*Aelezea uhusiano wake na Mwigulu, Lwakatare
*Asema yeye bado ni mwanachama hai wa Chadema, amkwepa Kibanda
SIKU chache baada ya Mahakama kumuachia kwa dhamana mshitakiwa
mwenza wa Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare, Joseph Ludovick, amefunguka na
kuelezea tuhuma ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake, ikiwamo uhusiano
wake na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Nchemba.
Ludovick, ambaye anadaiwa kurubuniwa na Nchemba na hivyo kumrekodi
Lwakatare wakipanga mipango ya kumdhuru Mhariri Mtendaji wa gazeti la
Mwananchi, Denis Msaky, alijitokeza juzi katika mtandao wa kijamii wa
Mabadiliko na kuomba kuulizwa jambo lolote, kwa kile kilichoonekana
kutaka kujibu tuhuma ambazo zimekuwa zikielekezwa dhidi yake.
Maswali na majibu yake ilikuwa ni kama ifuatavyo;
KUHUSU UHUSIANO WAKE NA MWIGULU
Akielezea uhusiano wake na Mwigulu baada ya kuulizwa swali na mtu
aliyejitambulisha kwa jina la Abdul Dello, Ludovick alisema ni wa
kawaida na kwamba haufikii kama ule wa Lwakatare na Maggid Mjengwa.
“Tumejuana kwenye mitandao ya kijamii na tukadevelop ukaribu, ilitokana na mimi kukosoa mijadala yake na kumpinga.
“Ninayo mahusiano na watu wengi tu nje ya Chadema. Mfano ni huyo
Mwigullu, Sixtus Mapunda, Mbunge Kangi Lugora, nk.na sidhani kama ni
dhambi hii. Wapo wengi tu wenye uhusiano kama huu. Wote hawa katika
nyakati tofauti tumesaidiana mengi.
Katika swali lake lingine, Abdul Dello alihoji: “Ludo, Mwigulu Nchemba
alithibitika kukutumia m-pesa ya elfu 50 ilikuwa ya kazi gani?
Ludovick alijibu akieleza kuwa: “Nilikuwa na tatizo binafsi la kifamilia, nilihitaji msaada.”
KUHUSISHWA NA USALAMA WA TAIFA
Mtu mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Hamis Hamad alimuuliza akisema:
“Ludo, unasemwa sana mtaani kuwa wewe ni TISS Agent (wakala wa usalama
wa taifa) uliyepachikwa pale Chadema kwa ajili ya kuiua kifo cha kawaida
na ndiyo maana unafanya kazi nyingi za kujitolea badala ya kwenda
kufundisha kama taaluma yako ya ualimu inavyokuruhusu, kweli?
Majibu ya Ludovick yalikuwa hivi: “Nchi hii tunapenda majungu tuuu, na
magazeti yetu yamebobea kusambaza majungu na kupakazia watu. Huwezi
kuelewa dhana hii hadi ikukute. Juu ya kazi ni tofauti za kimtazamo, so
wengine wanapenda kuajiriwa na wengine hawapendi, so haicount hii. Ni
uamuzi tu. Niliijua Chadema 2006 na kujiunga rasmi 2009. Hakuna
aliyenipachika huko. Ni by conviction, nakuhakikishia hata matatizo yote
ninayoyapata ni kwa sababu ya Chadema.”
AELEZA ANAVYOMFAHAMU LWAKATARE
Boniface Magessa alimuuliza hivi: “Ludovick, elezea kidogo unavyomfahamu
Lwakatare. Siku ya tukio la kurekodiwa ulikuwa wapi? Kama mlikuwa wote
siku hiyo, ulikaa mbele yake au nyuma yake?
Ludovick: “Magessa, Lwakatare tumekutana Bukoba 2010 wakati wa kampeni.
Tumefahamiana kwa sababu ya Chadema tu. Na ameendelea kuwa rafiki yangu
na kiongozi wangu.
Siku ya tukio la kurekodiwa nilikuwa nyumbani kwake Lwakatare. Siyo muhimu juu ya location”.
MASWALI MENGINE
Leila Sheikh alimuuliza hivi; “Ludo, eti uliwahi kuruka ukuta usiku fulani?
Ludovick: “Da Leilah umefunga wewe? Sasa haya ya kuruka ukuta usiku
fulani ni nini tena? Teh teh, hebu fafanua? Marcois, siku hizi kibwagizo
changu ni kuwa natazama yote haya nayo ni ubatili mtupu, ni sawa na
kufukuza upepo”.
Swali lake lingine lilisomeka hivi: “Kama wewe ni mwanachama hai wa
Chadema kwa nini umeitwa 'msaliti' na shabiki wa Chadema kuwa ile kanda
ya Lwakatare ulitumwa na Mwigulu kuipiga? Je, ile kanda ni ya kweli?
Inadaiwa kuwa ile kanda inaonesha nia/mpango wa kumuumiza Msacky.
Katika majibu yake Ludovick naye alijibu “Leila, mimi ni Mwanachadema
hai. Kuitwa msaliti ni hali halisi ya sasa. Lakini inawezekana kuwa mimi
wanayeniita msaliti, siku moja wakaona kuwa ndiye mwokozi. Fikiria kama
ningekuwa natumika kama mnavyosema, kwa nini kesi ya ugaidi imefutwa?
Si ningesema tu kuwa kulikuwa na watu wengine kadhaa? Kama ninatumika,
kwa nini nikamatwe Iringa na kusafirishwa usiku tena chini ya ulinzi
mkali? Leila teh teh kwamba nilitumwa kurekodi ile kanda!!! Yaani na
Lwakatare naye akatumwa ili aongee haya tunayotuhumiwa kuyapanga? Na je,
suala hili ikionekana kuwa ni kweli Lwakatare alilifanya, nani atakuwa
msaliti kwa Chadema? Je, chama chetu kinazo sera za kudhuru waandishi?
Sasa msaliti ni yule anayechafua chama kwa kupanga mambo yasiyoendana na
sera za chama? Au ni yule anaye kilinda chama? Haya si nyote mnajua
concept ya whistle blowers? Hamtegemei wawemo ndani ya Chadema?
Na je, kama Mahakama itaamua kuwa tuhuma zetu ni kweli bila chembe ya
shaka, ninyi mtaendelea kusema nini, kuwa mimi msaliti au wote sasa
tutakuwa wasaliti? Naomba tuachie mahakama suala hili. Kuitwa msaliti
wakati unaumia kwa ajili ya hao wanaokuita wasaliti, kibinadamu inaumiza
sana. Na hilo ndilo linanitokea.
Kuhusu kwa nini watu wote wananilaumu, si kweli. Wapo wasioona hivyo,
ila in a great party propaganda chafu za CCM na za Chadema zimenifanya
muhanga wa mambo haya. Uhusiano wangu na Lwakatare kwa sasa ni wa
mashaka sana.
Swali jingine la Sheila ni hili: “Je, wewe bado mwanachama wa Chadema?
Kama ndiyo, mbona walikutema kwa muda ukakaa rumande bila dhamana? Kwa
nini wewe ambaye ni volunteer wa Chadema ulikanwa pale baada ya
kushikiliwa na polisi? Huo ndiyo u****wa kafara.
Alijibu hivi: “Mimi ni mwanachama wa Chadema na nakuhakikishia mateso yote ninayoyapata ni kwa sababu ya Chadema.
Masharti ya dhamana hayakuwa wadhamini wawekwe na Chadema, bali watu
wawili. Sasa sidhani kama Chadema walikuwa na kesi mahakamani hadi
watafute wadhamini. Kuhusu kuwa volunteer wa Chadema ni majungu
niliyoyazungumza. Sijawahi kuwa volunteer wa Chadema. Mimi ni mwanachama
wa kawaida.
Nyoni Magoha alimuuliza hivi: “Wewe bado una imani na Chadema? Utaendelea kuwa mwanachama hai au umeshajitoa/utajitoa?
Majibu ya Ludovick: “Ninayo imani kubwa sana na isiyotetereka kwa Chadema. Nitaendelea kuwa mwanachama hai”.
Hata hivyo, Ludovick ambaye anatajwa kuhusika na tukio la kutekwa na
kujeruhiwa kwa Mhariri Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Ltd, Absalom
Kibanda, alikwepa kuzungumzia jambo hilo na hata alipoulizwa baadhi ya
maswali yenye mwelekeo huo.
Kuhusishwa Ludovick na tukio la Kibanda kunatokana na utata wa kauli na
mwenendo wake siku ambayo Mhariri Mtendaji huyo alijeruhiwa.