Tumeshangazwa mno na ukimya wa Serikali kuhusu janga kubwa la biashara ya dawa za kulevya ambalo limeikumba nchi yetu kwa muda mrefu sasa. Hatutaki kuamini kwamba Serikali haina taarifa za kuwapo kwa janga hilo hapa nchini, wala kuamini kwamba Serikali hiyo bado haijatambua ukubwa wa tatizo hilo.
Mbali na kauli nyepesi za polisi na taasisi nyingine husika kwamba zinafanya uchunguzi ili kugundua watu wanaojihusisha na biashara hiyo, hatujasikia kauli nzito kutoka kwa kiongozi mkuu wa nchi, Rais Jakaya Kikwete ambaye ndiye pekee mwenye sauti yenye mamlaka anayeweza kuzungumzia tatizo hilo, hasa kwa kutilia maanani kwamba biashara hiyo haramu sasa imefikia kiwango cha kutisha na wananchi wamechoka kusikia ahadi zisizotekelezeka za kuikomesha.
Hivyo, wakati huu wananchi hawategemei Rais Kikwete atoe kauli zilizozoeleka kwamba anayo orodha ya watu wanaojihusisha na biashara hiyo na kuwataka waache uhalifu haraka. Tunasema kauli kama hizo zimezoeleka kwa wananchi na sasa ni wakati wa kuwaeleza hatua zilizochukuliwa dhidi ya watu hao, ikiwa ni pamoja na mipango na mikakati inayochukuliwa na Serikali hivi sasa katika kutokomeza janga la dawa za kulevya hapa nchini.
Yamesemwa mengi kuhusu nguvu ya kifedha waliyonayo magwiji wanaoendesha biashara hiyo, kwamba wanajigamba hadharani kwamba wameitia Serikali yetu mfukoni. Pamoja na majigambo hayo, sisi tunadhani kwamba kinachohitajika kwa sasa ni Rais Kikwete kuthibitisha kwa vitendo kwamba kweli anao ujasiri na utashi wa kisiasa wa kutokomeza biashara hiyo ambayo tayari imevuruga maisha ya vijana wengi hapa nchini na kuharibu taswira ya nchi yetu.
Hatuna shaka yoyote kwamba Rais anazo zana zote za kupambana na watu hao kwa kuwa yeye kikatiba ndiye mkuu wa nchi, kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu, kwa maana ya kuwa kamanda wa majeshi ya ulinzi na usalama. Kwa nafasi hiyo, anawezaje kushindwa vita ya kutokomeza biashara hiyo kama anao ujasiri na utashi wa kisiasa wa kushinda vita hiyo, huku wananchi kwa ujumla wao wakiwa nyuma yake?
Wananchi wanauliza maswali kuhusu wapi Rais Kikwete amekwazwa katika vita hiyo. Maswali hayo ni ya msingi, kwani sio siri kwamba hivi sasa zipo taarifa za kutosha kuhusu mitandao ya biashara hiyo na majina ya magwiji wanaomiliki na kuendesha biashara hiyo.
Serikali inajua fika kwamba mtambo wa kuongeza thamani ya heroini umeingizwa nchini. Kilo 150 za heroini walizokamatwa nazo wasichana wawili wa Tanzania walipotua huko Afrika ya Kusini hivi karibuni zilitengenezwa na mtambo huo.
Serikali inajua kwamba wapo maelfu ya Watanzania walio katika magereza katika nchi mbalimbali duniani baada ya kubambwa na dawa za kulevya. Baadhi yao tayari wametaja majina ya magwiji wa biashara hiyo na kinachotakiwa sasa sio tu Serikali kuyafanyia kazi majina hayo, bali kuwafuata vijana walio katika magereza huko nje ili kupata taarifa za kina kuhusu mitandao hiyo.
Ukimya wa Serikali unatia shaka. Sasa yanahitajika mabadiliko makubwa katika uongozi wa viwanja vyetu vya ndege, vikosi vya ulinzi na usalama na mamlaka za kupambana na dawa za kulevya. Sisi tunadhani mpango wa Serikali kutaka kubadilishana wafungwa na nchi nyingine una ajenda ya siri, haufai.
Source:Mwananchi
Tanzania hakuna uongozi imara..ko hili tatizo halitoisha leo wala kesho
ReplyDelete