KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, familia ya Said Abdallah inayoishi
Buguruni jijini Dar es Salaam imelazimika kutokwa machozi upya baada ya
maiti ya mtoto Sophia Said (1) aliyefariki dunia kwa ugonjwa wa malaria,
kuibwa na watu wasiojulikana na kaburi lake kuachwa wazi, Uwazi
limechimbua.
Tukio hilo la aina yake na lililoacha maswali mengi,
lilitokea usiku wa Julai 20, 2013 kwenye Makaburi ya Buguruni Kwamkanda,
Mtaa wa Mnyamani jijini Dar es Salaam. Marehemu alizikwa Juni 20, 2013.
Uwazi
lilifika eneo la tukio na kukuta umati, ikiwemo familia ya Said
ukitokwa machozi huku wakiliangalia kaburi hilo likiwa wazi.
Mbao na miti iliyotumika kwenye mazishi ya mtoto huyo vilikutwa pembeni ya kaburi.
Wakati
watu wakiendelea kumwaga machozi huku wakiulizana nini maana ya tukio
hilo, Said ambaye ndiye baba mzazi wa marehemu alifika na kushuhudia
maajabu hayo ambapo naye alishindwa kujizua na kuanza kulia.
Baada ya hali kutulia kidogo, mwandishi wetu alihojiana na mfiwa huyo ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Nashindwa
hata kuelezea vizuri kwani tangu nizaliwe sijawahi kuona kaburi
limefukuliwa, maiti haipo na isijulikane ilikopelekwa.
“Nikiwa kazini
muda si mrefu uliopita nilipigiwa simu na shemeji yangu Said Masoud
ambaye anaishi maeneo haya, akaniambia kaburi lipo tupu na haoni maiti
ndani yake.
“Akasema mbaya zaidi, mbao na miti iliyotumika siku ya
mazishi viko pembeni kuashiria kwamba waliofanya kitendo hiki ni watu
waliokusudia.
“Niliishiwa nguvu, baadaye nilijikaza na kuja hapa. Ndiyo nimefika kama hivi na kukuta watu wengi nao wanashangaa.
“Nilipochungulia
kaburi niliona ni kweli lilibaki tupu. Marehemu alikuwa ni mtoto wangu
wa kwanza, niliwazaa mapacha na kwa sasa amebaki mwenzake aitwaye Salah.
‘Kinachonishangaza ni kwamba, marehemu tulimzika Juni 20 na kaburi limefukuliwa Julai 20, ina maana ni mwezi mmoja umepita.
“Sijajua
kwa nini imetokea hivi! Mpaka sasa hakuna mtu ninayemshuku kuhusika na
tukio hili, inawezekana ni mambo ya kishirikina, nakwenda kutoa taarifa
polisi na kisha tutarudishia mchanga kaburini.
“Kusema ule ukweli inauma sana jamani! Mwanangu yuko wapi? Hata kama ni marehemu lakini nijue alipo.”
Naye
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mnyamani, Jabir Sanze ambaye alikuwa
katika eneo la tukio, alipoulizwa na mwandishi kuhusu kitendo hicho,
alisema:
“Hili ni tukio la ajabu, polisi wanahaha kutafuta maiti na
wanafanya uchunguzi wa kina kwani tukio hili linaonekana halikufanywa na
mtu mmoja.”