yaliyotolewa na mfalme huyo kwamba Mandla hakuwa chifu sahihi wa ukoo wa Madiba. Alidai kwamba hakukuwa na cheti chochote halali kilichotiwa saini wakati mandla alipotawazwa kuwa chifu mwaka 2007 – sherehe ambazo zilisimamiwa na Mandela mwenyewe.
Gazeti la Mail & Guardian wiki iliyopita liliripoti kuwa uchifu wa Mandla ulilalamikiwa kabla ya Mandela kulazwa hospitalini, ikielezwa kama kweli anafaa kuendelea kuwa chofu ikizingatiwa kuwa mama na baba yake walimzaa bila kuoana.
Mgogoro unaoendelea hivi sasa kati ya Manla na shangazio yake, Makaziwe Mandela, na wanafamilia wengine unaonekana kama kichocheo kwa baadhi ya wanafamilia hiyo ambao wangetaka Mandla avuliwe uchifu.
Jumamosi iliyopita, Dalindyebo alisema hawezi kumheshimu mtu “ambaye haheshimu familia yake” na kusema Ndaba ambaye ni mdogo wake Mandla ndiye anastahili kuwa chifu.
Lakini juzi, Mandla alijibu mapigo kupitia kwa msemaji wake, Freddy Pilusa akisema: “Tamko lililotolewa na Mfalme Dalindyebo kwamba amemuondolea Mandla madaraka yake ya kimila ni kichekesho.
“Ni mchakato mrefu wa kimila kumuondoa chifu. Huwezi kuamka tu asubuhi na kuitisha mkutano wa wafuasi wako na kuchukua uamuzi mzito kama huo,” alisema Pilusa.