Katika siku za hivi karibuni, tumeshuhudia matukio makubwa ya wizi, ujambazi na ujangili yakiwa yanawahusisha baadhi ya askari katika majeshi yetu ya ulinzi na usalama. Matukio hayo yamesababisha aibu na fadhaa kwa jamii nzima ya Watanzania, kwani wananchi wengi sasa wanauliza wapi tunakoelekea kama majeshi yetu ya ulinzi na usalama ambayo yana dhima ya kulinda raia, mali zao na rasilimali za taifa ndio yanashiriki katika uhalifu.
Baada ya viongozi wetu wengi nchini kutokomea katika vitendo vya ufisadi na kupoteza imani ya wananchi, hasa baada ya kuzikwa kwa Azimio la Arusha, imani ya wananchi ilibaki tu kwa majeshi yetu ya ulinzi na usalama. Ni masikitiko makubwa kwamba vyombo hivyo sasa vimeingia dosari kubwa na sio siri kwamba zinahitajika juhudi za makusudi ili kuyarudisha katika mstari ulionyooka.
Tumeghadhabishwa na ushiriki wa askari wetu katika vitendo vya ujangili na ujambazi. Juzi watu 10, wakiwamo askari wawili wa Jeshi la Polisi wenye silaha walikamatwa wilayani Kisarawe na meno ya tembo 75 yenye uzito wa kilo 305 na thamani ya Sh850 milioni. Kwa mujibu wa mamlaka za Maliasili, meno hayo yaliyokuwa yakisafirishwa kuja Dar es Salaam yakiwa katika magari mawili yanaonyesha kwamba wameuawa tembo wapatao 35.
Hili ni tukio la pili kuripotiwa katika kipindi kisichozidi wiki moja, kwani wiki iliyopita askari Magereza watatu wa Wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara walikamatwa wakiwa na gari la Jeshi la Magereza pamoja na silaha likiwa limepakia nyara za Serikali, wakiwamo twiga, pundamilia, swala na mbuni wenye thamani ya Sh56 milioni.
Itakumbukwa kwamba Ofisa wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Suleyman Chesano ambaye amekuwa akikabiliwa na kesi ya kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya Sh4 bilioni, alipandishwa tena mahakamani, jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita, baada ya kukutwa na meno mengine ya tembo kilo 781 yenye thamani ya Sh9.3 bilioni. Hii ilikuja baada ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Sajenti Azizi Yusufu, kukamatwa akiwa na pembe mbili za ndovu na bunduki moja aina ya rifle, eneo la kibaoni, wilayani Karatu, mkoani Arusha.
Katika tukio la aina yake lililotokea mkoani Kilimanjaro hivi karibuni, askari wawili wa Jeshi la Polisi wakiwa na gari la jeshi hilo walikamatwa wakiwa wamepakia magunia 18 ya bangi wakiisafirisha kwenda nchi jirani. Mmoja wa askari hao alitoroka na kutokomea kusikojulikana. Wakati huohuo, wakazi wa Dar es Salaam pengine hawajasahau tukio lililotokea Kariakoo miezi michache iliyopita ambapo askari polisi wawili walipora Sh150 milioni kutoka kwa majambazi waliokuwa wameiba fedha hizo kutoka kwa mfanyabiashara mmoja.
Tulimsikia Rais Jakaya Kikwete juzi akiwakemea Takukuru na watumishi wa Idara ya Uhamiaji kwa kula rushwa na kufumbia macho wahamiaji haramu zaidi ya 52,000 walioingia nchini kutoka nchi jirani. Kwa kuwa yeye ni Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa nchi, ni matumaini yetu kwamba atapitisha fagio la chuma katika majeshi yetu ili wabaki tu askari wenye nidhamu, uadilifu, uzalendo na wanaofuata maadili ya kazi zao za ulinzi na usalama wa nchi yetu.