Kana kwamba alisikia kilio cha wakazi
wa Dar es Salaam waliokuwa na shauku ya kumwona lakini ikashindikana,
Rais Barack Obama wa Marekani amewaomba radhi kwa hali hiyo.
Akizungumza juzi wakati wa dhifa
iliyoandaliwa kwa ajili yake na ujumbe wake na Rais Jakaya Kikwete
katika Ikulu ya Dar es Salaam, Obama alisema akirudi nchini siku zijazo,
atapita mitaani akiwa katika gari la wazi.
"Niliona wananchi walivyojitokeza kwa
wingi kutupokea barabarani, nilifarijika sana lakini hawakuweza kutuona
vizuri kwani tulikuwa ndani ya gari maalumu-The Beast.
"Miaka ya sitini Rais John Kennedy
alipokuja hapa, alipita na gari la wazi mitaani wananchi wakamwona,
naomba radhi nikija tena nitaonekana," alisema Obama.
Watu wengi waliozungumza na vyombo
vya habari walionesha dhahiri kiu ya kutaka kumwona Rais huyo wa kwanza
mweusi wa Marekani, lakini wakaishia kuona gari lake ambalo hata hivyo,
lilipita kwa kasi barabarani kwenda Ikulu na kurudi Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere.
Kama ilivyokuwa imezoeleka huko
nyuma, Rais wa nchi ambaye amekuwa akifika nchini kwa mara ya kwanza,
amekuwa akipita mitaani kwa gari la wazi sambamba na mwenyeji wake
akisalimiana na wananchi, hiyo imekuwa ikifanyika pia kwa wasanii wa
kigeni.
Hata hivyo, safari hii ulinzi
ulionekana kuwa mkali katika ujio wa Rais Obama na kusababisha wenye kiu
ya kumwona moja kwa moja kushindwa kufanya hivyo isipokuwa waliokuwa na
uwezo wa kufika uwanjani na katika shughuli alizofanya maeneo kadhaa
jijini.
Mapema, Rais Kikwete alimhakikishia
Rais Obama kwamba kuanzia sasa Afrika itapenda kuona ongezeko la
uwekezaji na uhusiano wa kibiashara baina yake na Marekani.
Kikwete alisema hayo juzi usiku
katika Ikulu ya Dar es Salaam katika dhifa ya kitaifa aliyomwandalia
Rais Obama ambaye alimalizia ziara yake jana.
"Hii inaweza kuwa katika ngazi ya mataifa mawili au Taifa la Marekani na eneo la Jumuiya ya Afrika Mashariki,"alisema Kikwete.
Alimwambia uzinduzi wa Mpango wa
Nishati ya Umeme kwa Afrika wenye lengo la kusaidia nchi za Kiafrika
kukabiliana na upungufu wa nishati hiyo ni msaada ambao umekuja kwa
wakati mwafaka.
Alisema Afrika imekuwa ikilenga kuwa
na uchumi mkubwa na hatimaye kujiletea maendeleo, lakini kikwazo kikubwa
kimekuwa ni tatizo la umeme wa kutosha.
"Hatua hii ya Marekani kusaidia
katika eneo hilo, itakwenda sambamba na kuwezesha mataifa ya Afrika
kuibua uwezo wao wa kukuza uchumi na kuboresha maisha ya watu wao,"
alisisitiza Kikwete.
Alisema hatua hiyo itaimarisha
ushindani, itakuza maendeleo ya viwanda na kufanya nchi za Afrika
kushiriki vizuri katika uchumi wa dunia na kuwa wabia katika biashara ya
kimataifa badala ya kuwa wapokeaji wa misaada ya kigeni.
"Tunakupongeza kwa uongozi wako
katika kukabiliana na changamoto za maendeleo na usalama zinazolikabili
bara la Afrika. Umekuwa kishawishi kikubwa kwetu, tunaoamini katika
demokrasia, uhuru wa mtu, fursa sawa, kutokuwa na ubaguzi na kuwa na
Afrika isiyo na migogoro.
"Wewe ni rafiki wa kweli wa Tanzania
na Afrika, siku zote tutaenzi amali hizo katika nyoyo na fikra
zetu,"Kikwete alimwambia Obama.
Alieleza matumaini ya Watanzania
kwamba Obama atapata fursa nyingine ya kuja nchini na kukaa angalau kwa
muda mrefu kidogo ili ajionee mengi nchini; nchi ambayo ina vivutio kama
Mlima Kilimanjaro, hifadhi za Serengeti na Ngorongoro na kisiwa cha
marashi cha Zanzibar.
Rais Kikwete alimshukuru Rais Obama
na Serikali yake na watu wa Marekani kwa msaada wao endelevu kwa
Serikali na watu wa Tanzania.
"Msaada wenu katika chakula, elimu, afya, barabara, umeme na maji umesaidia kuboresha maisha ya watu wengi nchini Tanzania.
"Naamini uendelevu wa msaada huo
utamaanisha watu wengi kuondokana na umasikini. Kauli yako ya
kutuhakikisha kwamba Serikali yako itaendelea kuisaidia Tanzania katika
maendeleo imepokewa nasi kwa mikono miwili na unyenyekevu mkubwa,"
alisema Kikwete.
Akiwa Symbion, Rais Obama aliihimiza
Serikali kuhakikisha miradi ambayo itaanzishwa chini ya mpango wa Power
Africa utekelezaji wake uharakishwe ili kutoa fursa kwa wananchi kuona
manufaa yao katika kujipunguzia umasikini.
Alisema katika mpango huo ambao
Serikali yake imeahidi kutoa dola za Marekani bilioni 7, alisema sekta
binafsi ambayo itahusishwa kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wake
itatoa dola za Marekani bilioni 9.
