Baada ya kushinda kata nne za Arusha kwenye
uchaguzi mdogo juzi, Chadema ilitamba kuwa kazi inayofuata ni kumng’oa
Meya kutokana na kuwa na viti vingi kwenye Baraza la Madiwani.
Lyimo aliliambia Mwananchi kuwa pamoja na Chadema kuwa wajumbe wengi kwenye Baraza la Madiwani, bado hawana ubavu wa kumtoa.
Alisema ili kumtoa katika nafasi hiyo wanahitaji
kuwa na theluthi mbili ya wajumbe . Lyimo alisema maana yake ni kuwa ili
ang’oke lazima Chadema waungane na madiwani wa CCM ndiyo watafanikisha
azma hiyo.
“Sharti la kumng’oa madarakani Meya au Mwenyekiti
wa halmashauri ni kupata theluthi mbili ya kura za wajumbe wote.
Najiuliza wenzetu watafikiaje kiwango hicho hadi waanze kutamba
kuning’oa madarakani,” alisema Lyimo.
Jiji la Arusha lina jumla ya wajumbe 32 kwenye
Baraza la Madiwani ambapo ukimtoa Meya, wajumbe wanaostahili kupiga kura
wanasalia 31 hivyo kufanya wenye nia ya kumng’oa kiongozi huyo kuhitaji
zaidi ya kura 24 kutimiza lengo lao.
Baada ya kunyakua viti vyote vinne kwenye uchaguzi
mdogo uliofanyika Jumapili iliyopita, Chadema imefikisha wajumbe 15
kwenye baraza ikiwa ni madiwani 12 pamoja na wabunge watatu, wawili wa
viti maalumu na mmoja wa jimbo.
Kwa upande wake, CCM kimebakia na wajumbe 14,
ikiwa ni madiwani 11 na wabunge watatu wa viti maalumu, huku TLP ikiwa
na wajumbe wawili ambao ni diwani mmoja wa kata na mwingine wa viti
maalumu.
Kata ya Sombetini ambayo awali ilishikiliwa na CCM
iko wazi baada ya aliyekuwa diwani wake, Alphonce Mawazo kujivua
uanachama na kuhamia Chadema.
Kutokana na mchanganuo huo, Meya Lyimo alisema
hana hofu ya kupoteza nafasi yake kwa sababu ili Chadema wafikie lengo
hilo, ni lazima waungwe mkono na wajumbe kutoka CCM, jambo alilosema ni
ndoto ya kutokea.
“Nakusisitizia ndugu yangu, mimi nipo na
nitaendelea kuwepo hadi mwisho wa kipindi changu kwa uwezo na msaada wa
Mwenyezi Mungu. Hakuna wa kuning’oa. Hata leo nilikuwa ofisini
kutekeleza majukumu yangu ya kuongoza kikao cha kamati ya fedha,”
alitamba Lyimo.
Meya huyo aliwataka madiwani kutoka Chadema kuacha
kupoteza muda na nguvu nyingi kuweka mikakati ya kumng’oa madarakani,
badala yake watumie muda na nguvu hizo kuwatumikia wananchi waliowaamini
na kuwapigia kura kwenye uchaguzi.