Spika wa Bunge, Anne Makinda, ameibuka na kauli yenye utata mkubwa
akivituhumu vyombo vya habari kwamba vinahongwa na wabunge wa kambi ya
upinzani ili viandike habari zao vizuri.
Bila kufafanua ni kwa jinsi gani wabunge hao wanatoa hongo hiyo mbali tu
ya kusema wanatoa kitu kidogo ili waandikwe vizuri, pia alikana
kuwakandamiza wabunge wa kambi hiyo na kuwabeba wale wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ambao wako upande wa serikali.
Alisema hana upendeleo katika uendeshaji wa vikao vya Bunge kama
anavyoshambuliwa na baadhi ya watu na kwamba lawama zinazoelekezwa kwake
zinatokana na watu kuangalia upande mmoja.
Spika Makinda alitoa ufafanuzi huo jana ofisini kwake jijini Dar es
Salaam wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu vurugu
mbalimbali zinazotokea katika vikao vya Bunge mjini Dodoma na hasa juu
ya kuporwa au kugeuzwa kwa hoja za upinzani.
Spika Makinda alikuwa ametoka kuzungumza na Spika wa Korea Kusini, Kang Chang Hee.
"Ndiyo najua mnapewa 'kitu kidogo' na hawa wanaoanzisha vurugu bungeni,
lakini kusema Spika anapendelea hili siyo kweli hata kidogo," aliongeza
Spika.
Alisema iwapo angekuwa na kawaida ya kuwakandamiza wabunge wa upinzani
kwa kiasi kinachosemwa wengi wa wabunge hao wa upinzani wasingekuwapo
bungeni.
“Mimi siwapendelei wabunge wa CCM, ningekuwa hivyo hawa wapinzani
wasingekuwapo bungeni,” alisema Makinda muda mfupi baada ya kuzungumza
na ujumbe wa Bunge la Korea Kusini uliomtembelea ofisini kwake.
Makinda alisema wakati wa kuendesha vikao vya Bunge haitakiwi kuwa na
itikadi za vyama na kwamba kufanya hivyo kunaweza kusababisha vurugu.
Wakati Spika akitoa utetezi huo, wabunge wa upinzani kwa nyakati tofauti
wamekuwa wakimtupia lawama za wazi hususani wanapokuwa katika vikao vya
Bunge kwamba anawapendelea wabunge wa CCM.
Miongoni mwa mambo ambayo Spika Makinda amekuwa akilaumiwa ni pamoja na
kukalia zaidi ya taarifa 10 za ushahidi juu ya kauli za wabunge wa
upinzani zilizowasilishwa kwake na yeye kuzikalia kwa muda wote bila
kusema lolote.
Miongoni mwa ushahidi huo, umo wa mawaziri kusema uongo bungeni.
Pia Spika amekuwa akilaumiwa jinsi mjadala wa hoja binafsi za wabunge wa
upinzani ‘zilivyoporwa’ na serikali, kama ile ya Mbunge wa Kuteuliwa
(NCCR-Mageuzi), James Mbatia, kuhusu mitalaa ya elimu; ya mbunge wa
Ubungo (Chadema), John Mnyika, kuhusu hali ya upatikanaji wa maji katika
jiji la Dar es Salaam, na hata ya Mbunge wa Arumeru Mashariki
(Chadema), Joshua Nassari, kuhusu ardhi ya Meru.
Zote hizi ama ziligeuzwa na kupoteza maana yake hali iliyosababisha
mvutano mkali bungeni ukiacha picha ya upendeleo wa dhahiri kwa baadhi
wafuatiliaji wa mijadala ya Bunge.
Akizungumzia mchakato wa kupata Katiba mpya, Spika Makinda alisema Bunge
la Katiba litakutana Novemba, mwaka huu na litawajumuisha wabunge wote
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja
na wajumbe 160 ambao hata hivyo alisema sheria haijasema wanapatikana
vipi.
Alisema mwezi ujao serikali inatarajia kupeleka muswada wa sheria ili
kufanya marekebisho ya namna ya kupata wajumbe hao 160 ambao siyo
wabunge.
Spika alisema katika Bunge hilo, yeye hatakuwa mwenyekiti na kwamba wajumbe wenyewe watachagua kiongozi atakayewaongoza.
Kauli ya Makinda iliwahi kusemwa pia na Naibu wake, Job Ndugai, mara
baada ya kuahirisha kikao cha Bunge kwenye mkutano uliopita, kufuatia
vurugu zilizotokea baada ya hotuba ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani
Wizara ya Mambo ya Nje, Ezekiah Wenje, kutamka kuwa Chama cha Wananchi
(CUF) kina uhusiano na vyama vinavyounga mkono mashoga.
Wakati vurugu zikiendelea nje ya viwanja vya Bunge kwa wabunge wa CUF na
Chadema kuzozana, Ndugai alipita ndipo aliulizwa na waandishi Kulikoni,
lakini katika hali ya kushangaza, alivituhumu vyombo vya habari kwamba
ndivyo vimesababisha hali hiyo.
“Haya yote mmesababisha ninyi waandishi, mnawadekeza sana wabunge wa
upinzani, hata wangefanya nini mnawapamba pamba, lakini mkumbuke siku
wakiingia madarakani watafanya haya haya wanayofanya leo,” alisema
Ndugai bila kufafanua kauli yake.
Kwenye mazungumzo yake na ujumbe wa Bunge la Korea uliomtembelea ofisini
kwake, Spika alisema unalenga kudumisha ushirikiano katika nyanja
mbalimbali zikiwamo za uwekezaji na kuendeleza uchumi wa nchi hizo
mbili.
Kwa upande wake, Spika wa Korea, Chang Hee alisema nchi yake imepiga
hatua kubwa ya maendeleo ingawa haina chanzo chochote cha kuzalisha
nishati ya umeme ikilinganishwa na Tanzania.
Alisema Bunge la Tanzania linafanya vizuri kwa upande wa nafasi za viti
maalum ikilinganishwa na Korea Kusini ambayo idadi ya wanawake bungeni
ni ndogo.
Nipashe:
Basi kama ni hivyo ata CCM inahonga ili nayo iandikwe vizuri
ReplyDelete