Akizungumza na NIPASHE ofisini kwake jana, DPP Eliezer Feleshi, alisema bado hajapata jalada lolote la uchunguzi wa Polisi kuhusu waliohusika kwenye sakata la kuruhusu dawa kupitishwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA).
Hata hivyo, alisema ili jalada hilo limfikie linatakiwa kupitia kwa Wakili Mkuu wa Serikali, Kanda ya Dar es Salaam.
“Jalada haliwezi kutoka moja kwa moja kwa Polisi uwanja wa ndege kuja kwangu, lazima kwanza lipitie kwa Wakili Mkuu wa Serikali, Kanda ya Dar es Salaam,” alisema.
Wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi, Kikosi cha Viwanja vya Ndege nchini, Deusdedit Kato, aliliambia gazeti hili kuwa jalada la matukio hayo lilishapelekwa kwa DPP kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Hata hivyo wakati akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu, Kato, alitoa ufafanuzi kwamba jalada hilo lilishapelekwa kwa Wakili Mkuu wa Serikali Kanda ya Dar es Salaam na siyo kwa DPP kama alivyokuwa amesema awali.
Kwa upande wake, Wakili Mkuu wa Serikali wa Kanda hiyo, Ponziano Lukosi, alithibitisha kupokea jalada hilo na kwamba kwa sasa wanalifanyia kazi kwa kuangalia iwapo kuna mapungufu yoyote au la.
Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa sheria haipaswi kuweka bayana iwapo jalada limepokelewa au la kutokana na masuala ya usalama kwani suala kama hilo linagusa maslahi ya watu kwa kuwa ni ya mabilioni ya fedha.
Aidha, kufuatia matukio mfululizo ya kukamatwa kwa watuhumiwa wa dawa za kulevya wanaodaiwa kuwa ni Watanzania kwenye viwanja vya ndege nje ya nchi wakipitia JNIA, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, wiki iliyopita alisema kuwa atalishughulikia suala hilo kama alivyofanya bandarini.
Alisema anafahamu kila kitu kuhusu matukio ya dawa za kulevya, lakini anasubiri mamlaka zilizo chini yake kama vile TAA na bodi yake, uongozi wa JNIA na Polisi, ili wafurukute kwanza kama alivyofanya bandarini kwa lengo la kupima utendaji wao wa kazi.
Hata hivyo bado ukimya umeendelelea kutanda katika Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (TAA) kwa kushindwa kuzungumzia lolote kuhusiana na kushamiri kwa vitendo hivyo kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyere (JNIA).
Wiki iliyopita, Mkurugenzi wa TAA, Suleiman Suleiman aliahidi kuzungumzia suala hilo kupitia gazeti hili lakini cha kushangaza baada ya mwandishi wa habari hizi kwenda ofisini kwake alikataa kuzungumza na kwamba atafanya hivyo kwa waandishi atakapopata muda.
NIPASHE lilimpigia simu mkurugenzi huyo lakini ilikuwa inaita tu bila kupokelewa.
Kuhusu Watanzania waliokamatwa na dawa za kulevya Hong Kong, Shirikisho la Polisi la Kimataifa (Interpol) nchini, jana lilisema kuwa bado hawapewa taarifa rasmi.
Julai 5, mwaka huu wasichana wawili wa Kitanzania walikamatwa nchini Afrika Kusini wakiwa na dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine kilo 150 zenye thamani ya Sh. bilioni 6.8, zilizokuwa zikisafirishwa kutoka Tanzania.
Wasichana hao ambao ni Agness Gerald (25) na Melisa Edward (24), walikamatwa nchini humo katika Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, uliopo eneo la Kempton Park.
Siku kadhaa baadaye, taarifa kutoka Hong Kong, zilieleza kwamba maofisa ushuru wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Hong Kong (HKIA), walimkamata kijana mwenye umri wa miaka 25 akitokea Tanzania akiwa na dawa na za kulevya aina ya heroine kilo 1.6 zenye thamani ya Sh. bilioni 1.5 kwenye mzigo wake wa mkononi.
Taarifa zinaeleza zaidi kwamba, maofisa hao jioni siku hiyo hiyo walimkamata Mtanzania mwingene mwenye umri wa miaka 45 ambaye alipelekwa hospitali na kutolewa gramu 240 za dawa aina ya heroine. Mbali na hilo, pia Mtanzania mwingine mwenye miaka 28 alikamatwa akiwa na kilo 2.03 za cocaine.
Source:Nipashe