KWANINI KUNA KIGUGUMIZI MAPAMBANO ZIDI YA DAWA ZA KULEVYA TANZANIA?


Biashara ya dawa za kulevya inaonekana kushamiri nchini, huku kukiwa na maswali mengi juu ya akina nani hasa wahusika wa shughuli hii, hata inashindwa kukomeshwa.
Waliopewa mamlaka kuzuia dawa hizo nao wanahusika au hawana ujuzi, wafukuzwe?
Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wa makala hii, wana mashaka kwamba huenda baadhi ya vigogo au wafanyakazi waliopewa mamlaka kupambana na dawa nchini, wanahusika kufanya biashara hii au kuwasaidia wanaoifanya kwa manufaa yao, madai ambayo wamekuwa wakiyakanusha vikali.
Hata hivyo baadhi ya watu ambao wamewahi kuwa majambazi na kujihusisha na biashara haramu, akiwamo mchungaji mmoja kutoka Arusha ambaye amewahi kuwa jambazi kabla ya kuamua kuokoka na kumtumikia Mungu, anasema ni vigumu mno na huenda ni jambo lisilowezekana kufanikiwa kufanya mambo mabaya nchini kama ya ujambazi au dawa za kulevya na ukadumu katika kazi hiyo kama hauna mtandao na wale ambao wanahusika katika kuzuia vitendo hivyo.
“Kama una mawasiliano na wenye mamlaka utafanya biashara yoyote chafu, kama huna ni ngumu kutokamatwa, mimi nimewahi kuwa jambazi, ninaongea haya kwa uzoefu, sio kweli kwamba ulinzi nchini ni mbaya, bali kuna watumishi si waaminifu” anasema Mchungaji huyo.
Kwa uzoefu wake ni kuwa iko haja kwa viongozi walioko Serikalini kama kweli wana lengo la kupambana na dawa za kulevya, kwanza kuwachukulia hatua wote ambao waliwakagua na kuwaruhusu wahusika wa dawa wanaokamatwa kupita.
Ni kama hakuna lengo la kupambana na dawa za kulevya
“Kama mtu amepita uwanja wa ndege, inapaswa kujulikana alikaguliwa na nani? Wote waliohusika wakamatwe mara moja, waunganishwe kwenye kesi ya hizo dawa za kulevya, hii itaonyesha kweli Tanzania tuna lengo la kupambana na dawa za kulevya, lakini kinachofanyika sasa ni usanii wa mchana kweupe,” anasema Mchungaji huyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
Hatua kali kwa wauza dawa
Baadhi ya wananchi akiwamo Ameria Haule, mkazi wa Ubungo anashauri kutungwe sheria kali za kupambana na dawa za kulevya.
Aidha, Juma Hamisi wa Mtongaji, na Tuma Msongwa wa Manzese, Dar es Salaam wanasema pale ambapo mtu amekamatwa na aina yoyote ile ya dawa za kulevya, na kukawa na uthibitisho, kusiwe na haja ya kufanya upelelezi juu yake zaidi, badala yake hukumu itolewe mara moja. Hali kadhalika wakashauri dhamana iondolewe, wakisemabiashara hii ni sawa na mauaji.
Kituo cha daladala kwa Manyanya

Mojawapo ya vituo vya daladala ambavyo vinadaiwa kutumiwa kwa dawa za kulevya ni cha daladala cha Kinondoni kwa Manyanya,  kama unaelekea Posta ukitokea Kinondoni.
“Ni kawaida kuwaona vijana wakisinzia hapa kuanzia asubuhi hadi asubuhi, kama kweli wenye mamlaka wana lengo la kupambana na dawa, wangekuja hapa ikawasomba hawa wote wanaosinzia, kisha ikawapime ili kuona walicholewa kimetokana na nini…kuna madai kuwa hao ndio wauzaji wazuri wa rejareja hapa Kinondoni, hali kama hiyo iko pia vituo vingine vingi vya daladala, huenda ndio sababu kwanini inakuwa vigumu kupiga marufuku wapiga debe kuwepo, maana wauza dawa wanajichanganya na wapiga debe,” anasema mkazi mmoja wa eneo hilo ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini.
Ubungo darajani
Katika maeneo ya Ubungo kuna watu kadhaa wanahusika na dawa hizi; Kwa mfano yuko jamaa ambaye huzunguka usiku akisambaza dawa za kulevya kwa gari lake dogo. Hali ni mbaya zaidi eneo la Ubungo Maziwa, wapo hadi akina mama kadhaa kwenye vijiwe vya vijana wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Maeneo mengine ya Tanzania
Karibu nchi nzima, kuna kashfa hii ya kuwapo kwa dawa za kulevya, huku maswali makuu yakielekezwa kwa wana usalama nchini kama ni kweli hawaoni yanayoendelea.
Iundwe tume ya siri
Baadhi ya wananchi wanashauri kuundwe kikosi cha siri kuchunguza utendaji wa askari ili kutoa mashaka ambayo yanaonekana kuongezeka miongoni kwa jamii kuwa baadhi yao huenda wanashiriki katika biashara hii ya dawa mbalimbali za kulevya yakiwemo cocaine, mirungi na bangi.
Wanahoji ni kwanini Serikali ni kama inaonekana kushikwa na kigugumizi katika kupambana na tatizo hili la dawa za kulevya, licha ya idadi ya watumiaji ikionekana kuongezeka kadri siku zinavyokwenda mbele.
Wengine wakashauri Rais Kikwete kumaanisha katika kuchukua hatua na kuwachukulia hatua viongozi ambao wanaonekana wazi kutochukua hatua
Ahadi nyingi vitendo haba
Licha ya kuwapo madai mengi miezi ya hivi karibuni ikiwemo kwamba kuna viongozi wa dini wanahusika  na dawa za kulevya, wapo wabunge waliosema wanawajua wenye kufanya biashara hiyo, baadhi ya viongozi wakielezwa kuhusika.

Hali ya dawa za kulevya nchini
Kwa mujibu wa ripoti ya ofisi ya Waziri mkuu, Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya, tatizo la dawa za kulevya nchini limeendelea kukua licha ya jitihada mbalimbali zinazofanyika katika kupambana nalo.
Hali hii inadhihirishwa na kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kilichokamatwa hususan heroin na cocaine katika mwaka 2011 ikilinganishwa na mwaka 2012.
Takwimu zinaonyesha kuwa kilo 264.3 za heroin zilikamatwa mwaka 2011 ikilinganishwa na kilo 185.8 zilizokamatwa mwaka 2010. Takwimu hizi zinaonyesha.
Ongezeko la asilimia 42 la kiasi cha heroin kilichokamatwa katika kipindi cha mwaka mmoja tu. Aidha, mwaka 2011 kilo 126 za cocaine zilikamatwa ikilinganishwa na kilo 63 zilizokamatwa mwaka 2010 ambalo ni ongezeko la asilimia 100.
Source:Mwananchi

Post a Comment

4 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. HAHAHAHA BIASHARA YA WAKUBWA KIJANA

    ReplyDelete
  2. MMILIKI WA HOME SHOPPING CENTRE AMWAGIWA TINDIKALI

    ReplyDelete
  3. Hiyo ni biashara ya CCM huwezi kuivuruga.

    ReplyDelete
  4. CCM oyeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeee

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad