KUMBE MAFUTA YA UBUYU NI SALAMA

TAASISI ya Saratani ya Ocean Road ya jijini Dar es Salaam, imesema mafuta ya ubuyu hayana madhara yoyote katika mwili wa binadamu kama yakitumiwa vizuri. Imesema kwamba, hadi sasa, hakuna tafiti zozote za kitaalamu zilizowahi kufanywa na kuonyesha mafuta hayo ni chanzo cha saratani ya ini.

Taarifa hiyo imetolewa jana na Daktari Bingwa wa Udhibiti wa Saratani, katika taasisi hiyo, Dk. Crispin Kahesa, alipokuwa akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu.

“Mafuta ya ubuyu siyo dawa bali yanazuia maradhi sugu yasiyoambukiza, yakiwamo saratani kwa sababu kitaalamu yana ‘ant oxidant’ (uchachu) ambao pia hupatikana kwenye baadhi ya matunda kama maembe, machungwa na mananasi.

“Tofauti iliyopo ni kwamba, mafuta hayo yana ant oxidant nyingi tofauti na iliyomo kwenye matunda. Ant oxidant husaidia kukinga maradhi mbalimbali ambayo mengi si ya kuambukiza, yaani maradhi sugu kama vile kansa, kisukari na shinikizo la damu,” alisema Dk. Kahesa.

Kazi nyingine ya ant oxidant mwilini aliitaja kuwa ni kuondoa sumu na kusaidia kutengeneza chembechembe hai mwilini.

“Kwa maana hiyo, ninachoweza kusema ni kwamba, dawa yoyote isipotumika vizuri na kwa kiwango kinachohitajika kwa mgonjwa, inaweza kumwathiri mgonjwa.

“Sukari au chumvi ikizidi, inaleta madhara, yaani hata dozi ya saratani isipotumika vizuri ina madhara.

“Narudia tena, mafuta ya ubuyu hayana madhara kama yakitumika vizuri, bali madhara ambayo watu wanayasema, yanatokana na jinsi wanavyoyatumia mafuta hayo, kwani wajasiriamali wanaoyatoa hawajui ni mgonjwa gani anapaswa kuyatumia na kwa wakati gani.

“Tatizo jingine ni katika maandalizi yake, kwa sababu haijulikani yanaandaliwa katika mazingira gani,” alisema.

Akielezea uwezo wa mafuta hayo kutibu ngozi ya albino, alisema hayana uwezo wa kuzuia mionzi ya jua isipenye katika ngozi hiyo.

Kutokana na hali hiyo, alisema albino hawatakiwi kuyatumia kwani yanaongeza madhara katika ngozi zao.

Dk. Kahesa alizishauri taasisi zinazohusika na udhibiti wa matumizi ya bidhaa mbalimbali, kufanya uchunguzi wa kina kabla bidhaa hazijasambaa kwa walaji.

Pia, alisema kuna haja, jamii kuwa na uelewa wa matumizi ya dawa ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea baada ya kuzitumia.

Matumizi ya mafuta ya ubuyu yameleta utata hivi karibuni, baada ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), kusema yanaweza kusababisha saratani ya ini.

Kwa mujibu wa TFDA, mafuta hayo yana kiwango kikubwa cha tindikali ya mafuta aina ya ‘cyclopropenoic fatty’, ambayo huweza kuathiri afya pindi yanapotumika kama chakula.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad