Hiyo inatokana na kauli ya Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba aliyoitoa jana
akisema kwamba wizara yake ilipinga tangu awali mpango huo kabla ya
kupitishwa na kuwa sheria na kwamba anaamini itaondolewa. Kauli hiyo ya
Makamba imekuja siku moja baada ya chama tawala, CCM, kukaririwa na
vyombo vya habari kikiitaka Serikali kuangalia vyanzo vingine vya mapato
badala ya tozo hiyo.
Akizungumza kwa simu jana Makamba alisema:
“Sikubaliani na hili suala na kupita kwake ilikuwa ni kuzidiwa nguvu.
Lakini najua haliwezi likatekelezeka ni lazima litabadilishwa kwa
kuangalia eneo lingine la kutoza kodi.”
Alisema msimamo wa wizara yake katika suala hilo
ni tofauti kwani imekuwa ikijitahidi kuhakikisha gharama za mawasiliano
zinapungua... “Wizara hatukubaliani na kodi hiyo. Nia yetu ni kupunguza
gharama za kupiga simu kwa kuwa ni kitu kinachowezekana.
“Nia yetu ni kushusha gharama iwe sifuri kabisa,
kitu chochote kinachopandishwa bei sisi hatukubaliani nacho kwa kuwa ni
kuwaumiza wananchi wetu hasa wa vijijini. Bidhaa ambayo inatakiwa
kushuka ni mawasiliano hivyo lazima iwe hivyo.”
Jana, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alisema
kwamba Serikali inapokea maoni ya wadau mbalimbali ili kuona namna ya
kufanya marekebisho ya tozo hiyo. Hata hivyo, alisema uamuzi wa
kuanzisha tozo hiyo haukuwa wa Serikali bali ulipitishwa na kukubaliwa
baada ya kujadiliana na Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa
Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.
“Hayo yalipendekezwa na Kamati ya Bunge siyo
Serikali. Tena walipendekeza vyanzo 67 vya kodi likiwamo hilo la kadi za
simu. Walipendekeza tukate Sh1,450 kwa mwezi, lakini sisi Serikali
tukashusha hadi Sh1,000 yaani kila mwananchi akatwe Sh33.3 kwa siku na
mapato yatakayopatikana yatakwenda kuboresha miradi ya maji, umeme
vijijini na barabara,” alisema Dk Mgimwa.
Upinzani mkali
Wabunge wa Chadema, John Mnyika wa (Ubungo) na
Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini), wamekuwa mstari wa mbele kupinga kodi
kwa kuonyesha jinsi itakavyowanyanyasa wananchi.
Mnyika amekuwa akikusanya saini za wananchi
wanaopinga mpango huo wa Serikali ili awasilishe bungeni hoja ya
wananchi kupinga tozo hiyo. Hadi sasa ameshakusanya saini zaidi ya
26,000.
Kwa upande wake, Zitto alisema kodi hiyo
haikujadiliwa kabisa kwa kuwa iliondolewa katika mapendekezo ya mapato
lakini ikarejeshwa kupitia Muswada wa Fedha ambao hutafsiri hotuba ya
Bajeti kisheria.
“Kama kodi hii haikuwa kwenye hutuba,
haikujadiliwa na Bunge, msingi wa Muswada wa Fedha kuwa na kodi hii
haupo. Kodi hii ilirejeshwa kinyemela bungeni na kupitishwa bila
mjadala.”