Mjukuu wa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Mandla Zwelivelile Mandela ambaye ameibua mgogoro mkubwa katika familia ya shujaa huyo wa Afrika katika mzozo wa makaburi amekuwa na mlolongo wa visa katika maisha yake.
Visa hivyo kwa sehemu kubwa vinahusu maisha yake ya ndoa kwani ameoa na kuacha mara tatu huku akikabiliwa na kisa kingine cha kudaiwa kuuza haki za televisheni za kuonyesha mazishi ya Mzee Mandela.
Mandla ambaye jana aliamriwa na Mahakama kurejesha mabaki ya miili ya watoto watatu wa Mandela, alizaliwa mwaka 1974 na kwa sasa ni Chifu wa eneo la Mvezo. Ni msomi mwenye shahada ya kwanza ya siasa aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Rhodes mwaka 2007.
Chifu huyo wa Kabila la Xhosa amekuwa na vituko vingi katika maisha yake. Mwaka 2009 alizua utata baada ya kuuza haki ya kutangaza mazishi ya Mandela atakapokufa kwenye kituo cha televisheni cha SABC kwa Rand 3 milioni (Sh481 milioni).
Hata hivyo, suala hilo lilifikishwa katika Mahakama Kuu ya Mthatha ambako hukumu ilitoka na alipewa siku 15 kutangaza kama kweli ameuza haki ya matangazo ya mazishi ya Mandela au akanushe taarifa hizo.
Taarifa zilisema kuwa kutokana na shinikizo la baadhi ya wanafamilia na mkazo wa hukumu ya Mahakama, Mandla alilazimika kukanusha kuuza haki ya matangazo ya mazishi ya Mandela kwa kituo kimoja cha televisheni.
Mandla ambaye ni mtoto wa Makgatho Mandela aliyefariki dunia mwaka 2005 baada ya kuugua maradhi yanayofanana na ya Ukimwi, alipata hadhi ya uchifu baada ya kifo cha baba yake mwaka 2007.
Mandela ambaye alikabidhiwa uchifu wa uongozi wa watu wa Kabila la Xhosa takriban miaka 70, ndiye aliyempendekeza Mandla kuchukua wadhifa huo. Alikabidhiwa wadhifa huo mwaka 2007 wakati huo akiwa na umri wa miaka 32. Majukumu yake yalikuwa kuongoza sherehe za kimila, kutatua matatizo ya ndani ya ukoo wao na kuwakilisha Kabila la Xhosa katika masuala ya kisiasa.
Kutokana na majukumu hayo, Mandla alichaguliwa kuwa mbunge mwaka 2009 kupitia Chama cha African National Congress (ANC). Mke wake wa kwanza ni Tando Mabuna-Mandela aliyemuoa mwaka 2004. Hata hivyo, mwaka 2009, mwanamke huyo aliomba talaka mahakamani akidai kuwa mumewe huyo ni mgumba.
Mke wa pili wa Mandla ni Anais Grimaud aliyezaliwa mwaka 1990 huko Reunion ambaye alibadili jina lake na kuitwa Nkosikazi Nobubele. Walioana Machi 2010 katika ndoa ya kimila.
Septemba 2011 alipata mtoto aliyepewa jina la Qheya II Zanethemba Mandela na alikaribishwa kwa Mandela kijijini Qunu kwa taratibu za kimila. Hata hivyo, Agosti mwaka 2012, Mandla alimkataa mtoto huyo akidai mkewe alikuwa ana uhusiano na kaka yake, kesi ilifika mahakamani na waliachana kutokana na sababu hiyo.
Mkewe wa tatu ni Nodiyala Mbali Makhathini ambaye walioana Desemba 24, 2011, lakini tayari amefungua kesi ya kudai talaka.
MANDLA:MJUKUU ANAYE INYIMA USINGIZI FAMILIA YA MZEE MANDELA
0
July 04, 2013
Tags