ONYO lililotolewa na Ikulu ya Marekani dhidi ya Serikali ya Rwanda,
linalomtaka Rais wa nchi hiyo, Paul Kagame, kuacha kuwasaidia waasi wa
kikundi cha M23, lina kila dalili zinazomuweka kwenye kundi la viongozi
wa Kiafrika ambao hatma yao baada ya kuachia madaraka inazungukwa na
wingu la mashaka.
Rais wa Marekani, Barack Obama, ambaye mapema
wiki hii alikaririwa na vyombo vya habari mbalimbali duniani akimtaka
Rais Kagame kuacha kukisaidia kijeshi kikundi cha waasi wa M23,
anaaminika kuitoa kauli hiyo kama msimamo wa serikali yake inayopinga
watawala wanaojihusisha na uhalifu wa kivita.
Ingawa hadi sasa
Rais Kagame hajatajwa na Ikulu ya Marekani kama mmoja wa viongozi wa
Afrika wanaotuhumiwa kwa uhalifu wa kivita, onyo lililotolewa na Rais
Obama linadhihirisha kuwepo kwa ushahidi unaomhusisha na matukio ya aina
hiyo yaliyopata kuwagharimu baadhi ya marais walionyooshewa kidole na
Marekani kwa aina hii hii anayonyooshewa sasa Kagame.
Wadadisi na wafuatiliaji wa mambo walioichambua kauli ya Rais Obama,
wanaeleza kuwa aliitoa baada ya Marekani kujiridhisha na ushahidi
ilioukusanya ukiihusisha Serikali ya Rwanda kuwasaidia waasi wa kundi la
M23.
Wanaeleza kuwa Marekani baada ya kubaini ushirika wa
majeshi ya Rwanda yaliyojipenyeza ndani ya makundi ya waasi wanaopigana
na Serikali ya Kongo, huku wakitekeleza vitendo vya kinyama dhidi ya
binadamu katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo yenye utajiri mkubwa
wa madini, imeamua kumtosa Kagame, ambaye amekuwa na uswahiba wa muda
mrefu na taifa hilo.
Katika tathimini yao kuhusu uzito wa onyo la
Rais Obama kwa Rais Kagame, wanaeleza kuwa hataweza kuepuka kitanzi cha
mashitaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC).
Waasi
wa kikundi cha M23, mbali na kuendesha mapambano dhidi ya majeshi ya
Serikali ya Kongo, jambo linalopingwa na jumuiya ya kimataifa, pia
wanatuhumiwa kwa ubakaji na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.
Tuhuma
hizo pia zinaelekezwa kwa majeshi ya Rwanda, yanayodaiwa kushirikiana
na waasi hao na ndizo zinazomuweka Rais Kagame katika hatari ya
kufikishwa mahakamani na hata kuhukumiwa kama ilivyokuwa kwa aliyekuwa
Rais wa Liberia, Charles Taylor, ambaye kwa sasa anatumikia kifungo cha
miaka 50 jela baada ya kupatikana na makosa ya uhalifu wa kivita nchini
Sierra Leone ambako zaidi ya watu 50,000 waliuawa katika vita ya wenyewe
kwa wenyewe na wengine wengi wakiachwa na ulemavu wa kudumu.
Kama
inavyotokea kwa Rais Kagame sasa, kwa Taylor pia ilikuwa hivyo hivyo,
pale alipokuwa akionywa na jumuiya za kimataifa na yeye kudharau maonyo
hayo.
Wakati wadadisi na wachambuzi wa mambo wakiwa na mtizamo
huo kuhusu onyo la Serikali ya Marekani dhidi ya Rais Kagame kujiingiza
kijeshi katika vita vya ndani ya Kongo, ushahidi uliokusanywa na taasisi
za Umoja ya Mataifa za kutoa misaada ya kibinadamu unaonyesha kuwa
wanajeshi wa Rwanda wanaopigana bega kwa bega na waasi wa M23 wamekuwa
wakijihusisha na vitendo vya kihalifu dhidi ya binadamu.
Ni
ushahidi wa aina hiyo ndio uliotumiwa na ICC, kumhukumu Taylor,
aliyekuwa akituhumiwa kuvisaidia vikundi vya waasi vya Revolutionary
United Front (RUF) na Armed Forces Revolutionary Council (AFRC) kwa
kuvigawia silaha za kivita kwa muktadha wa kupewa madini ya almasi.
Stephen
Rapp, mchambuzi wa sheria za makosa ya jinai wa Marekani, katika
mahojiano yake na gazeti la The Guardian la nchini Uingereza, alieleza
kuwa uongozi wa Serikali ya Rwanda una tuhuma za kujibu katika Mahakama
ya ICC, kuhusu mapigano yanayoendelea Mashariki mwa Kongo.
Kauli
hiyo ya Rapp inaunga mkono madai ya mara kwa mara ya mashirika ya
kimataifa yanayojihusisha na utetezi wa haki za binadamu ya Human Right
Watch, Save the Children, UNICEF na UNHCR, ambayo kwa nyakati tofauti
yamekuwa yakidai kuwa na ushahidi wa kutosha wa waasi wa M23 kusaidiwa
na Jeshi la Rwanda kufanya mauaji ya raia wasiokuwa na hatia katika miji
mbalimbali ya Mashariki mwa Kongo.
Inadaiwa pia kuwa upo
ushahidi unaoonyesha jinsi ambavyo waasi wa M23 wamekuwa wakiwatumia
watoto wadogo katika vikosi vya majeshi na ndio ambao wamekuwa
wakitangulizwa mstari wa mbele katika uwanja wa mapambano, hususan
katika matukio ya uhalifu wa kivita.
Tuhuma nyingine
zinazoelekezewa Serikali ya Kigali ni kufadhili kundi la waasi la CNDP,
lililokuwa chini ya uongozi wa Jenerali Bosco Ntaganda, ambaye
amejisalimisha kwenye Mahakama ya ICC mapema mwaka huu.
Sehemu
kubwa ya wapiganaji wa kundi la Ntaganda sasa wameungana na waasi wa
kundi la M23 na wamekuwa wakijiimarisha kiulinzi katika maeneo yenye
utajiri mkubwa wa madini nchini Kongo.