Dar
es Salaam. Siku moja baada ya Rais wa Marekani, Barack Obama kuondoka
nchini, maisha kwa wakazi wa Dar es Salaam yamerejea katika hali ya
kawaida, huku baadhi ya wafanyabiashara na ombaomba wakirejea kwa kasi
maeneo yaliyosafishwa wakati wa ujio huo.
Halmashauri
ya Jiji la Dar es Salaam ilianzisha operesheni maalumu ya usafi kabla
na wakati wa ujio wa Obama, hatua iliyopokewa kwa mtazamo tofauti na
wakazi hao.
Timu
ya Mwananchi iliyovinjari kona mbalimbali za Dar es Salaam jana,
ilishuhudia wafanyabiashara wakirudi huku wengine wakijenga upya vibanda
vilivyobomolewa.
Kwa
nyakati tofauti, baadhi ya wafanyabiashara hao, walisema changamoto za
maisha zinazowakabili ndizo zimewasukuma kurejea, kwa sababu hawana kazi
wala sehemu nyingine ya kufanyia biashara zao.
Kituo cha Mabasi Mwenge, kulikuwa na wafanyabiashara wachache walioanza kurudi taratibu kwa kuvizia.
Mwananchi
ilikutana na ombaomba kadhaa Barabara ya Sam Nujoma na ile inayoelekea
Kiwanda cha CocaCola Kwanza Mikocheni, huku polisi waliokuwa makutano
hayo wakiwaangalia bila kufanya chochote.
Wafanyabiashara hao walisema wameamua kuendelea kufanya biashara zao kutokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili.
Katika
maeneo ya Ubungo, wafanyabiashara ndogondogo walionekana kuendelea na
biashara hususan pembezoni mwa barabara, Ubungo Darajani na ndani ya
Kituo cha Daladala cha Ubungo.
Hata
hivyo, licha ya kuendelea na biashara hizo, baadhi yao wameonyesha
wasiwasi kufungua kwenye maeneo hayo waliyofukuzwa awali, kwani hakuna
tamko lililowaruhusu kuendelea.
Mmoja
wa wafanyabiashara hao, Jabir Hamis, alisema: “Nashukuru kumalizika kwa
ziara ya Rais Obama nchini, kwani tuna siku mbili hatujafanya
biashara.”
Wafanyabiashara
wengine waliorudi maeneo ya Ubungo, ni wale wanaofanya biashara za nguo
katika makutano ya Barabara za Mandela, Sam Nujoma na Morogoro na
bodaboda wanaoegesha Kituo cha Tanesco.
Tabata
Relini karibu na Ofisi za Mwananchi Communications Limited (Ltd),
wafanyabiashara ndongondogo waliovunjiwa vibanda, walianza kujenga
mabanda yao na kurudi kwa kasi.“Sisi bwana, tumerudi kwa sababu hapa
tunajipatia kula. Ni kweli tupo kinyume cha sheria, lakini hatuna jinsi
hapa ndipo tunapopata riziki zetu, nasomesha watoto kwa kazi hii ya
mamalishe,” alisema mmoja wa mamalishe ambaye hakutaka kutajwa.
Maeneo ya Buguruni, wafanyabiashara wanaopanga bidhaa zao
pembezoni mwa barabara, walirejea na kuendelea na shughuli zao kawaida.
Wauza nguo za mitumba wamerejea eneo la Bakhresa,
walisema wao wanaamini waliondolewa kupisha msafara wa Obama, baada ya
hapo wanaendelea.
Hali ya uchafu nayo ilionekana kurejea eneo hilo, mifuko
ya plastiki na makaratasi yalionekana kuzagaa barabarani ambayo Jumanne
ilikuwa iking’aa kwa usafi.
Maeneo ya Kariakoo kwenye makutano ya Barabara ya Uhuru
na Msimbazi, lilionekana katika hali ya usafi na kuvutia kama ilivyokuwa
wakati wa ujio wa Obama, ingawa wafanyabiashara walianza kurudi kwa
kuvizia mgambo.
Takriban wiki moja kuelekea ujio wa Obama, maeneo
mbalimbali ya katikati ya Dar es Salaam na pembezoni, yalikuwa katika
hali ya usafi na wafanyabiashara waliokuwa wakipanga bidhaa pembezoni
mwa maeneo yasiyo rasmi waliondolewa.
Imeandaliwa na Daria Erasto, Benjamini Mwangoka, Muka Mkufya, Minael Msuya na Amelda Ringo.
SURA HALISI YA UCHAFU DAR ES SALAAM YAREJEA SIKU MOJA BAADA YA OBAMA KUONDOKA TANZANIA
0
July 05, 2013
Tags