Kampala. Imeelezwa kuwa changamoto kubwa inayoikabili Timu ya
Taifa (Taifa Stars) kiasi cha kudhoofisha mipango yake ya kusaka
mafanikio ni baadhi ya wachezaji wanaoitwa kuitumikia kukosa uzalendo
kwa nchi yao.
Habari za ndani ilizozipata Mwananchi zinadai
kuwa, Kocha wa Stars Kim Poulsen amekuwa akikutana na wakati mgumu
katika kazi yake kwani baadhi ya wachezaji wamekuwa wakigoma kujiunga na
timu hiyo pale wanapoitwa.
Hali hiyo imedaiwa kuwa chanzo cha mafaniko duni ya kikosi hicho, kwa vile baadhi ya wachezaji wamekuwa hawajitumi uwanjani.
Chanzo hicho kilisema kuwa, Kim alilazimika
kufanya kazi ya ziada kuwashawishi baadhi ya wachezaji tegemeo kujiunga
na kikosi chake kwa ajili pambano dhidi ya Uganda lililopigwa jana
kwenye Uwanja wa Mandela jijini Kampala.
“Tunafanya jitihada za dhati ili Tanzania iweze
kufikia mafanikio lakini kuna vikwazo tunakutana navyo kama baadhi ya
wachezaji kukosa uzalendo,” kilidai chanzo hicho na kuongeza:
“Mfano John Bocco na Sure Boy (Abubakar Salum)
hawakutaka kwenda Mwanza ilimbidi Kim na Marsh (kocha msaidizi wa Stars)
wafanye kazi ya ziada kuwashawishi ndiyo wakakubali,”.
Mbali ya Bocco na Sure Boy, mchezaji mwingine
ambaye alitaka kujiondoa kwenye kikosi chake kwa madai kwamba
hathaminiwi kutokana na kutopangwa katika mechi kuwa Athuman Iddi.
“Unajua Chuji huwa anaitwa lakini hatumiwi na
Poulsen Stars hivyo akasema anajitoa kwa sababu umuhimu wake hauonekani,
lakini kukosekana kwa Mwinyi Kazimoto kukamfanya Kim amshawishi
aendelee kuwapo kikosi,” kilisema chanzo hicho.
Pia ilidaiwa kuwa hata wakati kikosi cha Stars
kilipokuwa jijini Mwanza, Boko na Sure Boy walitaka kugoma kwenda
Kampala, ambapo Poulsen na Marsh walipochukua jukumu la kuwashawishi na
ndipo wakakubali upanda ndege.