Kwa miaka mitatu iliyopita, Rehema Nduguru (50) anayeishi Mkoa wa Njombe alikuwa katika mazingira hatarishi ya kupata magonjwa ya ngono ikiwamo Ukimwi kutokana na kazi yake ya uhudumu wa baa.
Akitoa maelezo yake jijini Dar es Salaam hivi
karibuni, Rehema anasema kutokana na kazi hiyo alikuwa akilazimika
kufanya ngono zembe ili kujiongezea kipato. Hata hivyo, anashukuru Mungu
hakupata maambukizi ya Ukimwi.
“Wakati tukifanya kazi hiyo, mimi na wenzangu
tulikuwa tukifanya ngono zembe, hasa na madereva wa magari ya mizigo
yanayoegeshwa karibu na baa tulizokuwa tukifanyia kazi,” alisema Rehema.
Hata hivyo, Rehema sasa ameachana na kazi hiyo na amepata msaada kutoka Shirika la Kazi duniani (ILO).
“ILO walikuja Njombe na kutushauri tuunde vikundi
ambapo tulipewa fedha zilizotuwezesha kufanya kazi zenye staha. Sasa
ninauza nguo sokoni na ninapata fedha za kutosha kutokana na biashara
hiyo. Tumeanzisha ushirika wa kuweka na kukopa (Saccos) ambayo
inatuwezesha kujiendeleza kiuchumi,” anasema.
Kwa upande wake Mwajuma Sabuni anayefanya kazi
katika kiwanda kimoja jijini Dar es Salaam (jina linahifadhiwa)
analalamikia unyanyasaji wa kijinsia kutoka kwa waajiri wao.
“Nimefanya kazi katika kiwanda hiki kwa miaka saba
sasa. Kwa miaka miwili ya awali nilifanya kazi kama kibarua, lakini
baadaye nikaingizwa kwenye mkataba wa kazi na kuanza kukatwa mafao ya
uzeeni na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), bila kupewa kadi ya
uanachama na mwajiri wangu. Hadi sasa sijui hatima ya pensheni yangu,”
anasema na kuongeza:
“Kwa jumla hali ya ajira katika kiwanda hiki ni
ngumu hasa sisi wafanyakazi wa kike kwani rushwa ya ngono iko nje nje.
Wasimamizi wa vitengo ndiyo wahusika na ukiwakataa ajira yako inakuwa
hatarini. Licha ya kuwepo kwa Chama cha Wafanyakazi (Tuico) kinachojua
kero zote hizi, bado hazijashughulikiwa. Naiomba Serikali iingilie
katika kwa kuchunguza madai haya kwani tunanyanyasika mno.”
Maelezo ya wanawake hawa yanawakilisha kilio cha
wafanyakazi wengi wanaonyanyaswa kijinsia kutokana na kazi zao. Wengi
hulazimika kujiingiza kwenye ngono zisizo salama, hivyo kuhatarisha
maisha yao hasa kwa kupata ugonjwa wa Ukimwi.
Katika mkutano wa wadau wa kupambana na ugonjwa wa
Ukimwi, hasa maeneo ya kazi uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es
Salaam, wadau wanasema kuwa wanawake na wasichana wako kwenye hatari
zaidi ya kuathirika na ugonjwa huo na kwamba hatua stahiki zinapaswa
kuchukuliwa ili kukabilia na tatizo hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi
Tanzania (Tacaids), Dk Fatma Mrisho anasema kuwa makundi ya wanawake
walijitokeza kuomba msaada ili kujikwamua kimaisha na kujilinda.
“Hatari ya wanawake hawa kuathirika na Ukimwi ni
kubwa mno. Ni changamoto kubwa inayohitaji jitihada za kila mmoja wetu,”
anasema Dk Mrisho.