Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema litaivunja Timu ya
Taifa (Taifa Stars) mpaka Novemba mwaka 2014 iwapo itaondolewa na Uganda
katika machi ya marudiano kusaka tiketi ya kucheza michuano ya CHAN
mwakani.
Mwanza. Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la
Soka nchini (TFF), Saad Kawemba amesema iwapo Timu ya Taifa (Taifa
Stars) itafungwa katika mchezo wake wa marudiano dhidi ya Timu ya Taifa
ya Uganda (The Cranes), timu hiyo itavunjwa mpaka Novemba 2014.
Stars inahitaji ushindi wa mabao 2-0 ili kufuzu
kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani
(CHAN). Katika mchezo wa kwanza Stars ililala bao 1-0 kwenye Uwanja wa
Taifa.
Akizungumza katika hafla ya mlo wa jioni
iliyoandaliwa na Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL) juzi, Kawemba alisema
hakutakuwa na sababu ya kuwa na timu ambayo haishiriki mashindano
makubwa ya kimataifa, hivyo amewataka wachezaji kuhakikisha wanashinda
mchezo wa marudiano.
“Sababu ya kuja kuweka kambi Mwanza ni kuhakikisha
tunashinda mchezo wetu wa marudiano dhidi ya Uganda. Mwaka jana timu
ilipoweka kambi hapa Mwanza, ilikwenda Kampala na kushinda mechi tatu
kwenye michuano ya Chalenji iliyofanyika Uganda,” alisema Kawemba.
“Tupo Mwanza kwa sababu tunakwenda kucheza Kampala
Julai 27, mwaka jana wakati wa Chalenji tuliweka kambi hapa na
tulipotoka tulifika Kampala na kushinda mechi tatu mfululizo, sasa kama
tupo Mwanza tena ni kwa nini tusiende kushinda mechi hii.”
Kawemba alisema ni jukumu la wachezaji kuhakikisha
wanashinda mchezo huo ili kupata fursa ya kushiriki mashindano makubwa
Afrika mwakani.
“Naamini timu yetu nzuri na inaweza kushinda mechi
ya marudiano. Wachezaji hampaswi kuvunjika moyo na mashabiki kwa
kufungwa mchezo wa kwanza. Mashabiki siku zote wanataka ushindi na siyo
kufungwa,” alisema zaidi.
“Mashabiki ni watu wa kulaumu sana, wanataka timu
ifanye vizuri na matokeo yanapokuwa kinyume chake wanakasirika,” alisema
Kawemba na kuongeza:
“Wametusema viongozi kwamba tumeisahau timu na
kuweka mkazo zaidi kwenye uchaguzi wa TFF. Hakuna ukweli kwenye jambo
hili, TFF imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha timu inafanya vizuri
kwenye mashindano.”
Kwa upande wake Meneja wa Kanda wa Kampuni ya Bia
Tanzania (TBL), Malaki Sitaki alisema wadhamini hujisikia raha timu
inapofanya vizuri kwenye mashindano.
“Imani yetu ni kuwa tunayo timu bora, nzuri na
mategemeo yetu ni kushinda hata kwao. Kama walitufunga nyumbani, kwa
nini na sisi tusiwafunge kwao?” alihoji Sitaki.