KIKOSI
cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, maarufu kama Taifa Stars juzi
kilipoteza mechi yake ya kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika kwa
Wachezaji wa Ndani (CHAN) kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Uganda, The
Cranes kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kabla
ya mchezo huo, matarajio ya wengi yalikuwa ni Taifa Stars kuibuka na
ushindi kutokana na muonekano wa mechi yenyewe na rekodi ya Taifa Stars
kwa siku za hivi karibuni. Sasa matumaini ya Taifa Stars kucheza CHAN ni
madogo mno kulinganisha na hali ilivyokuwa hapo awali.
Hii
ina maana, Taifa Stars inatakiwa kupata ushindi usiopunguwa bao 1-0
kwenye mechi ya marudiano itakayochezwa wiki mbili zijazo kwenye Uwanja
wa Namboole huko Uganda.
Mengi
yalitokea katika mchezo wa jana, ambao uliwatoa vichwa chini Watanzania
wengi waliodhani timu yao ingeweza kufanya vizuri baada ya hivi
karibuni kuwa na matokeo ya kuridhisha.
TAIFA STARS ILIWAKOSA WAWILI, UGANDA ILIWAKOSA KUMI….LAKINI BADO MAMBO YAKAWA MAGUMU KWAO
Taifa Stars iliingia uwanjani ikiwa imewakosa wachezaji wake wawili tu wa kikosi cha kwanza kutokana na kanuni kuwabana, nao ni Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaochezea TP Mazembe ya DR Congo.
Samatta
na Ulimwengu hawakuweza kucheza mechi hiyo kutokana na ukweli kwamba,
hiyo ni michuano maalum kwa wachezaji wa ligi za ndani ya nchi pekee.
Shirikisho
la Soka Afrika, CAF lilianzisha michuano hii ili kutoa fursa kwa
wachezaji wanaoshiriki ligi za ndani za nchi zao nao kuonekana na kutoa
michango yao kwa timu zao za taifa ambazo mara nyingi zilikuwa
zikisheheni wachezaji wanaocheza nje ya Afrika.
Wachezaji
wanaocheza ligi za ndani katika nchi kama Nigeria, Ivory Coast na
Senegal, huwa hawapati nafasi ya kucheza michuano ya aina yoyote katika
vikosi vya nchi hizo ambavyo husheheni idadi kubwa ya wachezaji
wanaocheza soka la kulipwa nje ya Afrika hasa Ulaya.
Kwa
kutambua hilo, CAF ikaamua kuanzisha michuano hii ya CHAN ambayo
Tanzania imeshiriki mara moja na Uganda pia imeshiriki mara moja. Kwa
kutaka michuano hii ichezwe na timu kutoka pande zote za Afrika, CAF
ikawa inahakikisha kila pembe ya Afrika inashiriki michuano hii, ndiyo
maana leo Tanzania na Uganda zinawania nafasi ya kufuzu kucheza fainali
hizo.
Wakati
Taifa Stars ikiwakosa wachezaji wawili tu, Uganda iliwakosa wachezaji
kumi (10) ambao mara nyingi huwamo katika kikosi cha kwanza cha timu
hiyo. Hii ina maanisha Uganda ilikuwa na wachezaji wawili tu wa kikosi
cha kwanza kinachojumuhisha hata nyota wanaocheza nje ya Uganda.
Wachezaji
wa Uganda waliocheza mechi ya jana ambao mara nyingi huchezea timu ya
taifa ni Hamza Muwonge na Hassan Waswa ambaye jana alikuwa nahodha.
Wengine wote waliocheza jana, huwa hawana nafasi katika kikosi cha
Uganda. Kazi ipo.
TANZANIA LIGI DUNI, UGANDA LIGI BORA….
Kwa matokeo ya mechi ya jana, imedhihirika wazi kwamba Ligi Kuu ya Tanzania Bara, haina ubora kulingana na ile ya Uganda. Wachezaji wengi wa Taifa Stars hawakuweza kucheza vizuri mbele ya wenzao wa Uganda walioweza kutawala na kucheza kwa malengo katika eneo la kiungo kwa muda mwingi.
Kabla
ya mchezo ilionekana wachezaji wa Tanzania wangeweza kuwapiku wa Uganda
lakini muda mfupi baada ya mchezo kuanza, ubora wa wachezaji wa Uganda
ulikuwa ukitawala kila mara. Viungo kama Salum Aboubakar ‘Sure Boy’,
Frank Domayo, Amri Kiemba, Mrisho Ngassa na Mwinyi Kazimoto hawakuweza
kuwa imara na kuisaidia timu.
Bado
wachezaji hao wanacheza na majukwaa huku wakipoteza malengo ya timu
mara kwa mara hasa kwa kukariri mfumo wa kucheza pasi za nyuma wakati
timu ikipanda, na hata uanzishwaji wa mipira mara nyingi umekuwa ule
ule, kwamba mpira anaanziwa Aggrey Morris au Kelvin Yondani halafu
utaenda kwa Erasto Nyoni, naye ataupeleka kwa Sure Boy halafu Sure Boy
anaupeleka kwa Shomari Kapombe au unarudi tena kwa Morris ambaye
ataupiga juu katikati halafu John Bocco atashindana nguvu na mabeki wa
Uganda kisha anaupoteza halafu kazi ya kukaba inaanza.
