*Ni baada ya kusakwa siku kadhaa
*Ahojiwa kwa tuhuma za uchochezi
MWENYEKITI
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe
amejisalimisha polisi. Mbowe, alijisalimisha polisi jana saa 8.00 mchana
makao makuu ya Polisi Dar es Salaam na kuhojiwa na kikosi maalumu cha
makachero wa jeshi hilo.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Katibu
Mkuu wa Chadema, Dk. Willbrod Slaa, alithibitisha Mbowe kujisalimisha
polisi akiwa amefuatana na mwanasheria, Nyaronyo Kicheere.
“Si
kweli kwamba Mbowe amekamatwa, amekwenda polisi mwenyewe. Kama
nilivyoeleza kwenye mkutano wetu pale Manzese juzi…Polisi walikwenda
nyumbani kwake Mikocheni usiku kwa ajili ya kumkamata hawakufanikiwa.
“Siwezi kusema anahojiwa au vipi, bali ameenda huko kama tulivyokubaliana,” alisema Dk. Slaa.
Hatua
ya Mbowe kujisalimisha imetokana na tarifa kuwa polisi walivamia
nyumbani kwake saa 6.00 usiku Ijumaa iliyopita kwa lengo la kumkamata.
Chanzo cha kuaminika kutoka makao makuu ya polisi, kilisema Mbowe
alihojiwa kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo za uchochezi anaoufanya kwa
kujenga chuki kati ya wananchi na polisi.
Chanzo hicho kilisema
tuhuma nyingine ni kauli yake aliyowahi kuitoa kuwa polisi inahusika
katika tukio la mlipuko wa bomu uliotokea Juni 15 mwaka huu CHADEMA
walipokuwa wakihitimisha mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo kwenye
viwanja vya Soweto mjini Arusha.
Katika tukio hilo,watu wanne walikufa na wengine kadhaa kujeruhiwa vibaya katika tukio hilo.
Katika
tukio hilo,Mbowe alidai Chadema kina ushahidi wa kutosha kuwa polisi
wanahusika na tukio hilo kutokana na kuwa na mkanda wa video unaoonyesha
tukio zima.
Lengo la kufanya hivyo linadaiwa kuwa ni
kukidhoofisha chama hicho na kukisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika
uchaguzi wa madiwani Arusha.
Tuhuma nyingine ambayo Mbowe
alihojiwa ni kuhusiana na kauli yake kuwa kitendo cha Rais Jakaya
Kikwete kutohudhuria mazishi ya watu waliofariki dunia katika mlipuko
huo,kilihusishwa moja kwa moja kuwa ni ishara ya jeshi hilo kuhusika
katika mauaji hayo.
Habari zaidi zinasema Mbowe anatuhumiwa
kulichafua Jeshi la Polisi la Tanzania kwa kile alichodai ni moja ya
jeshi katili Afrika Mashariki.
Chanzo chetu kilisema tuhuma
nyingine ni uchochezi anaoufanya kuhusiana na kauli ya Waziri Mkuu
Mizengo Pinda aliyoitoa bungeni hivi karibuni.
Katika kauli hiyo, Pinda alisema alilielekeza jeshi la polisi kuwashughulikia watu wasiotii sheria.
Source:Mtanzania