Alisema kutakuwa na manufaa makubwa
iwapo mpango huo utahusisha Serikali na sekta binafsi kwa upande
mwingine akiongeza kuwa dhamira ya sekta binafsi katika kutoa kiasi
hicho cha fedha inaonesha nia ya Marekani kuinua Afrika yenye nuru,"
alisema Rais Obama akionesha matumaini ya mpango huo ambavyo unaweza
kunufaisha nchi nyingi za Afrika.
Obama ambaye aliitumia hotuba hiyo
kuaga Watanzania, alisema Symbion ni mfano wa miradi ambayo Marekani
imedhamiria kuitekeleza Afrika ya kuongeza maradufu uzalishaji wa
nishati ya umeme ambayo lengo ni kupunguza umasikini katika bara hilo.
Alisema ili miradi hiyo iwe na
manufaa kwa nchi husika kote alikopita, alitoa mwito kwa viongozi
kuhakikisha utekelezaji unaharakishwa ili kunufaisha nchi na kwa watu.
Alikemea tabia ya ucheleweshaji wa
miradi katika Afrika ikiwamo ya umeme lakini akasema ana imani na
uongozi wa Rais Kikwete kuwa mpango huo utatekelezwa kwa kasi. "Ni
lazima tuongoze katika utekelezaji wa miradi hii na naamini chini ya
Rais Kikwete hili linawezekana."
Alisema ili kufanikisha kuwa na umeme
wa uhakika ni vema kupunguza urasimu katika kuhudumia wawekezaji wa
sekta ya umeme ili wapate nafasi ya kuongeza kasi ya utekelezaji wa
miradi.
Aliongeza kuwa ufanikishaji wa mpango
huo utakuwa ni hatua ya ushindi kwa pande zote; yaani kwa Tanzania
ambayo itapata umeme wa uhakika ambao utasaidia kupunguza umasikini,
lakini pia kwa Marekani ambako wafanyabiashara watapata fursa ya
kuwekeza nchini.
Pia alitaka sheria na taratibu
zifuatwe na kuheshimiwa katika masuala yote ya uwekezaji ambao
utahusisha miradi itakayoanzishwa chini ya mpango wa Power Africa.
Alipoingia ndani ya mitambo ya Symbion, Rais Obama alikabidhiwa mpira wenye uwezo wa kuzalisha umeme wa gesi.
Mpira huo ambao umebuniwa na vijana
wa Kimarekani, unafaa kwa matumizi vijijini kwani unaweza hata kuchaji
vifaa vya umeme kama simu ambapo pia gesi hiyo ina uwezo wa kuwasha taa
inayoweza kutumika kumulika ndani ya nyumba.
Rais Obama alizindua mipira hiyo
ambayo itapatikana hivi karibuni nchini kwa kumpasia Rais Kikwete na
kueleza matumaini yake kuwa inaweza kuwa na manufaa makubwa katika
maeneo ambako hayajafikiwa na umeme.
Kampuni ya Symbion yenye makao yake
makuu Washington, Marekani imeajiri Watanzania 1,000 na Rais Obama jana
alitangaza kuwa ni kampuni pekee ambayo itasimamia ujenzi na ukarabati
wa miundombinu ya umeme inayofadhiliwa na Serikali ya watu wa
Marekani.
Symbion kwa sasa inatekeleza miradi
yenye uwezo wa kuzalisha umeme katika nchi za Afrika Mashariki na
Magharibi ambayo imepangwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.
Katika miaka mitano, kampuni hiyo imepanga kuwekeza kiasi cha Sh trilioni 3 katika uzalishaji umeme na njia za kuusafirisha.
Kati ya miradi hiyo, umo wa gesi
unaojengwa Mtwara wenye uwezo wa megawati 400 na unaendeshwa kwa
kushirikiana na kampuni nyingine ya Marekani ya General Electric (GE)
itakayotoa vifaa vya ujenzi katika mradi huo ambao unahusisha ujenzi wa
njia ya umeme yenye umbali wa kilometa 650.
Nchini, kampuni hiyo kwa sasa
inamiliki vituo vitatu vya kuzalishia umeme wa jumla ya megawati 217
ambavyo vipo Dar es Salaam, Dodoma na Arusha. Kituo cha Ubungo cha
Symbion kinazalisha megawati 112 kwa gesi na ndiyo kampuni inayozalisha
umeme mwingi unaoingizwa kwenye gridi ya Taifa.
Mitambo hiyo imetengenezwa mjini
Houston, Texas na inaelezwa kuwa ya kisasa zaidi yenye uwezo mkubwa wa
kufua umeme kwa kasi kama ilivyo injini ya ndege. Mitambo hiyo awali
ilikuwa ya Dowans ambayo iliileta nchini baada ya kupewa zabuni ya
kufanya hivyo na Kampuni ya Richmond.
Awali baadhi ya wabunge walishauri
inunuliwe na Serikali, lakini baadhi yao walikataa kuwa ni mitumba na
sheria ya manunuzi hairuhusu. Lakini mitambo hiyo ambayo baadhi ya
Watanzania waliikejeli leo ndiyo kimbilio la Serikali kutokana na vyanzo
vya kufua umeme wa maji kupungua uwezo wake.
Kutokana na mapenzi mengi waliyonayo
Watanzania kwa Obama, jana maelfu ya watu walikusanyikwa Ubungo ili
kumwona Rais huyo mweusi wa Marekani.
Tangu saa mbili asubuhi Ubungo
ilishafurika watu na hadi anawasili eneo hilo saa 5 asubuhi umati huo
ulishaongezeka hali inayoonesha kuwa Rais huyo ni kipenzi cha
Watanzania.