Kwa mchezo wa jana wa Taifa Stars, hakika kila siku tutalia kama hatutakubali kufuata yafuatayo;
KUREKEBISHA MFUMO WA SOKA TANZANIA…
Timu
zote tunazocheza nazo kisha zikatufunga, ukizitazama utagundua zina
mfumo wa kuopoa vipaji vya wachezaji wake, hasa kuanzia ngazi ya shule
za msingi, sekondari hata katika vyuo vikuu.
Mtazame
mfungaji wa bao pekee la Uganda, Dennis Guma huyu anatokea timu ya
Victoria University ambayo pia inashiriki Ligi Kuu ya Uganda. Timu hii
ina timu kibao za watoto wadogo ambao wanapitia katika mfumo mzuri wa
soka na hata kupata elimu ya dunia kwa pamoja.
Leo
hii wachezaji wengi kutoka Kenya au Uganda mpaka wanapofikia hatua ya
kucheza Ligi Kuu wengi wao ni agharabu kuwakuta na elimu chini ya kidato
cha nne au kidato cha sita kutokana na mfumo wao wa elimu dunia na ile
ya michezo hasa soka. Siwakosoi kwa kutokuwa na elimu, lakini utawasikia
wameshindwa kuendelea na elimu ya sekondari kutkana na matatizo ya
kifamilia.
Academy
nyingi za nchi hizo, zinawapa fursa wachezaji kupata elimu zote hizo
(soka na elimu ya darasani) kwa pamoja na ndiyo msingi wa mafanikio yao
leo hii. Hao wanakua kiakili huku wakijua namna ya kupokea mafundisho.
Hapa
kwetu leo hii kitazame kikosi cha Taifa Stars, kisha omba rekodi za
walipotokea wachezaji wake halafu uliza kuhusu elimu zao, utashangaa,
lakini ndiyo aina ya wachezaji tulionao. Tufanyeje? Hakuna jinsi.
Wachezaji
wengi wa Taifa Stars hawajulikani wanapotokea, unashtukia mtu anacheza
Simba, Yanga au Azam au hata timu nyingine ya ligi kuu bila hata ya
kucheza mechi moja ya ligi daraja la tatu au ile ligi ya taifa. Sasa
huyu atawezaje kupambana na mtu aliyepitia mfumo sahihi wa soka? Huu ni
utani.
Siyo
siri, Taifa Stars inaundwa na wachezaji wengi wa Simba, Yanga na Azam,
lakini ni Azam pekee yenye mfumo mzuri wa usajili wa wachezaji kwa kuwa
na academy yake inayozalisha wachezaji kila siku. Hizo Simba na Yanga
bado zina mfumo wa kuita lundo la wachezaji katika mazoezi yao na
kutazama uwezo wao kisha kuwasajili.
Sipo
hapa kuisifia timu fulani au kuiponda timu nyingine, natoa machungu
yangu ya rohoni kutokana kuumizwa na kipigo cha jana cha Taifa Stars
dhidi ya Uganda iliyoonekana kuwa dhaifu pengine kuliko hata kikosi cha
Taifa Stars.
KUKOSEKANA MAKOCHA WENYE UWEZO NALO NI TATIZO LETU…
Lazima
tukubali kwamba, Tanzania ina tatizo la makocha wenye uwezo wa
kufundisha hasa vijana wadogo. Hata kama leo hii serikali ya Tanzania
itakubali kubadili mtaala wa elimu yake na kuruhusu soka kuingia ndani
yake. Tunaweza kupata tatizo la ukosefu wa makocha.
Kuna
haja ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wadau wengine wa soka
kujitolea kuwafundisha makocha wa timu za watoto ili wawe wengi
watakaoweza kutoa elimu stahiki kwa watoto.
Leo
hii utazunguka mitaani na kukuta watoto wanafundishwa na kocha wao,
lakini ukimchungumza kocha huyo utagundua anafanya kazi hiyo kwa utashi
wake tena kwa kujitolea huku akikosa elimu hata ya msingi ya ukocha.
Hivi hapo unategemea kupata mchezaji bora? Hakuna.
Kozi
zinazotolewa na TFF lazima zitazame hali halisi ya uwezo wa mtanzania,
kwamba kozi inaletwa na kuwataka washiriki kuchangia kiasi cha fedha,
basi kisiwe kingi kiasi cha kuwafanya wengine kutomudu kulipia kwani
udhamini wakati mwingine unakuwa mgumu.
HITIMISHO…… NI LAZIMA TUFE ILI TUFIKE PEPONI…..!
Kwa
vyovyote vile, ni lazima mambo ya msingi yafanyike katika mfumo wa soka
la Tanzania ili kuiletea mafanikio nchi hii katika soka, nje hapo
tutakuwa tunaimba nyimbo zisizo na muitikiaji kila siku. Mafanikio
hayatakuja.
Lazima
TFF na klabu za soka za Tanzania zikubali kuendesha soka kitaalam na
siyo kibabaishaji kama ilivyo leo, pia ziwepo program zitakazokuwa
zinafanya kazi kikamilifu na siyo zipo zipo tu kama geresha.
SOURCE:SHAFII DAUDA
SOURCE:SHAFII DAUDA
mtaendelea kushika mikia! acheni siyo fani yenu mna lazimishwa
ReplyDelete